1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaQatar

Safari bado ndefu kwa Israel na Hamas kufikia makubaliano

12 Machi 2024

Qatar ambayo ni miongoni mwa wapatanishi katika vita vya Israel na Hamas imesema pande hizo mbili haziko karibu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na juu ya kuachiliwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina.

https://p.dw.com/p/4dR7b
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Qatar Majed Al-Ansari, akizungumza na waandishi wa habari mjini Doha
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Qatar Majed Al-Ansari, akizungumza na waandishi wa habari mjini DohaPicha: Imad Creidi/REUTERS

Mwezi mtukufu kwa Waislamu wa Ramadhaniulianza hapo Jumatatu bila ya kufikiwa makubaliano juu ya kubadilishana mateka kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Qatar Majed al-Ansari amesema katika mkutano na waandishi wa Habari kwamba licha ya kufanyika mazungumzo kwa wiki kadhaa yaliyowahusisha wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri hakuna hatua kubwa zilizopigwa.

Soma Pia:Wapalestina kuanza Ramadhan katika kivuli cha vita Gaza

Qatarimeeleza kuwa hali bado ni ngumu.hii inamaanisha kwamba hakuna uwezekano kwa sasa kwa pande zote mbili kukubaliana juu ya hatua zinazoweza kutatua tofauti zao lakini bado yapo matumaini na bidii zinaendelea kufanyika ili makubaliano yafikiwe katika siku za hivi karibuni.

Kushoto mbele: Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken. Kulia Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi
Kushoto mbele: Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken. Kulia Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi Picha: Egyptian Presidency/Xinhua/picture alliance

Marekani,Qatar na Misri zilikuwa na matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya kuanza mwezi wa Ramadhani, makubaliano ambayo yangejumuisha kuachiliwa mateka wa Israel na pia wafungwa wa Kipalestina pamoja na kuingia katika Ukanda wa Gaza misaada zaidi ya kibinadamu. Lakini mazungumzo hayo yalikwama wiki iliyopita.

Soma Pia:Guterres ataka usitishaji mapigano Gaza, Sudan

Wakati huo huo meli iliyobeba tani 200 za msaada kwa ajili ya watu wa Gaza imeondoka Cyprus leo Jumanne katika mpango wa majaribio kupitia njia ya baharini. Mashirika ya misaadayanasema eneo hilo linakaribia kutumbukia kwenye janga la njaa.

Meli ya shirika la misaada la Open Arms iliondoka katika bandari ya Larnaca nchini Cyprus, na shehena ya unga, mchele na bidhaa za protini. Zoezi hilo limefadhiliwa pakubwa na Umoja wa Falme za Kiarabu na linaendeshwa na shirika la misaada la World Central Kitchen (WCK) lenye makao yake makuu nchini Marekani.

Meli ya shirika la misaada la Open Arms iliyosheheni misaada ikielekea Ukanda wa Gaza
Meli ya shirika la misaada la Open Arms iliyosheheni misaada ikielekea Ukanda wa GazaPicha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Safari ya kuelekea Gaza kwa kawaida ingalichukua takriban saa 15 lakini kutokana na mashua hiyo kuwa inavuta mizigo mizito safari hiyo itakuwa ndefu, pengine itachukua hadi siku mbili. Cyprus iko zaidi ya kilomita 320 katika upande wa kaskazini-magharibi mwa Ukanda wa Gaza.

Kwingineko viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapanga kutoa tamko kuhusu kusitishwa vita mara moja kwa ajili ya kupisha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu na hatimaye kuwezesha hatua ya kudumu ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na wakati huo huo kuitaka Israel isianzishe operesheni ya ardhini katika mji wa Rafah.

Haya ni kulingana na yaliyomo kwenye rasimu ya mkutano wa kilele utakaofanyika wiki ijayo mjini Brussels. Rasimu hiyo itahitaji kuidhinishwa na nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Vita kati ya Israel na Hamas vilianza pale wanamgambo wanaoongozwa na Hamas walipovamia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, ambapo waisraeli wapatao 1,200, wengi wao wakiwa raia waliuawa. Watu wengine karibu 250 walichukuliwa mateka.

Soma Pia:Meli ya misaada ya chakula imeanza safari kutoka Cyprus kuelekea Gaza

Wizara ya Afya ya Gaza imesema mpaka sasa zaidi ya Wapalestina 30,000 wameuawa katika mashambulizi ya kijeshi ya Israeli na Wapalestina zaidi ya elfu 70 wamejeruhiwa.

Vyanzo: AFP/RTRE/DPA