1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto aapa kutokomeza maandamano ya vurugu

26 Juni 2024

Rais wa Kenya William Ruto amelihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatano na kusema maandamano ya kupinga ongezeko la kodi na ushuru yalivamiwa na makundi ya wahalifu na kuapa kuwa matukio kama hayo hayatojirudia tena.

https://p.dw.com/p/4hVj3
William Ruto | Rais wa Kenya
Rais wa Kenya William RutoPicha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Ruto ameapa kwamba matukio ya uvamizi wa Bunge aliyoyaita "kitisho kwa usalama wa taifa", kamwe hayatojirudia kwa gharama yoyote." Hayo yanajiri wakati jumuiya ya kimataifa ikielezea wasiwasi wake kutokana na hali ya vurugu inayoshuhudiwa nchini humo.

Kupitia televisheni, Rais William Ruto wa Kenya ameapa kuchukua msimamo mkali dhidi ya "vurugu na machafuko" yaliyoshuhudiwa hapo jana baada ya maandamano ya kupinga mapendekezo ya serikali yake ya kupandisha kodi na ushuru kugeuka kuwa ya vurugu huku akilaani uvamizi wa Bunge :

Kenya | Waandamanaji jijini Nairobi
Waandamanaji jijini Nairobi wakipinga muswada wa kuongeza kodi na ushuru nchini KenyaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

" Cha kusikitisha zaidi, shambulio la leo dhidi ya utaratibu wa Katiba ya Kenya limesababisha watu kupoteza maisha, pia uharibifu wa mali, unajisi wa taasisi na nembo za uhuru wetu. Matukio ya leo yanaashiria mabadiliko muhimu ya jinsi tunavyoshughulikia vitisho kwa usalama wa taifa letu. Nalihakikishia taifa kuwa serikali imekusanya rasilimali zote ilizokuwa nazo ili kuhakikisha kuwa matukio ya aina hii hayatajirudia tena na kwa gharama yoyote ile."

 Rais Ruto aliwaambia waandishi habari kuwa serikali yake itatoa jibu kamili na mwafaka wa haraka kwa matukio ya uhaini akisema maandamano hayo yalivamiwa  na watu hatari.

Soma pia: Waandamanaji wavamia jengo la bunge Kenya

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Kenya Adan Duale ameamuru jeshi la nchi hiyo kupelekwa mitaani na sehemu mbalimbali ya nchi kusaidia polisi kukabiliana na kile alichokiita kuwa dharura ya kiusalama.

Wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, polisi na vikosi vya usalama kujizuia na matendo ya kutumia nguvu kupita kiasi huku akitoa wito wa kufanyika maandamano ya amani.

Zaidi ya mataifa kumi ya Magharibi yameelezea wasiwasi wao mkubwa kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa hapo jana ambapo watu watano wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Katika taarifa yao ya pamoja, balozi za nchi 13, zikiwemo Canada, Ujerumani, Uingereza na Marekani, zimetaja kushtushwa mno na matukio yaliyoshuhudiwa nje ya  Bunge la Kenya.

Wasiwasi kama huo umetajwa pia na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ambaye ameitaka nchi hiyo kuwa na utulivu na kujiepusha na ghasia zaidi.

Kauli za wanasiasa wa Kenya

Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Rais mstaafu wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: Shisia Wasilwa/DW

Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta ameelezea kusikitishwa kwake na maafa ambayo yametokea nchini mwake wakati wa maandamano hayo na kuongeza kuwa  ni haki ya kila Mkenya kuandamana kwa mujibu wa katiba  ya nchi hiyo. Kiongozi huyo wa zamani ameongeza kuwa ni wajibu wa viongozi kusikiliza vilio vya wananchi.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa ukatili dhidi ya waandamanaji na kushinikiza kufanyika kwa mazungumzo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati.

Kwa kiasi kikubwa, maandamano ya wiki iliyopita yaliyoongozwa na vijana maarufu kama "GenZ" yalikuwa ya amani, lakini machafuko yalizuka jijini Nairobi jana Jumanne, huku umati wa watu wakiwarushia mawe polisi, kuondoa vizuizi vilivyowekwa na kuvamia na kuchoma moto majengo ya bunge wakipinga hatua ya bunge hilo kupitisha muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024.

(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)