1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Job Ndugai amuomba radhi rais Samia na Watanzania

Deo Kaji Makomba
3 Januari 2022

Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai amejitokeza na kumuomba radhi Rais Samia Suluhu na Watanzania wote kufuatia kauli yake alioitoa kuhusu mikopo ya nchi.

https://p.dw.com/p/454no
Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Picha: DW/E. Boniphace

Akizungumza mbele ya wandishi wahabari Jijini Dodoma Spika Ndugai amesema kuwa hakuwa na nia mbaya wakati akitoa kauli hiyo na kwamba kauli yake ilihaririwa na baadhi ya watu wasio na nia njema wenye lengo la kumchonganisha na Rais

Amesema kuwa atakuwa amebeba dhambi kubwa kama atabeza juhudi za Rais ambaye ameweza kupata fedha nyingi kupitia mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku akiongeza kuwa hata Jimbo lake limenufaika kupitia fedha hizo za mikopo.

''Serikali ni baba yetu, serikali ni mama yetu.Tunahitaji serikali na tunaiunga mkono'',alisema Ndugai.

Soma piaSamia asisitiza kuwa serikali yake itaendelea kukopa:

''Nitumie fursa hii kumuomba radhi sana Mhe Rais na Watanzania wote''

Aidha Spika ndukai amesema kuwa anawasamehe wale wote waliorusha matusi kwake kutokana na kauli ya kichonganishi na kwamba yeye anabeba mzigo huo kwa kumuomba radhi Rais Samia pamoja na Watanzania wote.

''Binafsi yangu,popote pale ambapo nilihisiwa kama labda kwa namna moja ama nyingine nimetoa neno la kumvunja moyo rais wetu na akavunjika moyo. Nitumie fursa hii kupitia kwenu ( wandishi habari) kumuomba radhi sana mheshimiwa rais na kwa watanzania wote katika hali kama hii'', aliendelea kusema Ndugai.

Soma pia :Tanzania yaadhimisha miaka 60 ya Uhuru 

Mpasuko ndani ya CCM ?

Tansania Daressalam| Amtseinführung neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AFP/Getty Images

Katika siku za hivi karibuni Spika Job Ndugai alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akielezea kuwa Tanzania itapigwa mnada kutokana na mikopo mikubwa inayoendelea kuchukuliwa na serikali.

Kauli yake kuhusu Serikali kukopa, siyo tu kwamba imepishana na mtazamo wa Rais Samia Suluhu Hassan, bali pia inaonekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya baadhi ya wenyeviti wa chama hicho wa mikoa na jumuiya kujitokeza kumtetea Rais Samia, huku mitandao ya kijamii ikisheheni uvumi wa kila aina unaodai kuwepo na mpasuko ndani ya serikali na chama tawala.