Ndege iliyombeba makamu wa rais wa Malawi yaanguka
11 Juni 2024Ndege iliyombeba Makamu wa Rais Saulos Chilima mwenye umri wa miaka 51 na mke wa rais wa zamani Bakili Muluzi, Shanil Dzimbiri ilitoweka Jumatatu asubuhi wakati ikiwa safarini kutoka mji mkuu wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika, Lilongwe, kuelekea mji wa Mzuzu, katika upande wa kaskazini. Safari ambayo huchukua dakika 45.
Akilihutubia taifa moja kwa moja kwenye televisheni usiku wa kuamkia leo, Rais Lazarus Chakwera alisema waongoza safari za ndege walimwambia rubani wa ndege hiyo kutojaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Mzuzu kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na kumtaka arudi Lilongwe. Waongoza safari za ndege kisha wakapoteza mawasiliano na ndege hiyo na ikatoweka kwenye mtambo wa rada. Chakwera aliapa kuwa shughuli za utafutaji zitaendelea hadi ndege hiyo itakapopatikana. "Najua hii ni hali ya kuvunja moyo. Najua sote tuna hofu. Nami pia nina wasiwasi. Lakini nataka kukuhakishieni kuwa nitatumia raslimali zote zilizopo kupata iliko ndege hiyo. Na nina matumaini kuwa tutawapata manusura." Abiria saba na wahudumu watatu wa kijeshi walikuwa kwenye ndege hiyo ndogo inayomilikiwa na jeshi la Malawi.
Kamanda wa jeshi la Ulinzi la Malawi Paul Valentino Phiri amesema kuwa huenda ndege hiyo ilianguka katika Msitu wa Chikangwa lakini haijapatikana. Amesema operesheni za utafutaji na uokozi zinakwamishwa na ukubwa wa eneo la msitu na hali ya hewa yenye ukungu mwingi.
Maafisa wamesema karibu watu 600 wanashiriki katika zoezi hilo la kuitafuta katika msitu wa milima ya Vimphya karibu na Mzuzu. Polisi 300 wameungana na jeshi na walinzi wa misitu katika operesheni hiyo. Msemaji wa shirika la Msalaba Mwekundu la Malawi Felix Washoni amesema maafisa wake pia wanashiriki katika shughuli hiyo na wanatumia droni ili kusaidia kuitafuta ndege hiyo.
Rais Chakwera amesema Marekani, Uingereza, Norway na Israel zimejitolea kusaidia katika operesheni ya utafutaji. Ameuomba umma kujiepusha kusambaza taarifa za uwongo mitandaoni kuhusu tukio hilo. "Nimewaagiza maafisa wa Wizara ya Ulinzi wanaosimamia operesheni hiyo kuwapeni, kila mmoja, taarifa za mara kwa mara jinsi operesheni hiyo inavyoendelea ili wote mpate taarifa kuhusu hatua za kubaini kilichotokea kwa wapendwa wetu, na raia wenzetu waliokuwa katika ndege hiyo."
Makamu wa Rais Chilima na kundi lake walikuwa safarini kuhudhuria mazishi ya Waziri wa zamani wa serikali. Chilima alikuwa amerejea nchini kutoka ziara rasmi Korea Kusini siku ya Jumapili. Amekuwa makamu wa rais tangu 2020. Alikuwa mgomeba katika uchaguzi wa rais Malawi mwaka wa 2019 na akamaliza wa tatu, nyuma ya rais aliyeondoka Peter Mutharika, na Chakwera. Matokeo hayo yalibatilishwa baadaye na Mahakama ya Kikatiba ya Malawi kwa sababu ya dosari. Chilima kisha akajiunga na timu ya Chakwera kama mgombea mwenza katika duru ya pili ya uchaguzi wa kihistoria mwaka wa 2020, ambapo Chakwera alichaguliwa kuwa rais.
Reuters, AP