1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: CCM yaanza mchakato wa kutafuta spika mpya

George Njogopa 17 Januari 2022

Chama tawala nchini Tanzania CCM kinaanza vikao vyake kwa ajili ya kuchuja majina ya wagombea wa nafasi ya uspika wa bunge huku wagombea 71 wakijitokeza kuwania nafasi hiyo.

https://p.dw.com/p/45cvf
Tansania Wahlen 2020
Picha: picture-alliance/AP Photo

Jumla ya wagombea 71 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Kamati kuu ya chama hicho ndiyo yenye jukumu la kupitia majina ya wagombea hao ambao wamevunja rekodi kwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa wazi na spikaaliyejiuzulu Job Ndugai baada ya kutoa kauli  iliyokosolewa vikali na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kama alivyosema, katibu msaidizi wa CCM, Solomoni Itunda,kuwepo kwa wagombea wengi katika hatua hiyo ya kwanza, ni ishara ya kielelezo cha kuimarika kwa demokrasia ndani ya chama hicho.

Soma pia:

Upinzani Tanzania wakosoa utaratibu wa kujiuzulu kwa Ndugai

Job Ndugai amuomba radhi rais Samia na Watanzania

Ingawa katika majina ya waliojitokeza kuna wale wanaotazamwa kama wanasiasa waliojitosa kama kujaribu bahati tu, lakini baadhi ya majina kwenye orodhaa hiyo yanaonekana kuwa na nguvu zaidi na pengine yakawapa wakati mgumu wajumbe wa kamati kuu wanaokutana kuanzia leo.

Wachambuzi wa siasa za Tanzania wamekuwa na mijadala inayokinzana kimtazamo kuhusu kujitokeza kwa idadi kubwa ya wagombea kwenye nafasi hiyo inayotajwa kuwa ni nyeti.

Nafasi ya spika w abunge la Tanzania ilibaki wazi baada ya aliyekuwa spika Job Ndugai kujiuzulu, kufuatia kile kilichotizamwa kuwa tofauti kati yake na rais Samia Suluhu Hassan.
Nafasi ya spika w abunge la Tanzania ilibaki wazi baada ya aliyekuwa spika Job Ndugai kujiuzulu, kufuatia kile kilichotizamwa kuwa tofauti kati yake na rais Samia Suluhu Hassan.Picha: DW/E. Boniphace

Baadhi ya wachambuzi akiwemo John Kitoka, wanasema wagombea wengine kwenye kinyang'anyiro hicho wanajaribu kujipima namna wanavyokubalika kuelekea katika mbio za uchaguzi ndani ya chama na ule uchaguzi mkuu ujao wa 2025.

Spika ajaye huenda akakabiliwa na masuala mengi tete ikiwamo namna atavyomudu kushughulikia mjadala unaendelea kuhusiana na wabunge 19 wa kuteuliwa wanaodaiwa kuwakilisha Chadema. Chama hicho kimewakana wabunge hao na tayari kimeshawavua uanachama.

Ama masuala mengine ni namna atavyomudu kulifanya bunge linavyoendesha mambo yake kwa uwazi na kuteleleza jukumu lake la kutoingiliwa na mihimili mengine hasa muhimili wa serikali suala ambalo linatajwa lilijitokeza mara kwa mara wakati wa uongozi wa spika Ndugai.

Bunge lijalo limepangwa kuanza kukutana mapema mwezi Februari, na jukumu lake la kwanza litakuwa ni kufanya uchaguzi wa spika.