1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendeleza uvamizi Ukraine katika "siku ya giza" Ulaya

Daniel Gakuba
24 Februari 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema rais wa Urusi Vladimir Putin amefanya kosa kubwa kwa kuivamia Ukraine. Serikali ya Ukraine imeripoti mashambulizi ya wanajeshi wa Urusi katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/47Y7j
Ukraine Konflikt | Russischer Militärangriff
Picha: AFP

Ripoti za hivi punde zinaeleza kuwa wanajeshi wa Urusi wamevamia maeneo ya kusini, kaskazini na mashariki mwa Ukraine, na kuna taarifa za vifo katika kambi za kijeshi na miripuko karibu na miji kadhaa mikubwa nchini Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imeiharibu miundombinu 74 ya kijeshi ya juu ya ardhi nchini Ukraine, vikiwemo viwanja 11 vidogo vya ndege, hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la RIA.

Soma pia: Maoni: Putin ametangaza vita

Polisi ya Ukraine imesema Urusi imefanya mashambulizi zaidi ya 200, naye naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine amesema baadhi ya Warusi wameshikwa mateka katika mapigano makali mashariki mwa Ukraine.

Ukraine Konflikt | Ukrainische Streitkräfte
Wanajeshi wa Ukraine wakijiandaa kukabiliana na mashambulizi ya Urusi katika mkoa wa Lugansk, Februari 24, 2022.Picha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Wizara ya ulinzi mjini Kiev pia imethibitisha kuwa wanajeshi wake wapatao 40 wameuawa katika mashambulizi ya Urusi.

Mjini Kiev ving'ora vya tahadhari vimekuwa vikisikika, na watu wamejazana katika vituo vya treni wakijaribu kuuhama mji huo. Wengine wanatumia njia ya barabara ambapo msongamano mkubwa wa magari unashuhudiwa.

Soma pia:Putin atangaza operesheni za kijeshi Ukraine

Poland ambayo ni jirani wa Ukraine Upande wa magharibi, imeandaa treni za kuwasaidia wakimbizi kutoka Ukraine na kuweka vituo vya kuwapokea.

Pande mbali mbali zimelaani mashambulizi haya ya Urusi. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema leo ni siku ya giza kwa Ulaya kutokana na mashambulizi hayo, na kumuonya rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba amefanya kosa kubwa.

Janga barani Ulaya

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Putin ameamua kufuata njia ya damu kwa kuamuru mashambulizi dhidi ya Ukraine, ambayo Johnson ameyaita janga kwa bara Ulaya.

Deutschland Berlin | Olaf Scholz, Bundeskanzler | Statement Ukraine-Russland
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Putin amefanya kosa kubwa sana kwa kuanzisha uvamizi dhidi ya Ukraine.Picha: Michael Kappeler/AFP/Getty Images

Tayari Marekani imepeleka iwanajeshi wapatao 800 katika ukanda wa Baltiki unaopakana na Urusi, wakiwa na ndege za kivita.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemtaka Rais Putin kuima nafasi amani, lakini katibu mkuu wa Umoja wa Kujihami wa NATO Jens Stoltenberg amesema wito huo wa Guterres hauna nafasi tena kwa sababu amani barani Ulaya imekwishavunjwa.

Soma pia: Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine

Mjini Washington, Rais Joe Biden anafanya mkutano wa dharura na washauri wake wa masuala ya usalama.

Stoltenberg ambaye jumuiya anayoiongoza ina ndege za kivita zipatazo 100 na manowari 120 zilizo tayari kwa vita, amesema yeyote asihadaike kwamba NATO haitahakikisha usalama wa wanachama wake. Ukraine sio mwanachama wa Jumuiya hiyo.

China kwa upande wake imesita kukiita kilichofanywa na Urusi kuwa ni uvamizi dhidi ya Ukraine, badala yake imezitaka pande zote katika mzozo huu kujizuia.

Hakuna juhudi kubwa za kidiplomasia zinazoendelea kwa wakati huu. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amezitaka nchi washirika kuvunja uhusiano wa kibalozi na Urusi, lakini Urusi imezionya nchi hiyo dhidi ya kuchukuwa hatua kama hiyo.

Chanzo: ape, rtre