1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Mazungumzo ya deni la Marekani yakwama tena

Sylvia Mwehozi
20 Mei 2023

Mazungumzo ya ukomo wa deni la Marekani yamekwama kwa mara nyingine muda mfupi baada ya kuanza tena. Awali mazungumzo hayo yalisimama ghafla baada ya Spika wa bunge Kevin McCarthy kutangaza mapumziko.

https://p.dw.com/p/4RbCj
USA Washington | Schuldenstreit | Joe Biden
Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Mapema siku ya Ijumaa, mazungumzo ya pande mbili ya vyama vya Republican na Democratic yalisimama ghafla baada ya Spika wa bunge Kevin McCarthy kutangaza  kuwa ulikuwa ni muda wa kuchukua mapumziko na afisa mmoja wa Ikulu ya White House kukiri kwamba kuna tofauti. 

Soma:Biden aakhirisha ziara za nje kwa mzozo wa madeni

Wazungumzaji wakuu upande wa Republican waliondoka kwenye mazungumzo hayo muda mfupi baada ya kuanza tena Ijumaa jioni. Walisema hakuna mazungumzo zaidi yalipangwa kufanyika Ijumaa na hawakuwa na uhakika hatua zitakazo fuata. Lakini mshauri mkuu wa Ikulu ya White House kwa Rais Joe Biden alisema wana matumaini ya kupatikana suluhisho la haraka.

Marekani -Washington -White House
Rais Joe Biden alipokutana na Spika wa Bunge Kevin McCarthy katikati kushoto, Kiongozi wa Seneti Chuck Schumer kulia, Kiongozi wa Wachache katika Seneti Mitch McConnell.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Awali, Spika wa bunge McCarthy alidai kuwa suluhisho jepesi la mkwamo huo ni ikiwa tu timu ya Rais Joe Biden itakubali baadhi ya mapendekezo ya Republican ya kubana matumizi. "Lazima tupumzike", Spika McCarthy aliwaeleza waandishi wa habari bungeni akiongeza kuwa "hatutatumia fedha zaidi mwakani".

Wawakilishi wa Rais Joe Biden wamekwama katika mazungumzo na Warepublican wakitafuta kufikia makubaliano ya kuongeza kiwango cha kukopa cha Marekani na kuruhusu nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani kuepuka kushindwa kulipa deni lake. Hatari ya Marekani kushindwa kulipa deni lake inaweza kusababisha mtikisiko katika soko la dunia huku wawekezaji wakifuatilia kwa karibu mazungumzo hayo.

Chama cha Republican kinamtaka Biden kupunguza matumizi ili kiweze kumuunga mkono katika kuiongezea serikali kiwango cha kukopa, na kupuuza wito wa mara kwa mara wa chama cha Democratic wa nyongeza safi ya kiwango cha ukopaji bila ya masharti yoyote. Wademocrats wameanzisha mazungumzo hayo kama fursa ya kujadili bajeti ijayo wakati wizara ya fedha itakapotabiri kwamba Marekani inaweza kushindwa kulipa madeni yake na athari mbaya za kiuchumi.

Janet Yellen -Rais Joe Biden
Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen na Rais Joe BidenPicha: AP/Patrick Semansky/picture alliance

Ikulu ya Marekani White House imekiri kuwepo na tofauti baina ya pande zote mbili juu ya bajeti. Afisa mmoja wa White House amesema katika taarifa yake kwamba "kuna tofauti za kweli kati ya pande zote kuhusu masuala ya bajeti na mazungumzo yatakuwa magumu. Timu ya Rais inafanya kazi kwa bidii ili kupata suluhisho la kuridhisha la pande mbili ambalo linaweza kupitishwa na Bunge na Seneti. "

Kusimama ghalfa kwa mazungumzo ya Ijumaa, kulitokea siku moja baada ya Spika McCarthy kuashiria matumaini kwamba anaweza kuwasilisha muswada wiki ijayo, ingawa makubaliano ya kimsingi yatahitaji kufikiwa mwishoni mwa juma.

Wakati Republican wakihimiza kupunguzwa kwa matumizi na mabadiliko ya kisera, Biden naye amekabiliwa na ukosoaji ndani ya chama chake cha Democratic haswa wapenda maendeleo ambao wanadai kwamba hatua hizo zitaathiri programu za ndani zinazotegemewa sana na wamarekani.

Baadhi ya wanachama ndani ya chama chake wanamtaka Biden kutumia mamlaka yake chini ya kifungu namba 14 cha katiba ili kuongeza kiwango cha kukopa, wazo ambalo linaweza kuibua hoja za kisheria na hadi sasa Rais mwenyewe amekataa kulitilia maanani.