1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa Bunge la Tanzania amejiuzulu

Deo Kaji Makomba
6 Januari 2022

Spika wa Bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai amejiuzulu wadhifa wake kutokana na kutofautiana kwa kauli kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan.

https://p.dw.com/p/45DxM
Tansania Wahl des Premierministers Kassim Majaliwa
Picha: DW/H. Bihoga

Hatua iliyozua hali ya kile kinachoelezewa kuwa mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM. Akiwa Dodoma mwandishi wetu Deo Kaji makomba anayo ripoti kamili.

Hatua ya Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai kuamua kuachia ngazi katika nafasi hiyo kubwa katika moja muhimili nchini Tanzania inafuatia mashinikizo kutoka kwa wanachama wa chama tawala CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kumtaka spika huyo ajiuzulu kutokana na kwenda kinyume na Rais Samia baada ya Spika Ndugai kutoka hadharani na kupinga hatua ya Rais Samia kuchukua mikopo huku akidai mikopo itasababisha nchi kupigwa mnada.

Uamuzi wa kujiuzuli

Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Picha: DW/E. Boniphace

Katika barua yake ya kujiuzulu aliyoitoa kwa vyombo vya habari aliyomuandikia katibu wa CCM kujiuzulu nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba uamuzi huo ni hiari yake na amefanya kwa kuzingatia kujali masilahi mapana zaidi ya Taifa, serikali na chama cha CCM.

Ndugai kabla ya kuandika barua ya kujiuzulu alionekana kuponzwa na kauli yake aliyoitoa mwishoni mwa mwaka katika moja ya sherehe ya kabila la Wagogo huku akinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa nchi itapigwa mnada kutokana na mikopo inayochukuliwa na Rais Samia na siku chache badae Ndugai aliita wandishi na kumuomba msamaha Rais Samia na Watanzania kwa ujumla.

Fununu za Spika Ndugai kujiuzulu katika nafasi hiyo zilianza kusambaa tangu majira ya leo asubuhi na mnamo majira ya saa tisa mchana mbunge wa Kawe Askofu Gwajima alitoka hadharani mbele ya wandishi wa habari kumtaka Spika ndugai ajiuzulu.

 

Deo Kaji Makomba/DW