1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yatangaza ushindi mkoa wa Panjshir

6 Septemba 2021

Taliban imetangaza ushindi dhidi ya vikosi vya upinzani katika mkoa wa mwisho wa upinzani wa Panjshir, na kukamilisha udhibiti wao wa Afghanistan, wiki tatu baada ya kuutwa mji mkuu wa Kabul. Waasi wasema vita bado.

https://p.dw.com/p/3zyGr
 Afghanistan | Taliban am Gouverneurssitz in Panjshir
Picha: Social media/handout/REUTERS

Kufuatia ushindi wao wa haraka na kushangaza dhidi ya vikosi vya usalama vya serikali ya zamani, na uondowaji wa wanajeshi wa Marekani baada ya miaka 20 ya vita, Taliban ilielekeza mapambano dhidi ya vikosi vinavyoulinda mkoa wa milimani wa bonde la Panjshir.

Afghanistan, Panjshir | Widerstandskämpfer gegen die Taliban bei einem militärischen Training
Wapiganaji wa vuguvugu la kuipinga Taliban wakifanya mazoezi ya kijeshi katika mkoa wa Panjshir, Agosti 30, 2021.Picha: Jalaluddin Sekandar/AP/picture alliance

Wakati kundi hilo likitangaza ushindi, msemaji wao mkuu, Zabihulla Mujahid akionya dhidi ya majaribio zaidi ya kupinga utawala wao, huku akiwahimiza pia wanajeshi wa zamani kujiunga na vikosi vya utawala wao.

''Kuhusu wale wanaosababisha machafuko na ukosefu wa usalama na wale wanaofanya mambo yanayotengeneza mazingira ya vita, Emarati ya Kiislamu ya Afghanistan inaguswa sana kwenye visa kama hivyo na kamwe haitaruhusu shughuli zinazokwenda kinyume na mfumo serikali na watu wa Afghanistan na maslahi yetu.''

Soma pia: Mapambano kuwania jimbo la Panjshir yaendelea Afghanistan

Picha iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na Taliban ilionesha wapiganaji wake wakiwa ofisi ya gavana wa mkoa wa Panjshir, ambao ulikuwa ngome ya upinzani dhidi ya vikosi vya Kisovieti mnamo miaka ya 1980, na Wataliban mwishoni mwa miaka ya 1990.

NRF yaapa kuendeleza mapigano

Kundi la National Resistance Front (NRF) mjini Panjshir, linaloundwa na wapiganaji wanaoipinga Taliban na wanajeshi wa zamani wa jeshi la Afghanistan, siku ya Jumapili lilikiri kupata hasara kubwa katika uwanja wa vita na kutoa wito wa kusitisha mapigano.

Afghanistan, Panjshir | Widerstandskämpfer gegen die Taliban bei einem militärischen Training
Wapiganaji wa NRF wasema bado wako kwenye maeneo ya kimkakati ndani ya bonde la Panjshir.Picha: Ahmad Sahel Arman/AFP/Getty Images

Leo Jumatatu kundi hilo limesema kupitia ujumbe wa Twitter kwamba wapiganaji wake walikuwepo bado katika maeneo ya kimkakati katika bonde hilo, huku likiapa kuendeleza mapigano.

NRF inajumlisha wapiganaji watiifu kwa  Ahmad Massoud, mtoto wa kamanda mashuhuri aliepambana dhidi ya Warusi na Taliban Ahmad Shah Massoud, pamoja na masalia wa jeshi la Afghanistan waliokimbilia bonde la Panjshir.

Soma pia:Vita vyapamba moto Panjshir kati ya Taliban na waasi 

Taliban bado hawajakamilisha utawala wao mpya baada ya kuingia Kabul wiki tatu zilizopita kwa kasi ambayo wachambuzi wanasema huenda iliwashangaza hata wao wenyewe.

Wakati wanaanza mabadiliko makubwa ya kuongoza taasisi muhimu na miji ya mamia kwa maelfu ya watu, Mujahid alisema serikali ya mpito itatangazwa kwanza, na kuruhusu mabadiliko baadae.

Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffith, amewasili Kabul kwa siku kadhaa za mikutano na uongozi wa Taliban, ambao umeahidi kusaidia, kwa mujibu wa taairifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, na kuthibitishwa na msemaji wa Taliban.

Ahmad Massoud
Kiongozi wa NRF, Ahmad Massoud.Picha: Mohammad Ismail/REUTERS

Jumuiya ya kimataifa inazidi kuukubali utawala mpya wa Taliban kupitia harakati za kidiplomasia. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa hii leo nchini Qatar, ambayo ni mdau muhimu katika kadhia ya Afghanistan.

Soma piaTaliban yasherehekea kuondoka kwa Marekani

Blinken atazungumza na Waqatari pamoja na Uturuki kuhusu kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Kabul, ambao ni muhimu kwa kusafirisha msaada wa kiutu na kuwaondoa wa Afghan waliobakia.

Kisha ataelekea nchini Ujerumani siku ya Jumatano, ambako atafanya mkutano wa video wa mawaziri 20 kuhusu mzozo huo pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas.

Chanzo: Agencies