1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Tume ya kimataifa juu ya wahamiaji

Ramadhan Ali24 Novemba 2005

Tume ya kimataifa juu ya nyendo za wahamiaji duniani imetoa jana ripoti yake mjini Berlin, Ujerumani ikihimiza kuwapo sera maalumu ya kimataifa juu ya wahamiaji.

https://p.dw.com/p/CHoF
Wahamiaji nchini Burundi
Wahamiaji nchini BurundiPicha: AP

Tume ya kimataifa juu ya nyendo za uhamiaji duniani, imetangaza ripoti yake hivi punde chini ya kichwa:”UKWELI BADALA YA SIASA”.

Idadi ya wahamiaji kutoka kila pembe ya dunia, imepanda mnamo miaka 30 iliopita kutoka milioni 75 na kufikia milioni 200 na mnamo miaka ijayo, inatarajiwa hata kuongezeka zaidi.Taarifa hizi zimo ndani ya ripoti ya kwanza ya ile inayoitwa “Global Commission for International migration”iliotolewa mjini Berlin,Ujerumani.

Tume hiyo ya kimataifa ambamo mwanasiasa wa chama cha CDU na spika wa zamani wa Bunge la Ujerumani, Bibi Rita Süsssmuth ni mwanachama,inahimiza kuwepo sera maalumu ya kimataifa inayoshughulikia wahamiaji kwa shabaha ya kuhifadhi haki za wahamiaji na wakimbizi.Mbali na hayo, wahamiaji wajumuishwe barabara na jamii za zile nchi wanakohamia.

Wakati katika kambi ya mrengo wa kulia katika nchi za viwanda kama vile Ujerumani uwezo wa kukidhi wahamiaji na wakimbizi takriban umefikia kikomo chake,kambi ya mrengo wa shoto inawatetea kwa kubainisha manufaa makubwa yatakayostawisha na kunawirisha jamii ya mchanganyiko wa mila na utamaduni.Kambi zote mbili zinakosea hapo:Kwani, kulitatua tatizo la uhamiaji na wakimbizi,hakuhitaji kuingizwa nadharia za kisiasa,bali kuwa na nia ya kweli.

Katika nia hii ya ukweli,ni pamoja na kile kilichogunduliwa na Tume hii ya kimataifa ya uhamiaji kwamba, wahamiaji wengi sana si wakimbizi, bali ni watu walioamua kuhamia sehemu nyengine za dunia ,kwavile wameona huko wangekuwa na maisha bora.Kwa jicho la kambi ya mrengo wa kulia,hawa ni wakimbizi wa kiuchumi.Ni kweli pia kwamba jamii kama ile ya Ujerumani inayopungukiwa na idadi ya wakaazi,inahitaji wahamiaji.

Ukweli huu sasa umetambuliwa pia na kambi ya mrengo wa kulia.Hatahivyo, uhamiaji unakuwa na faida tu ikiwa kuna mkakati maalumu wa kuwajumuisha wahamiaji na jamii nzima na sio kuachia jamii mbali mbali za mila na utamaduni tofauti zinakulia pembezoni na mwenziwe.

Kwa hali hii si swali tena iwapo bali vipi nah ii inazihusu pande zote mbili-wananchi na wahamiaji.Wananchi sio tu wavumilie uhamiaji wa wageni bali wawape pia matumaini ya kustawisha maisha yao.Wanachohitaji wahamiaji sio tu hati za kuwaruhusu kuishi nchini bali fursa pia za kujihisi wana haki sawa katika jamii .Kufikia shabaha hii, kunahitaji mengi kufanywa na hasa elimu na mafunzo ya watoto na vijana ya wahamiaji.

Sera barabara ya uhamiaji inafanya kazi ikiwa tu, wahamiaji wakiamua kuwa ni sehemu ya jamii mpya waliojiunga nayo.Na ili iwe hivyo, haitoshi tu kujua lugha ,bali pia kujitambulisha wazi wazi na uhuru na sheria za nchi walimohamia.

Ripoti ya uhamiaji ya Tume hii ya kimataifa ina mwito kadhaa wa kinadharia:mara kwa mara Tume ikibainisha manufaa makubwa yanayoweza kupatikana kutoka maarifa na ujuzi wa wahamiaji.Wanaporudi maskani mwao au nchi zao, wahamiaji hawa wanarudi na ujuzi na maarifa mfano ya kidemokrasia.Wanaweza kuchangia kwa njia hiyo utawala bora na kujenga jamii ya kiraia ilio bora.Na hii ni kweli. Dosari dogo katika fikra kama hizi,ni kwamba wahamiaji wengi sio tu wakati Fulani watarudi makwao ,bali wanataka kujenga maisha mapya katika nchi nyengine mmbali na ile yao asilia-katika nchi kama vile Ujerumani.

Baadhi ya wahamiaji hawa, waweza kugeuka daraja kati ya nchi yao mpya na ile asilia.Muhimu zaid, ingekuwa bora kuwapa watu huko huko makwao, matumaini ya kuwa na maisha bora kwa njia ambayo nchi za Ulaya sio tu zinafungua milango ya masoko yao kwa bidhaa zao za kimimo .Kwani, ni kwa njia hii itawezekana kuzuwia hata vijana walioelimika kutozipa mgongo nchi zao .Ili iwe hivyo,linahitajika suluhisho la pamoja kwa Ulaya nzima-au kama vile alivyotarajia Katibu mkuu wa UM Kofi Annan, kutoka Tume hii-suluhisho la dunia nzima lipatikane kwa changamoto za wimbi lauhamiaji.