1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa:Afrika Kusini haikuipelekea silaha Urusi

4 Septemba 2023

Uchunguzi uliofanywa na Afrika Kusini ubaini kwamba nchi hiyo haikupakia shehena ya silaha kuipelekea Urusi izitumie katika vita vyake dhidi ya Ukraine. Serikali itachapisha mukhtasari wa matokeo ya uchunguzi huo.

https://p.dw.com/p/4VuKT
 Präsident von Südafrika Cyril Ramaphosa
Picha: Stanislav Krasilnikov/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema tume ya uchunguzi imegundua hakuna ushahidi kwamba Afrika Kusini ilipakia silaha au risasi katika meli ya Urusi mwezi Desemba mwaka uliopita. Akizungumza jana jioni katika hotuba yake kwa taifa Ramaphosa alisema hakuna madai yoyote yaliyothibitishwa kuwa ya kweli na wale walioyatoa hawawezi kuyathibitisha madai yao.

Ramaphosa alikuwa akizungumzia madai ya balozi wa Marekani aliyesema mapema mwaka huu kwamba serikali ya Afrika Kusini ilikuwa ikiipelekea silaha na risasi Urusi itumie katika vita vyake dhidi ya Ukraine. Balozi huyo alisema silaha hizo inadaiwa zilisafirishwa kupitia meli ya Urusi iliyotia nanga katika kambi ya jeshi la majini karibu na mji wa Cape Town Desemba mwaka jana.

Afrika-Russland-Gipfel
Rais Cyril Ramaphosa, kushoto, na rais Vladimir Putin wa Urusi wakiwa St Petersburg (27.07.2023)Picha: Sergei Bobylev/AP/dpa/picture alliance

Rasmi Afrika Kusini imetangaza msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine. Ramaphosa alianzisha uchunguzi kuhusu suala hilo baada ya upinzani katika bunge la Afrika kusini kusisitiza. Ramaphosa amesema serikali inapanga kutoa mukhtasari wa matokeo ya uchunguzi wa tume, lakini sio ripoti kamili kutokana na usiri wa taarifa za kijeshi.