1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olimpiki: Kenya yaandamwa na kivuli cha kututumua misuli

24 Julai 2024

Wanariadha wa mbio za masafa marefu wa Kenya waelekea kwenye Michezo ya Olimpiki wakihangaika kujiondoa kwenye orodha ndefu ya kashfa za matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

https://p.dw.com/p/4idt5
WADA
Nembo ya Shirika la Kupambana na Dawa za kututumua misuli (WADA) Picha: picture-alliance/dpa/EPA/J. C. Bott

Wanariadha wa mbio za masafa marefu wa Kenya waelekea kwenye Michezo ya Olimpiki wakihangaika kujiondoa kwenye kivuli cha orodha ndefu ya kashfa za matumizi ya dawa za kusisimua misuli ambazo zimeharibu sifa ya kujivunia ya taifa hilo la Afrika.

Soma pia: Wanamichezo wakimbizi walenga kutimiza ndoto zao Paris

Mwanariadha wa mbio za Marathon Beatrice Toroitich amekuwa mwanariadha wa hivi punde zaidi wa Kenya kuasi sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli mwezi uliopita alipopigwa marufuku ya maisha kushiriki riadha,  baada ya kupimwa kwa mara ya tatu na kubainika kuwa na dawa hiyo.

Kesi hiyo ilifuatia adhabu ya miaka sita aliyowekewa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 10 Rhonex Kipruto mapema mwezi Juni, huku mkimbiaji wa masafa marefu Rodgers Kwemoi pia akipigwa marufuku kwa miaka sita kwa kukiuka matumizi ya dawa za kusisimua misuli mwezi Mei.

Soma pia: Waandalizi wa Olimpiki Paris wasema wako tayari kwa Michezo

Idadi inaendelea kuongezeka

Olympiki
Mwanariadha wa Kenya wa mbio za masafa marefuPicha: Dylan Martinez/REUTERS

Kwa jumla takriban wanariadha 100 wa Kenya, hasa wanariadha wa mbio za masafa marefu, wamekabiliwa na vikwazo kwa makosa ya utumiaji wa dawa za kulevya tangu 2017, baada ya kunaswa katika msako mkali ulioendeshwa na Chama cha Kupambana na Matumizi ya Madawa ya Kulevya nchini Kenya (ADAK) kufuatia kashfa za matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.

"Kenya inapiga hatua kubwa katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli," afisa mkuu mtendaji wa ADAK Sarah Shibutse aliambia AFP katika mahojiano. "Hatulegei katika pambano hili ambalo ni kiini cha fahari yetu ya kitaifa."

Wanariadha wa Kenya wanaoshiriki mashindano mjini Paris wamefanyiwa vipimo kwa umakini, vipimo  matatu ya nje ya mashindano katika muda wa miezi 10 kabla ya michuano ya Olimpiki.

Wakuu wa Kenya wanaokabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli wameomba uungwaji mkono kutoka kwa kitengo huru cha Uadilifu wa Riadha (AIU), wizara ya michezo ya Kenya na vyombo vya sheria kusaidia katika uchunguzi na kupima wanariadha.

Shibutse alisema kuwa kwa upande wake kumesababisha kufungwa kwa maduka ya dawa kadhaa katika Bonde la Ufa -- kitovu cha mbio za Kenya ambako wanaoshukiwa husambaza dawa za kuongeza nguvu kwa wanariadha.

Upimaji wakati huo huo umeongezeka sana, na vipimo 2,000 vimefanywa katika mwaka uliopita. ADAK inalenga kuongeza idadi hiyo mara tatu hadi 6,000 kwa mwaka.

Soma pia: Juhudi za kuboresha riadha Kenya

Shibutse anasema idadi ya vipimo itaendelea kuongezeka hadi "wanariadha waelewe kuwa tunafanya hivi kwa manufaa yao wenyewe."

"Tuna sampuli nyingi zinazokusanywa ambayo ina maana kwamba kesi nyingi chanya za kusisimua misuli zinagunduliwa kuliko hapo awali. Hii ni ishara kwamba mchakato unafanya kazi," Shibutse alisema.

Wakati wa safari ya kutafuta ukweli nchini Kenya mnamo Machi 2023, mkuu wa AIU Brett Clothier alionya kwamba wanariadha walihitaji kujipanga ili kuchukua hatua kali dhidi ya utumiaji wa hizo katika riadha.

"Jambo moja ambalo kila mtu anapaswa kufahamu ni kwamba kwa kupima zaidi, kesi zaidi zitaripotiwa, lakini hiyo haimaanishi utumiaji wa dawa hizo hauzidi. Lakini hii ndio njia sahihi ya kushughulikia tatizo hili mara moja na kwa wote," Clothier alisema.

Mbinu ya ufuatiliaji wanariadha

Olympiki Tokyo | Emmanuel Korir na Ferguson Rotich
Wanariadha wa Kenya Emmanuel Korir na Ferguson RotichPicha: LUCY NICHOLSON/REUTERS

Mkuu wa elimu na utafiti wa kupambana na dawa za kusisimua misuli ADAK Martin Sisa Yauma alisema matumizi ya kufuatilia vinasaba vya kibaolojia vilivyochaguliwa kwa muda ambavyo vinafichua madhara kwa njia isiyo ya moja kwa moja ya matumizi ya dawa za kusimumua misuli (ABP), ambayo hufuatilia maadili ya damu ya mwanariadha kwa wakati, yametumika ipasavyo kuwanasa watumiaji wa dawa hizo hivi majuzi akiwemo Kipruto, bingwa wa dunia wa mbio za mita 10,000. Rodgers Kwemoi na bingwa wa zamani wa Jumuiya ya Madola na  bingwa wa Afrika katika mbio za mita 10,000 Joyce Chepkirui.

Kwa wanariadha wanaojaribu kujenga upya taaluma zao baada ya kunaswa na matumizi ya dawa za kusisimua misuli, njia ya kurudi kwenye mashindano mara nyingi ni ngumu.

Mark Otieno, bingwa wa zamani wa kitaifa wa mbio za mita 100, ambaye alipigwa marufuku kwa miaka miwili kwa kutumia dawa iliyopigwa marufuku ya anabolic steroid methasterone kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, alirejea Novemba mwaka jana kujaribu kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris.

"Sitamani marufuku ya dawa za kuongeza nguvu itokee kwa mtu mwingine," alisema Otieno, baada ya kushindwa kufuzu kwa mbio za Olimpiki za mita 100 kwa kutimka kwa sekunde 10.00.