1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masoud Pezeshkian aidhinishwa kuwa Rais wa Iran

28 Julai 2024

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amemuidhinisha Masoud Pezeshkian kuliongoza taifa la Iran. Pezeshkian, atakuwa Rais wa tisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuapishwa.

https://p.dw.com/p/4ipsj
Iran Masoud Pezeshkian Hafla ya kumuidhinisha
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amemuidhinisha rasmi Masoud Pezeshkian kuwa Rais wa IranPicha: leader.ir

Masoud Pezeshkian siku ya Jumapili 28.07.2024 alipokea cheti chake cha kuteuliwa kuwa Rais na baraka kutoka kwa kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, na hivyo akatangazwa rasmi atakuwa Rais wa tisa wa nchi hiyo. 

Hatua hiyo ni baada kumalizika uchaguzi uliofanyika mapema mwezi Julai.

Iran  Masoud Pezeshkian  Hafla ya kuidhinishwa kuwa Rais
Kushoto: Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei. Kulia. Rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian.Picha: leader.ir

Katika ujumbe uliosomwa na mkurugenzi wa ofisi ya Khamenei, kiongozi huyo amesema amemuidhinisha mwanamageuzi Pezeshkian ambaye amemsifu kuwa ni mtu mwenye hekima, mwaminifu, maarufu na msomi na hizo zikiwa ni miongoni mwa sababu zilimfanya amuunge mkono na kumuidhinisha awe Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais huyo mteule wa Iran Masoud Pezeshkian, ataapishwa mbele ya bunge siku ya Jumanne.

Hafla ya kumuidhinisha Pezeshkian, ilifanyika katika Msikiti wa Khomenei ulio katika mji mkuu wa Iran, Tehran na ilihudhuriwa na maafisa wakuu wa Iran pamoja na wanadiplomasia wa kigeni na ilipeperushwa mubashara kwenye televisheni ya serikali.

Soma Pia: Iran yakosoa vikali ziara ya Netanyahu nchini Marekani 

Kaimu rais Mohammad Mokhber alikabidhi majukumu rasmi kwa mwanamageuzi Masoud Pezeshkian mwenye umri wa miaka 69.

Baadaye Jumapili, Pezeshkian alimteua mwanamageuzi mwenzake Mohammad Reza Aref, mwenye umri wa miaka 72, kama makamu wake wa kwanza wa rais, kulingana na tangazo lililotolewa na Runinga ya serikali.

Iran  Makamu wa Kwanza wa Rais  Mohammadreza Aref
Mohammad Reza Aref,ameteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa IranPicha: Rouzbeh Fouladi/ZUMA Wire/picture alliance

Aref amewahi kuliwakilisha jiji la Tehran bungeni na pia aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa rais na waziri wa mawasiliano wakati wa rais mwanamageuzi Mohammad Khatami, aliyetawala Iran kuanzia 1997 hadi 2005.

Pezeshkian, ambaye ni daktari wa upasuaji wa moyo alikuwa mbunge wa mji wa kaskazini-magharibi wa Tabriz mnamo mwaka 2008, na alikuwa waziri wa afya chini ya utawala wa  Khatami.

Pezeshkian alishinda kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa rais mnamo Julai 5 kwa kumwangusha mhafidhina Saeed Jalili  walipo pambana kuchukua nafasi ya Rais Ebrahim Raisi aliyefariki katika ajali ya helikopta mwezi Mei mwaka huu wa 2024.

Alipata zaidi ya kura milioni 16, au asilimia 54 ya takriban kura milioni 30 zilizopigwa.

Ebrahim Raisi | Umoja wa Mataifa  New York
Rais wa Iran Ebrahim Raisi aliyefariki katika ajali ya helikopta mwezi Mei, 2024.Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Soma Pia: Masoud Pezeshkian: Nini cha kutarajia kutoka kwa rais mpya wa Iran 

Mfumo wa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba Rais sio mkuu wa nchi, na mamlaka ya juu kabisa nchini humo yamo mikononi mwa kiongozi mkuu, wadhifa unaoshikiliwa na Ayatollah Ali Khamenei kwa muda wa miaka 35 hadi kufikia sasa.

Rais mteule Masoud Pezeshkian amemshukuru kiongozi huyo mkuu pamoja na watu wa Iran, na ameahidi kuubeba mzigo mzito wa urais kwa hekima na taadhima.

Vyanzo: AFP/DPA