Wasifu wa Rais mpya wa Malawi
28 Juni 2020Rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera alikuwa muhubiri wa kanisa la kiinjili ambaye anasema aliingia kwenye siasa kuitikia mwito wa Mungu wake. Chakwera mwenye umri wa miaka 65 katika kipindi cha miaka saba iliyopita alikiongoza chama kikongwe kabisa nchini Malawi cha Malawi Congress Party MCP ambacho kiliitawala nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kuanzia mwaka 1964 hadi 1994 chini ya utawala wa chama kimoja wa dikteta Hastings Kamuzu Banda.
Harakati zake kisiasa
Chakwera alikiongoza chama hicho katika mwaka 2014 katika uchaguzi mkuu ambapo alishikilia nafasi ya pili akiwa nyuma ya Peter Mutharika katika uchaguzi wa rais. Kabla ya uchaguzi wa mwaka jana 2019 chama cha MCP kilishindwa katika chaguzi nne za urais tangu mwaka 1994 lakini Chakwera alifanya juhudi kubwa kukijenga upya chama hicho,akikitenganisha na utawala wa Banda aliyeongoza kwa mkono wa chuma na kukipa nguvu mpya.
Baada ya Chakwera kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana uliompa ushindi mwembamba Mutharika mwenye umri wa miaka 79, alianzisha kile kilichokuja kugeuka kuwa mapambano makubwa ya kisheria ya kihistoria.
Uchaguzi huo hatimae ulibatilishwa na mahakama ya juu kabisa ya Malawi ambayo ilibaini zilikuweko dosari nyingi ikiwemo kutumika kwa wino kufuta matokeo. Uamuzi huo wa mahakama kuu ya Malawi ulilitikisa bara zima la Afrika ambako viongozi walioko madarakani ni nadra kushindwa kwenye uchaguzi achilia mbali kupitia vyombo vya sheria.
Uchaguzi wa marudio ukaitishwa Juni 23 na Chakwera akatwaa ushindi wa kishindo akiibuka kidedea kwa kunyakua asilimia 58 ya kura kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.
Ahadi
Kiongozi huyo punde baada ya ushindi aliwaambia waandishi habari wa AFP kwamba watu wanataka mabadiliko,wanadai mabadiliko na wanawaona wapinzani kama sura ya mabadiliko''
Chakwera katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi alipata uungaji mkono wa watu maarufu nchini Malawi ikiwemo makamu wa rais Saulos Chilima,aliyekuwa rais wa taifa hilo Joyce Banda na vyama vingine vingi vidogo vya kisiasa.
Katika hotuba yake aliyoitowa Jumapili baada ya kuapishwa Chakwera aliahidi kwamba serikali yake itakuwa yenye kuwatumikia wananchi na sio ya kuwatawala,serikali itakayowahamasisha na sio kuwaghadhabisha na serikali itakayosikiliza badala ya kukemea na mwisho itakuwa serikali ya kupambana kwa ajili ya wananchi wake na sio kupambana dhidi yao.
Anatokea wapi?
Chakwera alizaliwa katika kijiji kilichoko karibu na mji mkuu Lilongwe ambacho hakina umeme wa maji ya bomba akitokea katika familia ya mkulima ambaye watoto wake wawili wakubwa wakiume walifariki wakiwa bado wachanga.Chakwera alipewa jina Lazarus ambalo ni la mtu aliyetajwa kwenye kitabu cha bibilia kwamba alifufuliwa miongoni mwa wafu.
Alisomea filosofia na thiolojia na kupata shahada ya kwanza na alikuwa rais wa baraza la makanisa nchini Malawi kuanzia mwaka 1989 hadi 2013 kabla ya kuwa kiongozi wa chama cha kisiasa cha MCP.
Kwa miaka mingi alikuwa akijihusisha sana na kamati ya masuala ya umma inayoheshimika sana nchini Malawi,likiwa ni kundi la misingi ya kidini la mashirika ya kutetea haki za kiraia,akiwa kama mtetezi wa masuala ya uongozi bora. Rais huyo mpya wa malawi anayezungumza kiingezera cha lafudhi ya kimarekani anasema anapenda kusoma na muziki wa kiasili,kimagharibi,na muziki wa kidini. Ameliambia shirika la habari la AFP hivi karibuni kwamba anapenda kuimba sana hata akiwa peke yake bafuni akioga.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Tatu Karema