1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Vita vyapamba moto Panjshir kati ya Taliban na waasi

4 Septemba 2021

Mapigano kati ya Taliban na vikosi vya upinzani yamepamba moto katika mkoa wa kaskazini wa Panjshir, ambapo mamia ya familia zimekimbia, wakati Taliban ikipambana kuchukuwa udhibiti wa ngome ya mwiso ya waasi.

https://p.dw.com/p/3zu87
Afghanistan, Panjshir  | Widerstand gegen die Taliban
Picha: Ahmad Sahel Arman/AFP/Getty Images

Wakazi wa maeneo jirani ya mkoa wa Parwan wanasema kwa siku nne sasa maisha yao yamevurugwa na mapigano yaliopamba moto kati ya Taliban na vikosi vinavyoongozwa na Ahmad Massoud, mtoto wa kamanda alieuawa, Ahmad Shah Massoud.

Viongozi wa Taliban wanasema juhudi za kufikia muafaka kwa njia ya majadiliano zilishindwa kuzaa matunda, wakati kundi hilo likijinadaa kutangaza kuundwa kwa serikali mpya, wiki kadhaa tangu kutwaa madaraka.

"Mpaigano yamekuwa mbaya zaidi na zaidi kila usiku," alisema mkaazi wa mji wa Jab al-Seraj Asadullah mwenye umri wa miaka 52. Yeye na wakazi wengine wa wilaya hiyo ya mkoa wa Parwan wanasema mapigano yamejikita zaidi milimani, lakini wakazi wengi bado wamekimbia eneo hilo.

Soma pia: Taliban kutangaza serikali mpya ya Afghanistan

Wakazi wanasema mapigano yalioongezeka yamezilazimu familia zisizopungua 400 kukimbia vijiji vilivyoko kwenyw barabara ambayo kawaida inaelekea kwenye mabonde matulivu na ya kijani ya Panjshir - umbali wa karibu kilomita 125 kaskazini mwa mji mkuu Kabul.

Moshi ulikuwa ukionekana ukitanda kutokea milima ya mbali wakati Wataliban wakishiriki mapigano ya kudhibiti mkoa wa mwisho kati ya mikoa 34 ya nchi hiyo.

Ahmad Massoud
Ahmad Massoud, kiongozi wa vikosi vya upinzani vinavyopambana dhidi ya Taliban katika mkoa wa bondeni wa Panjshir.Picha: Mohammad Ismail/REUTERS

Wanajeshi wa serikali?

Baadhi ya wakazi walisema katika siku kuelekea kuanguka kwa mji mkuu wa Kabula Agosti 15, waliona wanajeshi wa zamani wa jeshi la taifa la Afghanistan kutoka mikoa wa Kunduz, Kapisa, Parwan na Takhar wakielekea Panjshir baada ya mikoa hiyo kuangukia kwa Taliban.

Wakazi walisema wanajeshi hao walikuwa wanasafirisha magari ya kijeshi na vifaa vingine pamoja nao, lakini kukiwa na taarifa chache kwenda na kutoka Panjshir, ni vigumu kuhakiki madai hayo au kujua ni kiasi gani cha zana hizo zimetumiwa katika siku za karibuni.

Kama ilivyokuwa wakati wote wa mzozo wa Afghanistan, ambapo wanawake na watoto hukimbilia miji ya karibu, katika kadhia hii, wamekimbilia mji mkuu wa Parwan Charikar, na Kabul yenyewe, huku wanaume wakibaki nyuma kulinda nyumba zao.

Soma pia: Ulaya wataja masharti ya kushirikiana na Taliban

Shah Rahman, mkazi wa wilaya ya Syed Khil, alisema mke wake na watoto walikimbilia mjini Kabul siku tatu zilizopita. Yeye alirudi mapema Ijumaa asubuhi kukusanya vitu vyao na alisema alisimamishwa na Taliban njiani.

"Wanakagua kitambulisho chako na usajili wa gari kuhakikisha unatokea Parwana, na kisha wanakuachia kuingia," alisema.

Kama ilivyo kwa wakazi wengine wa Parwan, Rahman alisikia kuhusu vifo mkoani Panjshir, lakini madai hayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru kwa sababu barabara ya kwenda Panjshir inaendelea kuzuwiwa na mawasiliano ya simu yamekatwa wiki iliyopita.

