1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Mawaziri wa G7 wajadili juu ya kadhia ya deni la Marekani

12 Mei 2023

Mawaziri wa fedha wa kundi la mataifa saba tajiri (G7) wanaokutana kwenye mji wa pwani wa Niigata nchini Japan leo wamejadili namna ya kuepusha athari iwapo Marekani itashindwa kulipa deni lake la taifa.

https://p.dw.com/p/4RHeL
Japan | G7 Finanzministertreffen in Niigata
Mawaziri wa fedha wa kundi la mataifa saba tajiri G7 katika picha ya pamoja kwenye mkutano Niigata, Japan.Picha: Issei Kato/REUTERS

Mawaziri hao wa fedha wa nchi saba tajiri wamejadili juu ya umuhimu huo mkubwa ambapo iwapo itatokea Marekani ishindwe kulipa deni lake la taifa basi itakuwa ni kwa mara ya kwanza kabisa kwa taifa hilo kubwa lenye nguvu ya uchumi duniani kushindwa kuwajibika katika ulipaji wa deni la taifa.

Rais wa Benki ya Dunia David Malpass ameliambia shirika la Habari la Reuters pembezoni mwa mkutano wa G7 kwamba ni wazi, kwa taharuki illiyopo katika taifa kubwa kiuchumi duniani na endapo Marekani itashindwa kulipa deni lake la taifa hali hiyo itasababisha matatizo makubwa duniani.

Soma pia: Mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi za G7 waanza katika mji wa pwani wa Niagara nchini Japan.

Malpass amesema leo hii pia mawaziri pamoja na magavana wa benki kuu wa G-7 wamejadili kuhusu haja ya kuongeza tija na ukuaji wa uchumi, na kukabiliana na msongamano mkubwa wa madeni unaozikabili nchi kadhaa huku idadi ya nchi hizo ikizidi kuongezeka.

Washington yaondoa hofu juu ya hazina ya Marekani kuishiwa fedha

Weltbankpräsident David Malpass
Rais wa Benki ya Dunia David MalpassPicha: ANDREW KELLY/REUTERS

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner amesema leo kwamba anatumai wanasiasa nchini Marekani watafikia uamuzi kwa kutumia busara juu ya suala la kuongeza ukomo wa deni la taifa hilo, na yeye pia ametahadharisha juu ya hatari kwa uchumi wa dunia ikiwa Marekani itashindwa kulipa deni la taifa.

"Uchumi wa dunia unaweza kuathirika kutokana na michakato ya kisiasa, masoko ya fedha vilevile yatakabiliwa na hatari kubwa, ndiyo maana tunaitazama Marekani hasa wakati huu na tunatumai kwamba wabunge wa nchi hiyo watafikia uamuzi wa busara kwa kutilia maanani yanayoendelea katika serikali yao kuhusu suala la kuongeza kikomo cha deni lakini pia tunatumai wabunge wa Marekani watazingatia athari zinazoweza kuukumba uchumi wa dunia."

Soma pia: G7 yaonya dhidi ya kuubadilisha mfumo wa kimataifa kwa nguvu

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amesema bado hakuna uhakika kuhusu lini hazina ya Marekani inaweza kuwa imeishiwa fedha na hivyo kushindwa kulipa deni la taifa, lakini ameahidi kwamba atalifahamisha bunge kuhusu mabadiliko yoyote iwapo yatakuwepo kabla ya tarehe mosi mwezi wa sita.

Mkutano huo wa mawaziri wa fedha unaohudhuriwa pia na magavana wa benki kuu wa nchi za G7 unafanyika katika jiji la Japan la Niigata kwa siku tatu hadi kesho Jumamosi.

Mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G7 unatarajiwa kuanza tarehe 19 mwezi huu wa Mei katika jiji la Hiroshima nchini Japan.