1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yatokea tena Kaskazini Mashariki mwa Congo

16 Desemba 2019

Waasi wa kundi la ADF wameishambulia tena wilaya ya Beni Kaskazini mwashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuwa watu 22 katika tarafa za Ndombi na Kamango.

https://p.dw.com/p/3UsmS
Symbolbild Opfer der ADF
Picha: Getty Images/AFP/K. Mailro

Wakaazi wa wilaya ya Beni kwa mara nyingine wanahesabu maiti za wapendwa wao waliouawa kinyama na waasi wa ADF. Mmoja wa wakaazi aliyeponea chupuchupu katika eneo la Kamango, aliyezungumza na DW kwa njia ya simu, amesema walipoingia kijijini mwake waasi hao kutoka Uganda ADF walikuwa wakiuwa watu kiholela.

"Walipoingia walianza kuwafyetulia raia risasi, waliojeruhiwa ni wengi na waliouawa wapo. Milio ya risasi ilikuwa mingi kupita kiasi, jeshi liliingilia kati lakini lilichelewa kidogo. Isingelikuwa uingiliaji kati wa jeshi hilo, sote tungeliuwawa," alisema mmoja wa wakaazi wa Beni.

Mauwaji haya yanaendelea wakati jeshi la serikali linaendesha operesheni  dhidi ya ADF, lakini wadadisi wa masuala ya usalama wanasema kuna uzembe katika uongozi wa jeshi hasa katika operesheni zinazotajwa na jeshi la Serikali kuwa ndio za mwisho kufanyika katika eneo hili, ili kuwatokomeza waasi wa ADF wanaowauwa watu kila uchao.

Mwanasheria Omar Kavota, mdadisi wa masuala ya usalama na akiwa pia naibu mwenyekiti wa mashirika ya kutetea haki za binaadamu CEPADHO, anahoji kwamba, mikakati ya kuwalindia usalama wakaazi katika viunga vya maeneo ya vita, haikupangwa vizuri kwani inajulikana wazi ya kwamba, ADF wanaposhambuliwa katika maeneo ya misitu, basi na wao wanawashambulia na kuwaua wakaazi katika maeneo ambayo operesheni bado hazijaanzishwa.

Ikumbukwe kuwa, katika ziara yake mjini Beni, na alipotangaza kwamba operesheni kabambe zitaanzishwa katika eneo hilo dhidi ya waasi wa ADF, rais Félix Tshisekedi aliwahi kuwaahidi wakaazi, kwamba waasi hao watatokomezwa kabla ya sherehe za Krismasi pamoja na mwaka mpya. Lakini ahadi hiyo inaonekana kubakia kuwa ndoto tu.

Rwanda yakabidhiwa wapiganaji 291 waliokuwa tishio kwa usalama wa Congo

Kongo - Operation gegen die ugandischen Rebellen der ADF-Nalu
Picha: Reuters/Kenny Katombe

Huku hayo yakiarifiwa, maafisa wa jeshi la Congo wamekabidhi wapiganaji 291 na watoto 11 kwa maafisa wa Rwanda kwenye mpaka kati ya nchi hizo 2 mjini Bukavu. Jeshi limesema  wapiganaji hao walikuwa tishio kubwa kwa usalama wa Congo.

Shughuli hii ilifanyika kwenye mpaka wa Ruzizi ya Kwanza kati ya Bukavu upande wa Kongo na Cyangugu upande wa Rwanda. Jeshi la Kongo limesema wapiganaji hao wameshikwa wakati wa operesheni za kijeshi zinazofanyika katika wilaya ya Kalehe ndani ya mkoa wa kivu kusini, dhidi ya wanamgambo wa kundi liitwalo CNRD walioendesha mapigano katika  eneo hilo tangu kwa miaka kadhaa.

Jeshi hilo kupitia Kapiteni Dieudonné Kasereka,  msemaji wa operesheni ya kijeshi inayoitwa Sokola ya pili hapa kivu kusini, limesisitiza kwamba wapiganaji hao wamevushwa kwa hiari yao.

Hata hivyo, watu wengine wa familia za wapiganaji hao wanaoelezwa kuwa zaidi ya 1700 ambao sio wapiganaji, wanahifadhiwa katika kambi ya Nyamunyunyi katika mtaa wa kabare wanako subiri hatua itakayo chukuliwa na viongozi wa kisiasa, kama anavyoendelea kueleza msemaji huyo wa jeshi.

Wapiganaji hao wanyarwanda walipokelewa na afisa wa jeshi la Rwanda RDF, meja jenerali Alex Kagame, ambaye amesifu uhusiano baina na jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na nchi ya Rwanda kuhusu usalama kati ya nchi hizo mbili:

Vyanzo John Kanyunyu/Mitima Delachance