1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtazamo wa Putin kuhusu historia ya Ukraine

Daniel Gakuba
25 Februari 2022

Muda umewadia, Urusi imeivamia Ukraine. Putin pia ametumia historia kuweka madai yake juu ya Ukraine. Lakini madai hayo yana ukweli kiasi gani? DW inachambua.

https://p.dw.com/p/47cIY
Russland Moskau | Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin, tarehe 21 Februari akitoa mtazamo wake juu ya historia ya UkrainePicha: Alexey Nikolsky/AFP

 

Mzozo kati ya Ukraine na Urusi ulichukua sura mpya Jumatatu ya Februari 21, wakati rais wa Urusi Vladimir Putin alipotumia hotuba yake ya zaidi ya saa nzima kutambua uhuru wa ''Jamhuri za watu'' wa Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine. Alizungumza mengi, akitoa somo la historia ya Ukraine, baadhi ya sehemu akiitunga upya, kulingana na mtazamo wake. 

Madai ya Putin: ''Ukraine ya leo iliundwa na Urusi''

''Ukraine kama ilivyo leo iliumbwa na Urusi, ili ieleweke zaidi, iliundwa na Bolsheviki, Urusi ya kikomunisti,'' alidai rais wa Urusi. ''Mchakato huu ulianza mara tu baada ya mapinduzi ya 1917, Lenin na washirika wake waliigawanya ardhi ya taifa la kihistoria la Urusi. Hakuna aliyewauliza mawazo yao mamilioni ya watu walioishi kule.'' Aliongeza.

Uhakiki wa DW: Sio kweli

Kulingana na Putin, Lenin ndiye aliyeiunda Ukraine. Kwa mtazamo wake, Kuipa Ukraine hadhi ya jamhuri katika Muungano wa Kisovieti, lilikuwa kosa baya sana.

Rais huyo wa Urusi anarejelea sera ya utaifa ilivyokuwa mnamo miaka ya mwanzo ya Muungano wa Kisovieti chini ya uongozi wa Lenin. Watu wasio Warusi pembezeno mwa muungano huo walipewa aina fulani ya uhuru katika masuala ya lugha, utamaduni na uongozi.

Hata hivyo, Ukraine ya wakati huu haikuumbwa na Urusi kuwa taifa, Jamhuri ya Watu wa Ukraine ilikuwepo kwa takribani miaka miwili kabla ya kutekwa na 'jeshi jekundu' mwaka 1920. Hayo yalikuwa matunda ya juhudi za watu wa Ukraine kutaka uhuru ndani ya himaya ya Urusi, ambayo Ukraine ya sasa ilikuwa sehemu yake hadi mwaka 1917. Eneo ilipo Ukraine lilikwenda upande wa ufalme wa Austro-Hungarian hadi mwaka 1918 na likapata uhuru mwaka 1919.

Mtaalamu wa historia ya Ulaya Mashariki Guido Hausmann anaeleza kuwa, ingawa sio kwa hali ya kudumu, kuundwa kwa taifa la Ukraine kulitokea baada ya vita vikuu vya kwanza, na sio kwa hisani ya Urusi.

Ukraine Russland Konflikt | prorussische Demonstrationen in Donezk
Sanamu ya Vladimir Lenin, mwasisi wa Muungano wa KisovietiPicha: Alexander Ryumin/TASS/dpa/picture alliance

Mwanahistoria mwingine Joachim von Puttkamer anasema Putin ameshindwa kabisa kutambua kuwa utaifa wa Ukraine ulikuwepo mwanzoni mwa Muungano wa Kisovieti na hata baada yake. Anasema dhana kwamba Ukraine ni taifa bandia lililoundwa na Urusi ya Wakomunisti ni ujinga, ukitilia maanani vuguvugu la muda mrefu la utaifa wa Ukraine.

