1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Lavrov: Nchi za magharibi zinaurefusha mzozo wa Ukraine

13 Julai 2023

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi ameyalaumu mataifa ya magharibi kwa kurefusha vita nchini Ukraine akionya mzozo huo hautafikia mwisho hadi Marekani na washirika wake watakapoipa kisogo mipango ya kuishinda Urusi.

https://p.dw.com/p/4TobZ
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Russian Foreign Ministry via REUTERS

Sergei Lavrov, mwanadiplomasia mkuu wa Urusi, ametoa matamshi hayo kwenye mahojiano na gazeti moja la Indonesia akisema nchi za magharibi zinaendelea kuipatia Ukraine silaha nzito nzito zinazomwongezea ujasiri rais Volodymyr Zelensky kuendelea kupigana.

Mahojiano hayo yamechapishwa wakati Lavrov akiwa nchini Indonesia kuhudhuria mkutano wa mwaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya kusini mwashariki mwa Asia, ASEAN.

Amesema mwenendo huo ndiyo chanzo cha kutofikia mwisho kwa vita vinavyoendelea na ametahadharisha kuwa mzozo utakuwa wa muda mrefu hadi pale mataifa ya magharibi yatakapoondoa mawazo na mipango ya kutaka kuidhibiti na kuishinda Urusi kupitia Ukraine.

Lavrov ameyakosoa mataifa hayo kwa kupuuza mapendekezo ya mpango wa amani kutoka mataifa yanayoendelea na badala yake yanazidisha viwango vya silaha yanayozituma Ukraine.

Amesema mpango wa amani wa rais Zelensky wa kuitisha na kuipa amri Urusi hautafanya kazi.

Lavrov atahadharisha juu ya mipango ya kuipatia Ukraine ndege chapa F16

Ndege ya kivita chapa F16
Ndege za kivita chapa F16 zina uwezo wa kubeba silaha za nyuklia. Picha: U.S. Air Force/Staff Sgt. David Salanitri via ABACA/picture alliance

Katika hatua nyingine Lavrov amesema nchi yake itazingatia kuwa imo katikati ya kitisho cha nyuklia iwapo mataifa ya magharibi yataipatia Ukraine ndege za kisasa za kivita chapa F16.

Serikali mjini Kyiv imekuwa ikisisitiza kupatiwa ndege hizo mamboleo kama msaada kutoka kwa washirika wake ili kupambana na Urusi.

Ingawa hadi sasa hakuna idhini iliyotolewa kwa ndege hizo kupelekwa Ukraine, Lavrov amesema pindi hilo litaafikiwa, Urusi haitapuuza uwezo wa ndege hizo kubeba silaha za nyuklia na kwa hivyo Moscow italizingatia hilo kuwa kitisho cha  wazi cha nyuklia.

Zelensky asifu ahadi za silaha wakati Kyiv ikipambana na hujuma za Moscow

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine
Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine Picha: Sean Gallup/Getty Images

Wakati Moscow ikilalamika juu ya msaada zaidi wa silaha unaotolewa kwa Ukraine, kiongozi wa nchi hiyo Volodymry Zelensky ameendelea kupokea ahadi chungunzima za shehena ya zana za kivita.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo akiwa njiani kurejea nyumbani baada ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami NATO uliomalizika jana nchini Lithuania, Zelenksy amesema amepata matokeo mazuri wakati wa safari hiyo.

"Tunarudi nyumbani tukiwa na matokeo mazuri kwa nchi yetu na muhimu zaidi kwa mashujaa wetu. Nyongeza kubwa ya silaha. Hiyo inajumuisha mifumo ya ulinzi wa anga, makombora, magari ya kivita na mizinga. Pia ni muhimu kwamba kwa mara ya kwanza tangu uhuru tumeunga msingi wa usalama kwa Ukraine kuelekea kujiunga na NATO”, amesema kiongozi huyo.

Nchini Ukraine kwenyewe maafisa wa nchi hiyo wamearifu mapema leo asubuhi kuwa mifumo yao ya ulinzi imeangusha ndege 20 zisizo na rubani zilizorushwa na Urusi zikiulenga mji mkuu Kyiv.

Watu wanne wamejeruhiwa baada ya mabaki ya ndege hizo kutawanyika na kuanguka kwenye maeneo manne tofauti ya mji huo mkuu.

Hujuma hizo za Moscow zilianza majira ya usiku wa manane na mirindimo ya makombora ilisikika kwa uzito kwenye viunga vya mji huo.