1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO: China iwajibishwe kwa kuiunga mkono Urusi

18 Juni 2024

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema China inapaswa kuwajibishwa iwapo itaendelea na mwenendo wake wa kuisadia Urusi kijeshi.

https://p.dw.com/p/4hBPj
Marekani Biden akutana na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Rais wa Marekani Joe Biden alipokutana na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg katika Ikulu ya MarekaniPicha: Mark Schiefelbein/AP/dpa/picture alliance

Stoltenberg amesema serikali ya Kyiv inahitaji ufadhili wa kijeshi unaooleweka na thabiti huku akipigia chapuo kuongezwa kwa mafungu katika  bajeti za ulinzi za mataifa wanachama wa NATO kutokana na  mashaka ya Donald Trump katika kuisaidia Ukraine.

NATO mwezi ujao inaadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwake kwa mkutano wa kilele utakaofanyika mjini Washington ambao unalenga kutuma ujumbe madhubuti wa kuiunga mkono Ukraine kabla ya Rais Joe Biden kuchaguliwa tena kuwania kiti cha urais mwezi Novemba dhidi ya mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump.

China na lawama za kuendeleza vita vya Urusi na Ukraine

China Beijing 2024 | Ziara ya Vladimir Putin | akiwa na Xi Jinping
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping wakibadilishana hati wakati wa hafla ya kutiliana saini kufuatia mazungumzo yao mjini Beijing Mei 16, 2024.Picha: Sergei Bobylov/AFP/Getty Images

Stoltenberg ameitupia lawama China kwa kuzidisha mzozo kati ya Urusi na Ukraine kupitia kile maafisa wa Marekani wanasema ni kutoa msukumo mkubwa wa mauzo ya nje kwa shabaha ya kujenga upya sekta ya ulinzi ya Urusi.

Nikimnukuu hapa anasema Rais Xi Jinping "amejaribu kujenga hisia za kujiweja nyuma katika mzozo huu, ili kuepusha vikwazo na kuendeleza biashara. Lakini kiuhalisia ni kwamba China ipo katika jaribio la kutimiza malengo mawili kwa wakati mmoja, kwa kuiunga mkono Urusi kwa upande mmoja huku ikijaribu pia kudumisha uhusiano na mataifa ya Magharibi.

Amesema serikali ya Beijing haiwezi kudhibiti vyote, na kama haitabadiliki mkondo wake itapaswa kukabiliwa na ipasavyo kwa kitendo hicho. "Kuna mazungumzo yanayoendelea miongoni mwa washirika wa NATOkuhusu jinsi ya kukabiliana na matokeo ya usalama kutona na ukweli kwamba China inaunga mkono juhudi za vita za Urusi nchini Ukraine." Alisema Stoltenberg.

China yakana tuhuma za uchochezi

China hata hivyo imetetea uhusiano wake na Moscow na kuzitaja ripoti za Marekani kama upotoshaji. China imekwenda mbali zaidi na kusema, haitoi msaada wa silaha kwa pande yoyote katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine, tofauti na inavyofanya Marekani na washirika wake wa Magharibi.

Aidha Stoltenberg ameongeza kuseama ziara ya Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Korea Kaskazini, ambayo inaipa makombora Moscow licha ya kuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, inaonyesha wazi  jinsi gani serikali ya Moscow "ilivyokuwa tegemezi" kwa viongozi wa kimabavu.

Soma zaidi:Marekani yaidhinisha Ukraine itumie silaha kuyashambulia maeneo ya Urusi

Mkutano wa kilele wa NATO wa 2014 uliweka lengo la ufadhili ambalo lilifikiwa na nchi tatu pekee  ambazo Marekani, Uingereza na Ugiriki, lakini pamoja na mambo mengine muhimu mkutano huu wa sasa wa Washington tofauti na wanachama 32 wa muungano huo pia utaleta washirika wanne muhimu kutoka Asia-Pacific: Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini.

Chanzo: AFP