Puttkamer ambaye ni mwenyekiti wa masuala ya historia ya Ulaya Mashariki katika chuo kikuu cha Friedlich Schiller mjini Jena, anasema Lenin alichukuwa uamuzi kwa kufuata vuguvugu la kutaka kuundwa kwa utaifa wa Ukraine, kwa hiyo siyo yeye alieiumba.

Madai ya Putin: Ukraine haijawahi kuwa na historia ya utaifa thabiti

Katika hotuba ya Putin wikei hii, alidai kuwa Ukraine haijawahi kuwa na utaifa thabiti. Alisema baada ya kusambaratika kwa Muungano wa Kisovieti mwaka 1991, Ukraine ilifuata bila kufikiria mfumo wa kigeni wa uongozi ambao hauna misingi yoyote katika uhalisia wa historia yake.

Uhakiki wa DW: Huu ni upotoshaji

Anachomaanisha rais wa Urusi kuhusu ''Utaifa thabiti'' bado kina utata, na si rahisi kuitolea hukumu kauli hiyo ya Putin. Lakini, kama ilivyoelezwa juu, utaifa wa Ukraine ulikuwepo kabla ya Umoja wa Kisovieti. Ingawa haukudumu kwa muda mrefu, bali miaka miwili tu. Haikudumu kwa sababu Muungano wa Kisovieti haukuiruhusu, iliimeza Jamhuri ya Watu wa Ukraine.

Hata mtu akiichimbua historia, kuna kipindi kingine cha uhuru wa Ukraine kati ya utawala wa Poland (kuanzia karne ya 14 hadi ya 15) na utawala wa Urusi (kuanzia karne ya 18 hadi mwaka 1917): Mwaka 16438, Wakosak walilikomboa karibu eneo zima la Ukraine kutoka ufalme wa Poland na Lithuania, na kuunda utawala wa shirikisho uliojulikana kama Hetmanate ambao ulidumu kwa miaka 100.

Kitu kingine muhimu kisiasa kabla ya utawala wa Poland, mnamo enzi za kati za historia, ni himaya ya Waslavik ya Kievan Rus. Himaya hiyo ilijumuisha mataifa ya leo ya Ukraine, Belarus na Urusi, kwa hiyo, yote matatu yana chimbuko katika ufalme wa Kievan Rus.

Guido Hausmann ambaye ni mkuu wa kitengo cha historia katika taasisi ya utafiti ya Leibnitz kwa ajili ya Ulaya mashariki na kusini iliyoko Regensburg, anaeleza: ''Hoja ya Urusi ni kwamba huo ulikuwa mwanzo wa utaifa wa Urusi. Kwa upande mwingine, Ukraine inauona kama mwanzo wa utaifa wake. Haya madai ''yanayokinzana ya urithi wa zama za kale''  huchunguzwa pia kwa njia tofauti, anasema Hausmann. Kilicho dhahiri ni kwamba zama hizo Ukraine haikuwa sehemu ya Urusi.

Kwa vyovyote vile, katika historia eneo la Ukraine ya sasa liliwahi kuwa sehemu ya mataifa mengine. Lakini, mataifa mengine ya leo kama Ujerumani yamepitia njia kama hiyo. Ni kwa maana hiyo kwamba hoja ya Putin ya kukanusha utaifa wa Ukraine haina nguvu.

Licha ya kwamba Ukraine ina mizizi mirefu ya mafungamano ya kihistoria na Belarus na Urusi kuanzia zama za kati, vuguvugu la muda mrefu la utaifa wa Ukraine haliwezi kupuuzwa. Na mwisho, Ukraine imekuwa taifa huru kwa miongo mitatu iliyopita baada ya kusambaratika kwa Muungano wa Kisovieti. Mchakato wa kuondoka katika muungano huo na kujitangazia uhuru, ulipopigiwa kura ya maoni mwaka 1991, ulipata ushindi wa kishindo wa asilimia 90 ya kura.

 https://www.dw.com/a-60895811