1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mizozo ya Ukraine na Gaza yatawala Jukwaa la Shangri-La

1 Juni 2024

Mkutano wa masuala ya usalama unaowaleta pamoja maafisa wa ngazi ya juu wa ulinzi duniani umeingia siku ya pili leo Jumamosi nchini Singapore.

https://p.dw.com/p/4gWua
Ujumbe wa China kwenye mkutano wa usalama wa Shangri-La unaofanyika Singapore.
Ujumbe wa China kwenye mkutano wa usalama wa Shangri-La unaofanyika Singapore.Picha: Roslan Rahman/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa kila mwaka unaojulikana kama Jukwaa la Majadiliano ya Usalama la Shangri-Launafanyika kwenye mji mkuu wa Singapore, Singapore City.

Mwaka huu majadiliano yametawaliwa zaidi na mzozo wa Gaza, vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi pamoja na suala la usalama kwenye kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki.

Mapema leo asubuhi Rais Mteule wa Indonesia Prabowo Subianto aliwaambia wajumbe wanaohudhuria mkutano huo kwamba nchi yake iko tayari kutuma wanajeshi wa kulinda amani kusaidia utekelezaji makubaliano ya kusitisha mapigano ya ukanda wa Gaza pindi yakapoafikiwa.

Prabowo alikuwa akizungumzia pendekezo la kusitisha mapigano la awamu tatu lililotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden.

Pendekezo hilo ambalo kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza limesema "linatia moyo" na linalitafakari limetoa matumaini ya uwezekano wa kumalizwa vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi saba.

Chini ya mpango huo Biden amesema Israel imependekeza hatua tatu muhimu za kumaliza vita.

Hatua ya kwanza itakuwa ni kipindi cha wiki sita cha usitishaji mapigano ambacho kitashuhudia vikosi vya Israel vikiondoka kwenye miji yote iliyo na watu wengi kwenye Ukanda wa Gaza.

Kisha itafuatiwa hatua ya pili na ya tatu inayojumuisha kubadilishana mateka wote na wafungwa, na baadae vikosi vya Israel vitaondoka kikamilifu na mpango wa kuijenga upya Gaza utaanza.

Prabowo amesema pendekezo hilo ni hatua iliyopigwa katika muelekeo unaostahili.

"Ingawa inabidi tuangalie na kuchunguza kwa makini kilichopo ndani ya pendekezo hili lililotangazawa na rais Joe biden, (lakini) tunaliona kama hatua muhimu hatua muhimu iliyochukuliwa katika kusonga mbele" amesema kiongozi huyo ambaye bado anashikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi wa Indonesia.

Prabowo mwenye umri wa miaka  72, amesema iwapo wataombwa na Umoja wa Mataifa kuchangia katika hatua za kusitisha mapigano basi wako tayari kutuma kikosi cha kulinda amani kusimami utekelezaji makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na kutoa ulinzi na usalama kwa pande zote zinazohasimiana.

Subianto aliyeshinda urais katika uchaguzi wa mapema mwaka huu anatarajiwa kuchukua wadhifa huo mnamo mwezi Oktoba kuongoza taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya waislamu duniani.

Zelensky kuhutubia jukwaa la Shangri-La siku ya Jumapili 

Singapore|Jukwaa la Usalama | Volodoymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodoymyr Zelensky akiwasili kwenye ukumbi wa mkutano wa Jukwaa la Usalama la Shangri-La nchini Singapore. Picha: Vincent Thian/AP Photo/picture alliance

Jukwaa la Shangri-La pia litakuwa uwanja mwingine wa kujadili hali ya usalama duniani inayotiwa kiwingu na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amewasili Singapore kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Shangri-La akilenga kuvutia uungwaji mkono wa kimataifa kwa utawala wake mjini Kyiv katika vita dhidi ya Urusi.

Alipowasili kwenye ukumbi wa mikutano alishangiliwa na watu waliokuwepo kwenye ukumbi wa mapokezo na kisha akasalimiana na maafisa kadhaa wa masuala ya ulinzi kutoka kila pembe ya dunia wanaoshiriki mkutano huo wa siku tatu. Zelensky anatawajiwa kulihutubia Jukwaa la Shangri-La kesho Jumapili (02.06.2024)

Ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba "nitafanya mikutano kadhaa, ikiwemo na Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam  na Waziri Mkuu Lawrence Wong, Rais wa Timor Jose Ramos-Horta, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austina na wawekezaji wa Singapore".

Zelensky amekuwa akifanya ziara kwenye mataifa ya Ulaya mnamo siku za karibuni kuomba misaada ziada ya kijeshi kwa ajili ya askazi wake katikati mwa hujuma nzito za Urusi inayosonga mbele kwenye uwanja wa vita.

Safari yake nchini Singapore haikutangazwa hadi dakika za mwisho kabisa kabla ya kuwasili kwenye hoteli kunapofanyika mkutano huo wa Shangri-La.

Suala la usalama kanda ya Asia na Pasifiki miongoni mwa ajenda za juu 

Katika hatua nyingine Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amehutumia mkutano wa Shangri-La leo Jumamosi na kusifu kile amekiita "enzi mpya ya usalama" kwenye kanda ya Asia na Pasifiki.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani  Lloyd Austin
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd AustinPicha: Chad J. McNeeley/US Dod/EPA

Matamshi yake ameyatoa wakati Washington inaonesha kufanikiwa katika sera yake ya kuimarisha mahusiano na washirika wake wa kanda hiyo kwa lengo la kuidhibiti China.

Marekani imekuwa ikiwaenga enga na kuwaleta karibu washirika wake tangu Japan hadi Australia, Korea Kusini na hata Ufilipino na kwa sehemu fulani utawala wa kisiwa cha Taiwan.

Dhamira yake kubwa ni kuzuia kutanuka kwa nguvu za kijeshi na ushawishi wa China kwenye kanda hiyo.

Austin amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa na "mabadiliko mapya kwenye maeneo yote ya ajenda ya ulinzi" kwenye kanda ya Asia na Pasifiki.

Hata hivyo China imejibu matamshi hayo ya Austin kwa kuituhumu Marekani kutaka kuunda mfungamano wa kijeshi unaofanana na ule wa Jumuiya ya NATO kwenye kanda hiyo.