1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz aunga mkono juhudi za amani Ukraine

20 Septemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameunga mkono juhudi za kimataifa kuleta amani nchini Ukraine katika hotuba yake mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

https://p.dw.com/p/4Wajq
UN-Vollversammlung in New York
Picha: Frank Franklin II/AP/picture alliance

Kwa mara nyingine tena kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, amemtaka rais wa Urusi Vladimir Putin akomeshe vita vya Ukraine, akisema Urusi inabeba dhamana kwa vita hivyo. Scholz amesisitiza kuwa ni rais Putin anayeweza kuvifikisha mwisho wakati wowote kwa amri yake moja.

"Lakini vita vya uchokozi vya Urusi vimesababisha mateso makubwa sio tu nchini Ukraine. Watu kote ulimwenguni wanateseka kutokana na mfumuko wa bei, madeni yanayoendelea kukua, uhaba wa mbolea, njaa na umasikini unaoongezeka. Ni kwa sababu vita hivi vinasababisha matokeo yasiyoweza kuvumilika. Ni sawa na sahii kwa ulimwengu uhusike katika kutafuta amani. Waakti huo huo, tujihadhari na suluhu za kinafiki zinazowakilisha amani kwa jina tu. Kwa sababu amani bila uhuru inaitwa uonevu. Amani bila haki inaitwa udikteta. Urusi pia lazima hatimaye ielewe hilo."

Katika hotuba yake kansela Scholz pia ameitisha mageuzi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yamezuiwa kwa kipindi kirefu, yajumuishe ushawishi zaidi kwa bara la Afrika, Asia na Amerika Kusini. Amesema ameridhika kwamba washirika zaidi, wakiwemo wachama watatu wa kudumu wa baraza la usalama wametangaza wanataka kusonga mbele katika suala la mageuzi, akimaanisha Marekani, Uingereza na Ufaransa.

Soma pia: Urusi yafanya mashambulizi katika miji ya Ukraine

Kansela Scholz pia amemhimiza Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alegeze msimamo kuhusu mipango ya mageuzi ya sheria yaliyozua utata nchini Israel. Katika mkutano wa dakika 50 na Netanyahu kandoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, Scholz amesisitiza juu ya umuhimu wa uungwaji mkono mpana wa kijamii kadri inavyowezekana kwa mageuzi ya msingi ya aina hiyo na kutambua kujitolea kwa dhati kwa rais wa Israel Isaac Herzog katika suala hilo.

Ramaphosa akosoa matumizi ya fedha katika vita badala ya maendeleo

Akiuhutubia mkutano wa mjini New York, rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema wakati umewadia kuongeza kwa kiwango kikubwa cha utoaji misaada ya maendeleo huku ulimwengu ukiwa bado ungali nyuma katika kuyatimiza malengo yanayoungwa mkono na umoja wa Mataifa ya kutokomeza umaskini kufikia mwaka 2030. Ramaphosa amekosoa utumiaji wa mabilioni ya fedha kwa ajili ya vita badala ya maendeleo.

 Präsident von Südafrika Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika KusiniPicha: Stanislav Krasilnikov/TASS/dpa/picture alliance

"Ni mashtaka ya uhalifu mkubwa kwa jumuiya hii ya kimataifa kwamba tunaweza kutumia kiwango kikubwa cha fedha kwa vita. Na kwa kweli matrilioni yanatumika kwa vita, lakini hatuwezi kuunga mkono hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukidhi mahitaji ya mabilioni ya watu ulimwenguni, kama kushughulikia njaa, afya, kuwajengea uwezo wanawake na kuhakikisha kuna maendeleo katika nchi ambazo ziko hatarini."

Ramaphosa amerudia wito wake kutaka diplomasia itumike katika kuvitafutia ufumbuzi vita vya Ukraine. Amesisitiza juu ya sifa za demokrasia za Afrika Kusini na kuhimiza demokrasia kufuatia mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi barani Afrika ikiweno nchini Niger. Amesema amekutana na rais wa Ukraine Volodymry Zelensky katika mkutano wa mjini New York na kuzungumzia mpango wa amani wa nchi za Afrika.

Hivi leo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatarajiwa kuandaa mkutano kuhusu hali ya hewa ambao utagubikwa na kukosekana kwa wazungumzaji muhimu kutoka nchi mbili kubwa zinazoongoza kwa utoaji wa gesi chafu za viwandani, China na Marekani.

(dpa, afptv)