1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

EU yazingatia majibu yake kwa mapinduzi ya kijeshi Niger

30 Agosti 2023

Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanazingatia majibu yao kwa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger katika mkutano mjini Toledo nchini Uhispania

https://p.dw.com/p/4VlRA
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakiwa na mkjumbe mkuu wa Umoja huo Josep Borell (katikati) pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa hao mjini Brussels mnamo Mei 22, 2023
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakiwa na mjumbe mkuu wa Umoja huo Josep BorellPicha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Ujerumani na Ufaransa zinashinikiza wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi nchini Niger na mashirika yanayowaunga mkono. Vyanzo kadhaa vya kidiplomasia vimeliarifu shirika la habari la dpa.

Soma pia:Balozi wa Ufaransa bado yupo Niger licha ya kuamriwa kuondoka

Borrell azungumzia uwezekano wa vikwazo kwa viongozi wa mapinduzi

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borell, amesema kuwa mawaziri hao wa ulinzi watachunguza uwezekano wa kuwawekea vikwazo viongozi wa mapinduzi hayo na uwezekano wa athari kwa jeshi na ushirikiano wa uhamiaji.

Soma pia:Niger yaliamuru jeshi kuwa kwenye tahadhari kubwa

Akikataa kutoa maelezo zaidi, Borell amesema kuwa baada ya mapinduzi mengine katika kanda hiyo, hali katika eneo la Sahel barani Afrika inaendelea kuwa mbaya.Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wako makini kutofanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi.

Borrell aitaja Niger kama mshirika muhimu

Takriban mwezi mmoja uliopita, Borell aliitaja Niger kama mshirika muhimu baada ya ziara nchini humo. Kwa Ufaransa, Niger imekuwa mshirika muhimu katika vita vyake dhidi ya makundi ya kigaidi hasa baada ya viongozi wa kijeshi nchini Mali na Burkina Faso kulazimisha kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa kutoka nchi zao.

Algeria yapendekeza muda wa miezi sita kwa serikali ya mpito Niger

Jenerali Abdourahmane Tiani - Kiongozi wa kijeshi nchini Niger akiwasili kukutana na mawaziri mjini Niamey nchini Niger mnamo Julai 28, 2023
Jenerali Abdourahmane Tiani - Kiongozi wa kijeshi nchini NigerPicha: Balima Boureima/Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Algeria Ahmed Attaf, amependekeza muda wa miezi sita kwa serikali ya mpito nchini Niger baada ya ziara yake wiki iliyopita katika mataifa matatu ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, ambayo imetishia kutuma wanajeshi wake nchini Niger ikiwa uongozi wa sasa wa kijeshi nchini humo utashindwa kudumisha demokrasia.

Kiongozi wa kijeshi anataka kipindi cha mpito kudumu kwa miaka mitatu

Katika mkutano na wanahabari uliopeperushwa kupitia televisheni, Attaf amesema kuwa kinyume cha hayo, kiongozi wa kijeshi nchini Niger jenerali Abdourahamane Tiani, ametoa wito wa kipindi cha mpito kitakachodumu kwa takriban miaka mitatu.

Attaf assisitiza nchi yake inapinga muingilio wa kijeshi Niger

Attaf amesisistiza msimamo wa nchi yake wa kupinga muingilio wa kijeshi nchini Niger na kusema taifa hilo halitaruhusu anga yake kutumika kufanikisha hatua hiyo.

Soma pia:Niger yawatimua mabalozi wa nchi 4 ikiwemo Ujerumani

Attaf ameongeza kusema kuwa katika mipango ya kisiasa ya kutatua mgogoro, Algeria itashiriki katika mawasiliano ya kina na mashauriano na pande zote zinazohusika ambazo zinaweza kuchangia utatuzi wa mgogoro huo kisiasa au kuunga mkono juhudi katika mwelekeo huu.

Soma pia:Niger yaziidhinisha Mali, Burkina Faso kuisaidia kijeshi ikivamiwa

Ziara ya Attaf wiki iliyopita, ilimfikisha katika mataifa ya Nigeria, Benin na Ghana, ambapo alifanya mikutano licha ya miito ya mara kwa mara ya nchi yake ya kuzuia muingilio wa kijeshi nchini Niger.