1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala kufungwa Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa Uganda

7 Agosti 2023

Hatua ya kufungwa kwa ofisi ya kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu nchini Uganda imepokelewa kwa wasiwasi mkubwa miongoni mwa watetezi wa haki wakihofia serikali haitawajibika.

https://p.dw.com/p/4UsF1
Schweiz | Menschenrechtsrat Volker Tuerk
Picha: Pierre Albouy/KEYSTONE/picture alliance

Mnamo mwezi Februari, serikali ya Uganda ilimfahamisha kamishna wa Umoja Mataifa anayehusika na haki za binaadamu kuwa muda wa mkataba wa uwepo wa ofisi hiyo usingerefushwa.

Mwezi uliofuata, Rais Yoweri Museveni alinukuliwa akitaja uwepo wa ofisi hiyo nchini Uganda kuwa jambo linalowapotosha watu kutojua ni wapi hasa wanastahili kuwasilisha malalamiko yao kuhusiana na kukiukwa kwa haki zao. 

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa umezifunga ofisi zao za Haki za Binadamu nchini Uganda

Tamko hilo likafasiliwa kuwa maamuzi yalikuwa yameshafanywa na hata jaribio la kuishawishi serikali kubadili msimamo wake halingefanikiwa.

Ofisi zafungwa rasmi

Sasa ofisi hizo zilifungwa rasmi Jumamosi (Julai 5) na kuwaacha wanaharakati wa haki za binaadamu katika mashaka kuhusiana na hali ya baadaye ya raia kuhusiana na haki zao za binaadamu.

Yoweri Musevini to sign anti-LGBT law
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

"Ofisi hii imechangia pakubwa katika kuhamasisha umma kuhusu haki za binaadamu kwa kiwango fulani, ambapo hata watoto walio chini ya miaka 15 wamekuwa wakifahamu hali ambapo haki zao hukiukwa kuanzia ngazi ya familia," anasema Dk. Livingstone Sewanyana, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa wakfu wa mtandao wa mashirika ya haki za binaadamu.

Soma zaidi: Ofisi ya haki za binaadamu kufungwa Uganda

Kwa upande wa wanahabari, mafunzo waliyoyapata kutoka kwa ofisi hiyo yaliwawezesha kuhusika moja kwa moja katika kufichua visa vya ukiukaji wa haki za binaadamu na kuwawajibisha wahusika, kwa mujibu wa murugenzi wa mtandao unaoshughulikia haki za binaadamu za waandishi habari, Robert Sempala.

Unyamazishaji wanaharakati wazidi

Mwenendo wa kudhibiti na kunyamazisha asasi mbalimbali za kiraia ambazo zilihusika katika harakati za kulinda haki za binaadamu umekuwa ukishuhudiwa pale baadhi zilivyonyimwa vibali vya kuendesha kazi zao au hata ofisi zao kuvunjwa na vifaa vyao kuporwa.

Uganda | Anti-LGBTQ Proteste in Kampala 2014
Waandamanaji wanaounga mkono sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.Picha: Ronald Kabuubi/dpa/picture alliance

Wadau sasa wanaitaka serikali ibebe jukumu la kulinda na kuwajibikia haki za binadamu.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia uvunjwaji haki za binaadamu Uganda

"Kwa sababu vyombo vya dola ndivyo hutajwa kila mara kukiuka haki hizo, tunataka kuwepo na mfumo ambao unahakikisha kuwa watu binafsi katika taasisi za kisheria kama vile polisi wanaadhibiwa kwa vitendo vyao,"  anasema Dk. Livingstone.

Ofisi hiyo ilifunguliwa mwaka 2005 kuchangia katika kufuatilia ukiukaji wa haki za binaadamu katika kipindi cha sintofahamu hasa kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo waasi wa LRA walihusishwa na visa vya ukatili.

Mwaka 2009, mkataba husika uliongezewa muda ili kushughulikia masuala yote ya haki za binaadamu kote nchini.

Katika taarifa aliyosambaza kwa vyombo vya habari, Kamishna Mkuu wa shirika hilo, Volker Tuerk, alielezea masikitiko yake kuhusu hali ya baadaye ya haki za binaadamu nchini Uganda hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2026.

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala