1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Uhispania yaishinda Ufaransa 2-1 kufika fainali ya EURO 2024

10 Julai 2024

Uhispania imetoka nyuma na kuishinda Ufaransa mabao 2-1 katika uwanja wa Alianz Arena mjini Munich, na kutinga fainali yao ya kwanza ya michuano mikubwa katika kipindi cha miaka 12

https://p.dw.com/p/4i56n
Wachezaji wa Uhispania washerehekea ushindi wao uwanjani Alianz Arena mjini Munich baada ya mechi ya nusu fainali kati yao na Ufaransa mnamo Julai 9,07.2024
Wachezaji wa Uhispania washerehekea ushindi wao uwanjani Alianz Arena mjini Munich Picha: Michaela Stache/REUTERS

Kikosi cha Kocha Didier Deschamps kilitangulia mbele kupitia bado lililofungwa na Randal Kolo Muani lakini Lamine Yamal alisawazisha muda mfupi baadae na kuwa mgungaji kinda zaidi katika historia ya michuano hiyo, huku bao la Dani Olmo katika dakika ya 25 likiihakikishia ushindi Uhispania.

Uhispania ni timu ya kwanza kushinda mechi sita michuano ya Euro

Mabingwa mara tatu Uhispania wamekuwa timu ya kwanza kushinda mechi sita kwenye Michuano ya Euro na wamebakiza mchezo mmoja kushinda taji la kuvunja rekodi la nne.

Soma pia:Uhispania na Ufaransa kutunishiana misuli nusu fainali ya EURO 2024

Maswali yataulizwa namna Wafaransa, ambao wamefika fainali mara tatu katika michuano minne iliyopita, wameshindwa kutambaa mbele ya Uhispania licha ya kujivunia vipaji vikubwa vya ushambuliaji.

Ufaransa walikuwa wamefunga mabao matatu tu kuelekea mechi hiyo, na kati ya hayo hakuwa hata moja lililofungwa na mchezaji wa Ufaransa kwenye mchezo wa wazi na kocha Didier Deschamps alishughulikia hali hiyo kwa kumuweka benchi fowadi Antoine Griezmann na kumuingiza Ousmane Dembele.

Soma pia:Euro2024: Uhispania yawatoa wenyeji Ujerumani robo fainali

Yamal alitengeeza nafasi ya kwanza ya mechi hiyo dakika nne baada ya mchezo kuanza, kwa krosi ya juu iliyomfikia Fabian Ruiz, ambaye kichwa chake kilikwenda juu ya lango la Ufaransa. Dakika nne baadaye, Mbappe alimpigia krosi Kolo Muani, ambaye alifunga bao lililoipa uongozi Ufaransa.

Lamine Yamal mfungaji kinda zaidi katika historia ya michuano ya EURO
Lamine Yamal mchezaji kinda wa UhispaniaPicha: Leonhard Simon/REUTERS

Wakati mashaka ya kabla ya mechi yaliwalenga wakongwe wa Uhispania Jesus Navas mwenye umri wa miaka 38, na Nacho mwenye miaka 34, ambao walichukua nafasi za Dani Carvajal na Robin Le Normand, vijana Aymeric Laporte na Marc Cucurella walifanya makosa yaliochangia bao la kwanza la Kolo Muani.

Yamal ni mfungaji mdogo zaidi katika historia ya EURO

Bao la Ufaransa lilionekana kuondoa upepo kwa Uhispania lakini alikuwa mchezaji mdogo zaidi uwanjani aliefunga bao maridadi kabisaa  la kusawazisha.

Bao hilo lilimfanya Yamal, ambaye tayari amesaidia mabao matatu kwenye michuano ya Euro 2024, kuwa mfungaji mdogo zaidi katika historia ya mashindano hayo, akiipiku rekodi ya awali kwa mwaka mmoja na nusu.

Soma pia:Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa dhidi ya Austria

Bao la Lamal, dakika 13 baada ya bao la kwanza la Ufaransa, liliamsha mashambulizi ya Uhispania na vijana hao wa La Roja walipata bao la kuongoza dakika nne baadaye kupitia kwa Olmo.

Nafasi bora zaidi kwa Ufaransa ya kulazimisha muda wa nyongeza iliangukia kwa nahodha wao zikiwa zimesalia dakika tano, lakini Mbappe alipiga shuti lake juu akiwa amebaki na kipa Unai Simon pekee.

Uhispania walikuwa bora 

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps, amekiri kuwa Uhispania walikuwa bora licha ya vijana wake kutangulia kufunga bao.

Hapo kesho England itacheza dhidi ya Uholanzi katika mechi ya pili ya nusu fainali, itakayoamua nani ataungana na Uhispania siku ya Jumapili mjini Berlin.