1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto atoa wito kwa Raila kuandaa maandamano ya amani

Shisia Wasilwa 16 Machi 2023

Rais wa Kenya William Ruto, amuambia Muungano wa upinzani wa Azimio nchini humo kuwa serikali ina wajibu wa kudumisha amani na utengamano wakati wa maandamano yanayopangwa kufanywa na upinzani siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4OktY
Kenia | Präsident William Ruto
Picha: James Wakibia/ZUMAPRESS/picture alliance

Rais William Ruto amesema kuwa vyombo vya dola havitaingilia maandamano hayo, lakini kiongozi wa upinzani Raila Odinga ana wajibu wa kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi na mali zao hayawekwi hatarini. 

Rais Ruto amesema kiongozi huyo wa upinzani amekuwa akitumia maandamano kwa muda mrefu huku damu ikimwagika na mali kuharibiwa, huku akishangaa ni vipi wakati huu Raila atadumisha amani wakati wa maandamano ambayo ameyapangia kufanyika siku ya Jumatatu pamoja na viongozi wenzake jijini Nairobi.

Vuta n'kuvute ya utawala uliopita na serikali yazidi Kenya

Upinzani umekuwa ukiandaa maandamano katika kaunti tofauti za taifa tangu kuanza kwa mwezi huu. Hata hivyo, maandamano ya Kisumu yalisababisha vurugu.

Upinzani ulikuwa umetoa muda wa siku 14 kwa serikali kuzingatia, siku hizo zitakamilika tarehe 20 mwezi huu. Moja ya masharti ni kwa serikali kupunguza gharama ya maisha, mageuzi kwenye taasisi inayosimamia uchaguzi ambapo tayari Rais Ruto ameteua jopo la kuwachagua makamishna wa tume ya uchaguzi ya IEBC. Tayari serikali imekiuka sharti hilo.

Upinzani wadai uchaguzi ulichakachuliwa na kummpa Ruto ushindi usiohalali

Kenia Oppositionsführer Raila Odinga
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga na Kiongozi wa chama cha NARC-Kenya ambacho ni sehemu ya muungano wa Azimio Martha Karua Picha: Shisia Wasilwa/DW

Aidha upinzani unataka sava ya uchaguzi mkuu ifunguliwe, ikidai kuwa kura za Raila ziliibiwa. Rais amesema hilo halitafanyika akidai kuwa seva zilifunguliwa upinzani ulipowasilisha kesi katika Mahakama ya Juu. Raila ameapa kufanya maandamano ya amani.

Hayo yanajiri huku viongozi wa dini wakishauri viongozi hao kutafuta suluhu kupitia mazungumzo. Baraza la Makanisa nchini tayari limekutana na Rais William Ruto na Raila Odinga katika nyakati tofauti kujaribu kutafuta mwafaka.

Raila odinga apanga mikutano zaidi ya hadhara Kenya

Hata hivyo Raila ameapa kuwa wakati huu hataitikia salamu za heri kama ilivyofanyika katika utawala wa Rais Mwai Kibaki mwaka 2007 na Uhuru Kenyatta mwaka 2017.

Kwa upande wake, Rais ameshikilia kuwa wakati huu hapatokuwa na serikali ya nusu mkate. Raila amewataka wafuasi wake kuandamana jijini Nairobi siku ya Jumatatu, akisema Wakenya wana haki ya kufanya maandamano.

Rais Ruto amewaambia Wakenya wasiwe na wasiwasi kuhusu maandamano hayo. Leo Raila anaanda maandamanoo mjini Nakuru kama sehemu ya maandalizi ya maandamano ya juma lijalo ambapo ameitaja siku hiyo kuwa ya mapumziko.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi.