1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta n'kuvute ya utawala uliopita na serikali yazidi Kenya

Shisia Wasilwa
6 Februari 2023

Nchini Kenya, vuta n'kuvute ya utawala uliopita wa Rais Uhuru Kenyatta na unaoendelea sasa wa Rais William Ruto inaonekana kupamba moto, huku kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga, akisema madai hayo hayana msingi.

https://p.dw.com/p/4N8rC
Kenia Präsidentschaftswahl | Raila Odinga
Picha: Boniface Muthoni/Zuma/IMAGO

Na kumtaka Rais Ruto kuacha kuingilia kazi ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Kodi. Hata hivyo, Rais Ruto alikuwa mwepesi wa kujibu na kusema kuwa kila Mkenya anastahili kulipa kodi bila ya kuzingatia hadhi yake katika jamii.

Raila, ambaye kwenye uchaguzi mkuu uliopita aliungwa mkono waziwazi na Uhuru Kenyatta, aliyasema hayo kwenye moja ya ngome zake za siasa ya Kibra, pindi tu aliporejea kutoka ziara yake ya Afrika Magharibi.

SOMA PIA: Odinga: Nitamuondoa Ruto madarakani

Kama alivyokuwa ameahidi kwamba angeliandaa mikutano ya hadhara kujadili masuala mazito ya taifa kama vile kuongezeka kwa gharama ya maisha, kiongozi huyo mkuu wa upinzani amekutana na suala tete la kodi ambalo limekuwa kiazi moto. Akiitetea familia ya Kenyatta, Raila alidai kuwa kodi ya urithi wa familia iliondolewa kwa Wakenya wote. 

Sheria ya Kodi

Jomo Kenyatta
Picha: AP

Sheria ya kutolipa kodi kwa mali ya urithi ilianzishwa mwaka 1969. Baada ya kifo cha rais wa kwanza, Mzee Jomo Kenyatta, Rais wa pili Daniel Moi aliongeza jina lake kwenye orodha yenyewe. Mwaka 1982, sheria ilibadilishwa na kujumuisha Wakenya wote kutolipishwa kodi.

Hata hivyo, muda mfupi tu baada ya cheche za Raila, Rais Ruto akawa mwepesi wa kulumbana kwenye mdahalo huo aliouanzisha.

SOMA PIA: Mahakama ya juu Kenya yaidhinisha ushindi wa Ruto

Mapema juma lililopita, aliyekuwa mama wa kwanza wa taifa la Kenya, Mama Ngina Kenyatta, ambaye ndiye mama mzazi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alijitosa kwenye mdahalo huo ambao unaelekea kuongezea makali, matamshi ya Rais Ruto kuhusu uwepo wa matabaka ya walalahai na walalahoi. Ni moja ya kauli mbiu alizotumia William Ruto wakati wa kampeini zake huku akiwavutia mahasla. Mama Ngina akiyakanusha madai ya Ruto.

Kwenye mkutano huo ambao Raila aliapa kushinikiza kuondolewa kwa serikali ya Rais Ruto madarakani, alizindua kile alichokiita Vuguvugu la Vijana litakalolinda demokrasia huku maafisa wake wakiwa wamevalia mavazi ya wanajeshi. Muungano wa Azimio unapanga kuelekea Machakos, siku ya Ijumaa, kisha baadaye Busia kumshinikiza Rais Ruto kuondoka madarakani, wakimkosowa kwa kuendekeza ufisadi na kushindwa kupunguza gharama ya maisha.