1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wapambana na wanaharakati katika msitu wa Hambacher

6 Septemba 2018

Kampuni kubwa ya nishati nchini Ujerumani ya RWE inakusudia kuyafyeka maeneo zaidi kwenye msitu wa Hambacher ili kuendeleza uchimbaji wa makaa ya mawe lakini wakazi wa sehemu hiyo wanapinga kuharibiwa kwa mazingira yao.

https://p.dw.com/p/34PXS
Hambacher Forst RWE bereitet Rodung vor
Picha: DW/Sebastian Weiermann

Kwa muda wa miezi kadhaa sasa wanaharakati wa ulinzi wa mazingira wamepiga kambi kwenye msitu huo wa Hambecher ili kuzuia shughuli za kampuni hiyo za kuendelea kubomoa mazingira ili kuweza kuchimba makaa ya mawe. Mara nyingine msimamo wa wanaharakati hao unakuwa wa kutumia mabavu dhidi ya polisi. Sehemu ya msitu huo haijakuwa na utulivu kwa muda mrefu sasa imekuwa ishara ya harakati za kutetea mazingira.

Kwa mara nyingine hivi karibuni mamia kadhaa ya polisi walikwenda kwenye sehemu hiyo ya msitu  wa Hambacher. Pia wafanyakazi wa kampuni ya nishati ya RWE waliwasili kwenye msitu huo ili kuanza kutayarisha kazi ya kuusafisha kwa ajili ya kundeleza uchimbaji wa makaa ya mawe.

Mara kwa mara wanaharakati wa mazingira wamepambana na polisi na wafanyakazi wa kampuni hiyo. Msemaji wa polisi ameeleza kwamba wameweza kuondoa vitu vingi ikiwa pamoja na vile vya kutia mashaka, kwa mafano magurudumu ya gari yaliyotiwa misumari lakini wamesema baya zaidi ni kwamba wanaharakati hao wamewarushia polisi kinyesi na mkojo. Kwa maoni polisi, upinzani wa jambo lolote lile unapasa kuendeshwa vingine.

Bango kwenye mti katika msitu wa Hambacher linasema ''Mti huu haupaswi kukatwa kwa ajili ya makaa ya mawe''
Bango kwenye mti katika msitu wa Hambacher linasema ''Mti huu haupaswi kukatwa kwa ajili ya makaa ya mawe''Picha: DW/I. Banos Ruiz

Polisi wamesema kwa sasa wanafanya kazi yao kwa utulivu. Hapo awali walifikiri kuwa wangekabiliwa na upinzani mkubwa wa wanaharakati hao. Wapo wanaharakati wapatao 200 kwenye sehemu hiyo ya msitu wa Hambacher.

Hata hivyo hali inaweza kubadilika ikiwa nyumba zitabomolewa ili kutayarisha uchimbaji wa makaa ya mawe. Inapasa kutilia maanani kwamba wanaharakati hao wanaungwa mkono pia na vijana wa makundi ya mrengo mkali wa kushoto maarufu kama Atonomy.! Kiongozi wa kikundi cha watetezi wa mazingira Jan Pütz ametishia kuchukua hatua ikiwa shughuli za kukata miti zitasonga mbele.

Lakini kampuni ya nishati ya RWE nayo imesimama kidete na inataka kuendelea na mpango wake wa kuisafisha sehemu ya msitu wa Hambacher ili kazi ya kuchimba makaa ya mawe iweze kufanyika. Msemaji wa kampuni hiyo Jan Peter Cirkel amesema sehemu ya msitu wa Hambacher inapaswa kutayarishwa kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe. Amefahamisha kwamba kampuni yake imepata kibali cha matayarisho ya kuondoa kila kitu kilichopo kwenye sehemu ya msitu, kuanzia tarehe mosi ya mwezi ujao.

Mwandishi: Zainab Aziz/Wenkert, Thomas (WDR)
Mhariri: Bruce Amani