1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aitaka serikali kutoa huduma bora kwa raia Kongo

Mitima Delachance27 Aprili 2023

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi ameitahadharisha serikali kuzidisha juhudi ili kutumikia raia inavyostahili akitarajia matokeo mazuri ya serikali hiyo miezi michache kabla ya uchaguzi

https://p.dw.com/p/4QcsK
Felix Tshisekedi
Picha: Boniface Muthoni/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Lakini upinzani katika jimbo la Kivu Kusini umeikosoa sera ya serikali na unaamini kuwa kile ambacho hakikufanyika katika miaka minne tangu Tshisekedi kuingia madarakani hakiwezi kufanyika tena katika miezi michache iliyosalia. 

Félix Tshisekedi ametoa onyo hilo katika hotuba yake mbele ya mawaziri hapo jana mjini Kinshasa alipofunga warsha ya kuwaongezea ujuzi zaidi wajumbe wa serikali ya Kongo. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha mshikamano madhubuti kati ya wajumbe wa serikali na kuwapa mwelekeo wa mabadiliko kupitia uongozi na usimamizi bora wa masuala ya umma kwa kuzingatia utekelezaji mzuri wa mpango wa serikali. Tshisekedi amewataka kufanya juhudi zote ili wafanikishe mpango wa serikali kwa ajili ya maendeleo ya mitaa mia moja na arobaini na tano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Soma pia: Jamhuri ya kidemokrasioa ya Kongo yafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri

""Ni kwa sababu hiyo nilimwomba Waziri Mkuu atoe maagizo kwa kila mmoja wenu kuhusu mpango huu wa Serikali, kuweka vipaumbele kwa vitendo vyenye matokeo ya kweli na yanayoonekana kwa kuzingatia matarajio ya wananchi wetu, na kufanya kazi kwa ufanisi ili kutekeleza majukumu yenu. Kwa ajili hiyo, taratibu zinapaswa kuwekwa ili kuhakikisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango wa serikali. Kwa hivyo Mnaweza kutegemea kwamba nawaunga mkono. Sina shaka kwamba mtafanikiwa kutumia kanuni zinazohakikisha uwiano wa utekelezaji wa mpango huu wa maendeleo ya mitaa mia moja na arobaini na tano ya Congo, mpango wa kina wa maono yangu kulingana na azma yangu ya kujenga nchi yenye nguvu, ustawi, na umoja. Mumefunzwa pia mambo muhimu yanayohusiana na utawala na uchumi”

Soma pia: Tshisekedi amrejesha Jean-Pierre Bemba serikalini

Kwa fursa hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jean-Michel Sama Lukonde alisisitiza azma ya serikali yake kuongeza juhudi za kuimarisha mfumo wa usalama wa nchi yake ili kukabiliana na ukosefu wa usalama Mashariki ya Congo. Sama Lukonde alikumbusha pia dhamira ya serikali ya kuhakikisha Congo inaheshimiwa nje ya mipaka yake, na alizungumzia pia kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya biashara nchini Congo. Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde amesema:

"Kufanya kazi kwa ajili ya nchi yenye ustawi kunahitaji serikali kufanya jitihada kubwa za kuunganisha, kuleta utulivu na kuhifadhi mfumo wa uchumi mkuu katika kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi ya nje na ya ndani. Katika hivyo, serikali italazimika kufanya kazi kwa mvuto bora wa nchi, haswa kwa uboreshaji wa mazingira ya biashara. Mwishowe, kujenga serikali iliyoungana kunamaanisha mchanganyiko wa juhudi zote za serikali kwa nia ya kufikia lengo moja la kuboresha hali ya maisha ya watu wetu”.

Upinzani unamkosoa Rais Tshisekedi kwamba ameshindwa kwa kiasi kikubwa. Madeleine Menge ni mwanachama wa chama cha kisiasa cha PPRD cha Rais wa zamani Joseph Kabila. Anahisi kwamba hizo ni nia njema tu ambazo kamwe hazitatimia kwa sababu muda uliosalia kabla ya uchaguzi kufanyika Desemba ni mfupi sana:

Licha ya ukosoaji huu, Wakongo pia wamekosoa chama cha PPRD kwa kushindwa kutekeleza sera zake kadhaa wakati rais wazamani Joseph Kabila alipokuwa madarakani.