1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuwakabidhi rasmi Taliban udhibiti wa Kabul

29 Agosti 2021

Kundi la Taliban watawala wapya wa Afghanistan, na wanajeshi wa Marekani wanaoihama nchi hiyo wameanza mipango ya makabidhiano ya uwanja wa ndege wa Kabul kwa njia za amani.

https://p.dw.com/p/3zdb1
Afghanistan Taliban Checkpiont am Flughafen Kabul
Picha: Wali Sabawoon/AP Photo/picture alliance

Afisa mmoja wa kundi la Taliban aliyezungumza na shirika la habari la Reuters siku ya Jumapili (Agosti 29) alisema kwamba walikuwa wanangojea kauli ya mwisho kutoka kwa wanajeshi wa Marekani ili waweze kuchukuwa udhibiti kamili wa uwanja huo wa ndege.

Alisema wanamgambo hao, ambapo walitwaa udhibiti wa mji mkuuu tarehe 15 Agosti baada ya kuvishinda nguvu vikosi vya serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na mataifa ya Magharibi, walikuwa na kikosi maalum cha wataalamu chenye wahandisi waliofuzu na walio tayari kuchukuwa udhibiti wa uwanja wa ndege.

Wakati Taliban wakijitayarisha kutwaa udhibiti kamili wa uwanja huo muhimu wa ndege nchini Afghanistan na ambao ni sehemu pekee iliyosalia kwenye mikono ya majeshi ya kigeni, ndege za mwisho za kijeshi za Uingereza ziliripotiwa kutuwa kwenye kituo cha jeshi nchini Uingereza zikiwa zimewabeba raia na wanadiplomasia kadhaa, zikihitimisha wiki mbili za operesheni ya kuwahamisha. 

Uingereza yakamilisha kukunja virago

Afghanistan | Soldaten aus Deutschland und den USA beobachten den Eingan zum Flughafen in Kabul
Wanajeshi wa Ujerumani na Marekani wakilinda uwanja wa ndege wa Kabul.Picha: Davis Harris/U.S. Marine Corps/Handout/REUTERS

Balozi wa Uingereza nchini Afghanistan, Laurie Bristow, alikuwa mmoja mwa wale waliowasili siku ya Jumapili (Agosti 29) kwenye uwanja wa kijeshi wa RAF Brize Norton ulio kaskazini magharibi ya London, masaa kadhaa baada ya serikali kutangaza kwamba wafanyakazi wote wa Kiingereza walishaondoka Kabul.

Uingereza inasema imewahamisha zaidi ya raia wake 15,000 na Waafghani 1,100 ambao walikuwa wako hatarini chini ya utawala mpya wa Taliban. Naibu Admirali Ben Key, ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza operesheni hiyo ya uhamishaji, alisema: "Tulijaribu kila tuwezalo."

Kwenye ujumbe wake kwa njia ya vidio, Waziri Mkuu Boris Johnson aliisifia operesheni hiyo akiita kuwa ni ya aina yake kuwahi kushuhudiwa katika siku za karibuni.

Johnson alaumiwa

Großbritannien | PK Boris Johnson zu COBR
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson: Tulikwenda Afghanistan kuisaidia na kuiunga mkono Marekani.Picha: Simon Dawson/Avalon/Photoshot/picture alliance

Hata hivyo, Johnson alikuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa kwa kushindwa kwake kuwahamisha Waafghani wote waliokuwa wakiwasaidia wanajeshi wa Kiingereza ndani ya kipindi cha kipindi cha miaka 20 ya kuwapo kwao nchini Afghanistan kulikoanza baada ya Mashambulizi ya 9/11.

Mwenyewe Johnson alikiri kwamba nchi yake "haikutaka kuondoka Afghanistan kwa njia hii" lakini alisema "tunapaswa kutambuwa kuwa tulikwenda huko na Marekani, kwa kuitetea na kuiunga mkono Marekani, na jeshi la Marekani ndilo lililoendesha sehemu kubwa ya mapigano."