1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EURO 2024: Ufaransa yalazimishwa sare ya 0-0 na Uholanzi

24 Juni 2024

Ufaransa imeshindwa kutamba mbele ya Uholanzi baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana. Ufaransa ilicheza bila ya nyota wake Kylian Mbappe ambaye ni majeruhi aliyekuwa akiitiazama mechi hiyo akiwa benchi.

https://p.dw.com/p/4hNdS
Euro 2024  Timu ya Taifa ya Ufaransa
Kikosi cha Ufaransa kilichoshindwa kutamba mbele ya Uholanzi na kutoka sare ya bila kufunganaPicha: Kai Pfaffenbach/REUTERS

Nahodha msaidizi wa Ufaransa, Antoine Griezman alishindwa kuzitumia vyema nafasi za wazi wazi, huku bao la Xavi Simons wa Uholanzi nalo likikataliwa na kuifanya mechi hiyo kuwa ya kwanza kumalizika bila ya kufungana tangu michuano hii ilipoanza.

Matokeo haya yanazifanya timu hizo mbili kubakia na pointi nne kila moja katika kundi D baada ya mechi za mzunguko wa pili. Poland ndio itaanza kuyaaga mashindano hayo kwenye kundi hili baada ya kufungwa mabao 3-1 na Austria katika mechi ya jana jioni na kuendelea kushika mkia. Na hata kama itaifunga Ufaransa katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, bado haitakuwa na nafasi ya kusonga mbele.

Soma pia: Ujerumani yawa ya kwanza kufuzu duru ya mtoano

Uholanzi itakwaana na kisiki Austria ambao wameonyesha mchezo mzuri katika mechi zake za awali.

Euro 2024  Uholanzi dhidi ya Ufaransa
Kyilian Mbappe akionekana kabla ya mechi kati ya Ufaransa na Uholanzi kwenye michuano yaEuro 2024 katika uwanja wa LeipzigPicha: REUTERS

Minong'ono ilihanikiza kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, ikiwa Mbappe atacheza na hasa kutokana na majeraha ya pua aliyoyapata kwenye mechi iliyopita ya ufunguzi dhidi ya Austria, ambapo Ufaransa iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mbappe siku ya Alhamisi alionekana mazoezini akiwa amevaa barakoa na kocha wa Ufaransa Didier Dechamps alikuwa na matumaini kwamba angeweza kucheza. Lakini Dechamps baadae alisema haoni sababu ya kumtia hatarini Mbappe kwa kumchezesha kwenye mechi ambayo hawakulazimika sana kushinda.

Ufaransa, ilikosa nafasi kama tatu za wazi katika kipindi cha pili, baada ya Aurélien Tchouaméni, Griezmann na Ousmane Dembele kushindwa kupenya kwenye lango la Uholanzi lililodhibitiwa na Bart Verbruggen.

Katika dakika ya 69, Xavi alipiga shuti maridadi lililompita kipa wa Ufaransa Mike Maignan, ingawa hata hivyo goli hilo lilikataliwa baada ya kubainika kwamba Denzel Dumfries alikuwa ameotea na kumzuia Maignan kuokoa shuti hilo la Xavi.

Griezman amekiri baada ya mechi hiyo kwamba alikuwa na nafasi nzuri za kuifungia timu yake na kusema ilikuwa ni aibu kubwa kushindwa kufunga licha ya kuwa na mpira tena karibu na goli. Amesema walikuwa imara katika safu ya ulinzi na hata kimbinu, lakini walichoshindwa ni kufunga goli.

EURO 2024 Uholanzi dhidi ya Ufaransa
Mashabiki wa Uholanzi waliojitokeza kwenye mechi kati ya timu yao na Ufaransa katika mji wa LeipzigPicha: Mahmut Serdar Alakus/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Ufaransa yaisambaratisha Uholanzi 4-0

Mbappe naye anakiri kwamba Ufaransa ilishindwa kutumia nafasi walizopata na kusema kuwa cha msingi kwao kwa sasa ni kuhakikisha wanacheza vizuri zaidi ili kushinda. Naye amekiri kwamba walitengeneza nafasi nzuri lakini walishindwa kuzitumia ili kuondoka na ushindi. Mbappe akasema kuna namna wanahitaji kujirekebisha.

Kwa upande wa Uholanzi ni kilio kitupu. Nahodha wake Virgil van Djik alilalama kamba walinyimwa bao lililofungwa na Xavi. Akasema Ufaransa walikuwa na nafasi zao, na wao pia walikuwa na nafasi moja ama mbili za kufunga.

Mashabiki wa Uholanzi walifurika pomoni kwenye uwanja wa Leipzig na mji wa Leipzig ulifunikwa na rangi ya chungwa kabla ya mechi hiyo. Licha ya mashabiki wa Ufaransa kujitutumua, lakini hawakufua dafu. Inasemekana mmoja ya mashabiki wa Ufaransa alikwenda na jogoo uwanjani hapo usiku wa kuamkia siku ya mechi. Haikuwa wazi ikiwa jogoo huyo naye alikua na tiketi ya kutazama mechi.

Kwenye mechi ya awali ya kundi D, Austria ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Poland ambayo kimsingi tayari imeyaaga mashindano hayo ya Euro 2024, licha ya kumchezesha nahodha wake Robert Lewandowski.