1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa:Wapiga kura wakumbwa na hofu ya virusi vya corona

Zainab Aziz Mhariri:Sylvia Mwehozi
15 Machi 2020

Ufaransa inaelekea kupiga kura leo hii Jumapili lakini kuongezeka kasi ya kusambaa virusi vya corona kote nchini humo kunaweza kusababisha wapiga kura kuogopa kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

https://p.dw.com/p/3ZRxi
Coronavirus Symbolbild
Picha: Reuters/D. Ruvic

Wapiga kura watawachagua mameya wa mabaraza 35,000 ya miji, vijiji na mji mkuu wa Paris na karibu madiwani nusu milioni katika uchaguzi unaofanyika wakati huu wa mlipuko wa virusi vya corona na pia wakati ambapo wasiwasi umeongezeka nchini Ufaransa juu ya siasa za nchini humo.

Wakati huo huo Ufaransa na Uhispania zimetangaza hatua za dharura na kuzifunga huduma kadhaa ili kuzuia kuenea virusi vya COVID 19. Ufaransa itafunga maduka, mikahawa na sehemu za burudani kuanzia leo Jumapili na watu wapatao milioni 67 wanaoishi nchini humo wametakiwa wakae nyumbani kama hatua mojawapo ya kusaidia kupambana na virusi vya corona vinavyo sambaa kwa haraka ambapo idadi ya watu walioambukizwa nchini humo imeongezeka mara mbili katika muda wa saa 72. 

Waziri Mkuu Edouard Philippe amesema serikali ya Ufaransa haina jinsi nyingine isipokuwa kuchukua hatua ya namna hiyo baada ya idara ya afya ya umma kutangaza kuwa watu 91 wamekufa na karibu watu 4,500 wameambukizwa hadi kufikia sasa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/L. Marin

Nchini Ujerumani mamlaka ya mji mkuu, Berlin na ya jiji la Cologne katika jimbo la North Rhine Westfalia  zimetangaza kufungwa  baa, vilabu vya starehe, majumba ya sinema na kumbi za matamasha wakati ambapo Ujerumani inaongeza juhudi za kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi hivyo vya COVID 19. Kuanzia sasa hafla yoyote inayowahusisha watu 50 au zaidi katika mji wa Berlin imepigwa marufuku.

Uhispania, imechukua hatua za dharura ili kuzuia kuenea kwa virusi vya COVID 19 imewataka watu wake wapatao milioni 46 kubaki majumbani wakati ambapo nchi hiyo imethibitisha watu 6,391 kuwa wameambukizwa idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la watu 600 tangu Jumamosi. Watu 195 wameshafariki kutokana na homa inayosababishwa na virusi vya corona nchni Uhispania.

Katika hotuba yake kupitia kwenye runinga kwa taifa, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alielezea kuhusu hatua ya hali ya dharura ya wiki mbili iliyotangazwa kwa ajili ya kupambana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Mipaka zaidi imefungwa kote ulimwenguni huku rais wa Marekani Donald Trump akitangaza kwamba Marekani ambayo siku chache zilizopita iliweka marufuku ya wasafiri kutoka nchi kadhaa za Ulaya na sasa marufuku hiyo itazihusu pia Uingereza na Ireland ambazo hapo awali zilikuwa hazimo.

Wakati huo huo, China, ambapo virusi vya corona vilikoanzia mwishoni mwa mwaka jana,imeeendelea kulegeza vizuizi vyake hali hiyo ikiashiria kwamba kitovu cha virusi hivyo sasa kimehamia katika nchi za Ulaya magharibi. Zaidi ya watu 150,000 wameambukizwa virusi vya COVID 19 ulimwenguni kote na zaidi ya 5,600 wamekufa kutokana na homa inayosababishwa na virusi hivyo.

Vyanzo:/RTRE/AP