1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani kuhusu vita vya Ukraine yafanyika Saudia

7 Agosti 2023

Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 40 wamekutana Jumapili nchini Saudi Arabia ili kujaribu kuutafutia suluhu mzozo wa Ukraine, na wameafikiana kuendeleza "mashauriano ya kimataifa" ili kujenga msingi wa pamoja wa amani.

https://p.dw.com/p/4UqA8
Saudi Arabien, Dschidda | Ukraine Gipfeltreffen
Picha: Saudi Press Agency/Handout/REUTERS

Miongoni mwa walioshiriki mazungumzo hayo mjini Jeddah ni wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na washauri wa kiusalama kutoka mataifa ya Ukraine, Marekani, Ujerumani, China, India, Brazil na Afrika Kusini. Urusi haikualikwa kuhudhuria mkutano huo lakini ilikuwa ikipewa taarifa na wajumbe wa Saudia kuhusu maendeleo ya mazungumzo hayo.

Saudi Arabia, ambayo imeandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano huo, imesema lengo ni kutafuta "njia ya kisiasa na kidiplomasia" ya kumaliza vita vya Ukraine . Kwa ujumla wajumbe hao wameafikiana juu ya umuhimu wa kuendelea na mashauriano ya kimataifa na kubadilishana maoni ili kujenga msingi wa pamoja ambao utafungua njia ya amani.

Wanadiplomasia waliofuatilia kwa karibu mazungumzo hayo wameliambia hapo jana shirika la habari la dpa kwamba Saudi Arabia na mataifa mengine kadhaa walipendekeza muelekeo wa mpango huo wa amani kwa ajili ya Ukraine huku wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia mapendekezo hayo.

Soma pia: Ukraine yataka juhudi zaidi za kuleta amani kwenye mkutano nchini Saudi Arabia

Wanadiplomasia hao wamesema ni muhimu kuona China ambayo ndio mshirika mkuu wa Urusi, imehudhuria mazungumzo hayo. Ikumbukwe kuwa Beijing haikushiriki mkutano wa awali wa kimataifa uliofanyika huko Copenhagen nchini Denmark mnamo mwezi Juni.

Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya (EU) amesema China ilishiriki kikamilifu na kupokea vyema wazo la mkutano wa tatu wa aina hiyo. Wanadiplomasia wa Umoja huo wamebaini kuwepo kwa uungwaji mkono mpana wa kuendelea majadiliano kuhusu misaada ya kibinadamu, usafirishaji wa chakula pamoja na masuala ya nyuklia na mazingira.

Saudi Arabien, Dschidda | Ukraine Gipfeltreffen
Wajumbe wa nchi zaidi ya 40 wakifanya mazungumzo mjini Jeddah kuhusu mzozo wa Ukraine (06.08.2023)Picha: Saudi Press Agency/Handout/REUTERS

Wanadiplomasia wa Magharibi wanatumai kuwa mkutano wa Jeddah ungeliweza kuongeza uungwaji mkono kwa Ukraine kutoka nchi zinazoendelea,ambazo baadhi hazijachukua msimamo uliyo wazi juu ya mzozo huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameliambia gazeti la Bild am Sonntag kuwa kila hatua ya maendeleo kuelekea amani ya haki huleta matumaini kwa watu wa Ukraine.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika matarajio ya mpango huo wa amani, ni usitishwaji mapigano kwa pande zote, kuanzisha mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine  na yatakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, kuheshimu mipaka ya Ukraine na kubadilishana wafungwa. Hata hivyo, haikubainika ni nchi gani nyengine mbali na Saudia zilizounga mkono pendekezo hilo.

Msimamo wa Ukraine na Urusi

Andrii Yermak, ambaye aliongoza ujumbe wa Ukraine kwenye mkutano huo, amesema licha ya maoni tofauti, nchi zote zilizohudhuria mikutano iliyojitolea kuheshimu mikataba, sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa, zinaafiki msimamo wa kuheshimu uhuru na mipaka ya nchi yake.

Soma pia: Saudi Arabia yaandaa mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema: " Leo ni siku nyingine inayoonesha juhudi zetu za kimataifa. Wajumbe wetu wanafanya kazi mjini Jeddah, Saudi Arabia, katika mkutano wa washauri wa viongozi wa nchi kuhusu Mfumo wa Amani. Kwa jumla, nchi 42 zinawakilishwa huko. Mabara tofauti, mbinu tofauti za kisiasa kwa masuala ya kimataifa, lakini kila mtu anashughulishwa na kipaumbele cha sheria za kimataifa."

Pendekezo la amani la rais Volodymyr Zelensky  linajumuisha kuondolewa kwa askari wote wa Urusi katika ardhi ya Ukraine na kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita na Mahakama ya kimataifa, pamoja na kupewa dhamana ya kimataifa ya usalama.

Saudi Arabien Wolodymyr Selensky und Prinz Badr bin Sultan bin Abdulaziz
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiwa na Mwanamfalme Badr bin Sultan bin Abdulaziz wakati akiwasili mjini Jeddah kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (19.05.2023)Picha: STR/AFP

Wajumbe kutoka baadhi ya nchi walifanya mikutano pembezoni mwa mazungumzo hayo ya siku ya Jumapili. Mshauri mkuu wa Usalama wa Ikulu ya Marekani Jake Sullivan alikutana na Yermak, ambaye ndiye mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine.

Urusi imekuwa ikitoa kauli tofauti kufuatia mazungumzo hayo. Awali Ikulu ya Kremlin ilisema itafuatilia kwa karibu mkutano huo lakini msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova, amesema mazungumzo hayo bila ushiriki wa Urusi ni upuuzi mtupu, huku msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov akiliambia Gazeti la New York Times kwamba kwa sasa hakuna msingi wowote wa makubaliano na Ukraine na kwamba operesheni ya kijeshi ya Urusi itaendelea.

Soma zaidi: China kushiriki mazungumzo ya Jeddah kuhusu mpango wa amani wa Ukraine

Mara kadhaa Saudi Arabia imekuwa ikipendekeza kusimamia upatanishi katika mzozo wa Urusi na Ukraine. Mwaka jana Riyadh ilitangaza kuwa ilisaidia katika zoezi la kubadilishana wafungwa kati ya Kyiv na Moscow. Mwezi Mei, Zelenskiy alihudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu uliofanyika Saudia.

Ufalme huo wenye utajiri mkubwa wa mafuta pamoja na majirani zake wa Ghuba hadi sasa wanapinga shinikizo la Magharibi la kukata mawasiliano na Urusi tangu ilipoanzisha uvamizi wake nchini Ukraine Februari mwaka jana.