Asadullah anasema Panjshir na Parwan ikiwa ndiyo mikoa iliyokuwa salama zaidi nchini Afghanistan kwa muda mrefu, wakazi wanatatizwa zaidi na mapigano kuliko maeneo mengine ya nchi.

Afghanistan | afghanische Soldaten in der Panjshir Provinz
Baadhi ya magari ya kivita waliondoka nayo wanajeshi wa zamani kuelekea Panjshir.Picha: Ahmad Sahel Arman/AFP/Getty Images

"Watu hawa hawajapitia mapigano ya kweli kwa miaka 20 na hawawezi kumudu kuwaona watoto wao wakilia usiku wakati risasi na maroketi vikirindima," alisema.

Mabomu ya kutegwa ardhini

Siyo mapigano tu yanayotokea kilomita chache kutoka makazi yao yanayowazuwia kuondoka nyumbani kwao. Wakazi wawili walizungumzia madai kwamba Taliban wanawafanya raia kukusanya maiti za wenzao waliokufa kutoka maeneo ya milima.

"Wanajua kuna mabomu ya ardhini, hivyo wanawafanya watu wasio na hatia kukusanya maiti," alisema mkazi mmoja alieomba kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, wakazi wengine walipinga madai hayo, ambayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Soma pia: Taliban yasherehekea kuondoka kwa Marekani

Kwa upande wake, kundi la Taliban lilikanusha vikali madai ya wapiganaji wake kuwadhuru kwa maksudi raia. Kamanda moja wa Taliban alisema hatari ya kudhuru maisha ya raia ndiyo imewafanya kujizuwia kushiriki vita kamili Panjshir.

"Hatutaki kuwadhuru raia, vingine tungeingia kikamilifu na vita hii ingekuwa imeshaisha ndani ya siku mbili, lakini hatutaki watu maskini na wasio na hatia kuteseka tena. Licha ya ahadi hizo, raia bado hawajihisi salama, hata katika maeneo yanayoizunguka Panjshir.

'Sote tutakufa kwa njaa'

Ingawa Parwan ilikuwa ngome ya muda mrefu ya Massoud mkubwa, wakati wa ukaliaji wa majeshi ya Kisovieti na upinzani wake dhidi ya utawala wa Taliban katika miaka ya 1990, wakazi wa Parwan wanasema wanataka kukomesha mapigano.

Karte Afghanistan Pandschir Tal EN
Ramani ya Afghanistan ikionesha bonde la Panjshir

"Pande zote zinazungumzia Quran na wanasema ni Waislamu, lakini wanafanya nini, kuuwa Waislamu wengine. Hii laazima ikome," alisema Shir Agha, mkazi wa Parwan alieko katika umri wa miaka 30.

Kwa wakazi wanaobakia katika wilaya ya Jab al-Seraj, haitoshi tu kwamba mapigano yamegeuka suala muhimu. Wanasema maeneo yao ambayo yalikuwa yanategemea zaidi utalii wa ndani kuja bonde la Panjshir, yanapambana kutokana na kufungwa kwa bonde hilo na kutokana na masuala ya kibenki nchini kote.

Soma pia: Marekani yaonya kuhusu kitisho cha kuaminika kwenye uwanja wa ndege wa Kabul

Kama ilivyo kwa miji mingine, Charikar inateseka kutokana na ukosefu wa pesa taslim wakati ambapo mabenki yanapambana kufungua tena na ofisi nyingi zimefungwa tangu Taliban walipotwaa madaraka. Kwa wakazi wanaotafuta kukimbia mapigano, ukosefu wa pesa taslimu unaumiza hasa.

Habib Golbahar, ambaye anasema kuhamisha familia yake kutamgharimu pesa kidogo alizoweka akiba, anasema watu mjini Parwan wanapambana kutafuta hata Afghani 100, ambazo ni sawa na dola 1.13.

Huku ofisi nyingi za serikali na binafsi zikiwa bado zimefungwa, na uchumi wa utalii ukishuka, Golbar anasema kitisho cha kiuchumi, ni hatari sawa na, kama siyo zaidi ya vita vyenyewe.

"Wanaweza kupigana kwa miaka mingine 10 wakiuawana, lakini sote tutakufa kwa njaa kabla ya hapo,"

 

Chanzo: Mashirika