1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROMA-Kikundi cha waasi wa Kihutu wa Rwanda chakubali kuacha harakati zake za kijeshi.

31 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFRZ

Kikundi kikuu cha waasi wa kabila la Kihutu,kimetangaza leo kuwa kinaacha harakati zake za mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya Rwanda na kwa mara ya kwanza kimelaani mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo mwaka 1994.

Katika ripoti yake iliyotolewa mjini Roma na Ignace Murwanashyaka,kikundi hicho cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda(FDLR),kinalaani mauaji ya mwaka 1994 ambapo kikundi hicho kimekuwa kikishutumiwa kutekeleza mauaji hayo kwa kiwango kikubwa.

Kikosi cha jeshi la Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika eneo la Maziwa Makuu-MONUC,kimepokea kwa mikono miwili uamuzi huo na kueleza ni uamuzi muhimu utakaosaidia kumaliza vita vya mara kwa mara katika eneo la Maziwa Makuu.

Kikundi hicho cha FDLR kimesema kimekubali kuweka silaha chini kwa utashi wao na kurejea nchini Rwanda kwa amani,ikiwa ni hatua zitakazoendana na mpango wao wa kupokonywa silaha.

Tangazo hili limetolewa baada ya kuwepo mazungumzo yaliyochukua siku tisa na wawakilishi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mjini Roma.Serikali ya Rwanda haikuwakilishwa katika mazungumzo hayo.