1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Comoro asifu amani kabla uchaguzi wa Jumapili

10 Januari 2024

Rais wa Comoro Azali Assoumani ana matumaini ya kushinda awamu ya tatu madarakani katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.

https://p.dw.com/p/4b5mk
Rais wa Comoro Azali Assoumani
Rais Azali Assoumani anawania muhula wa tatu wenye utataPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais Azali Asumani amesifu rekodi yake ya kudumisha amani na kujenga barabara na hospitali katika nchi hiyo inayokabiliwa na umasikini. Wapiga kura kiasi 340,000 wanatarajiwa kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais mpya katika uchaguzi ambao wagombea sita wanawania kiti cha urais.

Upinzani umegawika kati ya wale wanaotaka uchaguzi na wale wanaotaka uchaguzi huo ususiwe, hali inayoiweka kambi ya rais Azali Assoumani kuwa na matumaini makubwa ya kushinda katika duru ya kwanza ya upigaji kura.

Soma pia: Rais wa zamani wa Comoro Ahmed Sambi afungwa maisha kwa uhaini

Rais Assoumani, mwenye umri wa miaka 65 na ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ameitawala Comoro kwa mkono wa chuma na wapinzani wake wengi wametupwa gerezani au kulazimika kwenda uhamishoni.