1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa Gaza wasema mashambulizi ya IDF yameua 100

25 Desemba 2023

Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas imesema shambulio la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Maghazi liliua watu 70. Wakati huo huo, mashambulizi ya Israel Gaza yameendelea Siku ya Krismasi.

https://p.dw.com/p/4aZCi
Gaza | Mzozo wa Mashariki ya Kati | Uharibifu Gaza
Isael imesema inachunguza ripoti kwamba shambulizi lake limeua makumi ya raia katika kambi ya wakimbizi.Picha: Menahem Kahana/AFP

Kwenye mazishi huko Gaza siku ya Jumatatu, msururu wa Wapalestina walishika sanda nyeupe zilizokuwa na miili ya watu wasiopungua 70 ambao maafisa wa afya wa Palestina walisema waliuawa katika shambulio la anga la Israel lililolenga kambi ya wakimbizi ya Maghazi katikati mwa ukanda huo uliozingirwa.

Ilikuja baada ya moja ya usiku mbaya zaidi kwa ukanda huo katika vita vya wiki 11 kati ya Israel na Hamas. Mtu mmoja alimkumbatia mtoto aliyekufa na wengine walikuwa wamejawa na hisia.

"Mashambulizi hayo yaliotokea saa nane za usiku. Kuta na mapazia vilituangukia," mtu mmoja alisema. "Nilifika kwa mtoto wangu wa miaka minne lakini nilichopata ni mawe."

Gaza | Uharibifu wa mashambulizi ya Israel
Mashambulizi ya Israel yameharibu sehemu kubwa ya Ukanda wa GazaPicha: Adel Hana/AP

Mashambulizi hayo yalioanza muda mfupi kabla ya saa sita usiku yaliendelea hadi Jumatatu. Vyombo vya habari vya Palestina vilisema Israel ilizidisha mashambulizi ya anga na ardhini katikati mwa Gaza huku wakaazi wa eneo hilo wakisema kuwa wameshuhudia moja ya usiku mbaya zaidi tangu vita kuanza.

Soma pia: Papa Francis ataka vita vya Gaza vikomeshwe

Msemaji wa wizara ya afya Ashraf Al-Qidra alisema wengi wa waliouawa Maghazi walikuwa wanawake na watoto. Wengine wanane waliuawa wakati ndege na vifaru vya Israel vikifanya mashambulizi kadhaa ya anga kwenye nyumba na barabara katika maeneo ya karibu ya al-Bureij na al-Nusseirat, maafisa wa afya walisema.

Madaktari waliongeza kuwa shambulizi la anga la Israel katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza liliua watu 23 na kupelekea vifo vya Wapalestina kuwa zaidi ya 100 katika usiku mmoja.

Papa Francis alia na mauji ya raia wasio na hatia

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, alisema katika ujumbe wake wa Krismasi siku ya Jumatatu kwamba watoto wanaokufa katika vita, ikiwa ni pamoja na huko Gaza, ndiyo "Yesu wadogo wa leo" na kwamba mashambulizi ya Israel yanavuna "mavuno ya kutisha" ya raia wasio na hatia.

Wakazi kadhaa walitoa maombi kwenye mitandao ya kijamii kwa watu wawapatie hifadhi baada ya kugeuka wasio na makazi kufuatia kuondoka katika nyumba zao huko Bureij.

Vatikan Petersdom 2023 | Papa Francis Urbi et Orbi
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, ameyataja mashambulizi ya Israel Gaza kuwa mavuno ya kutisha dhidi ya raia wasio na hatia.Picha: Tiziana Fabi/AFP/Getty Images

"Nina watu 60 ndani ya nyumba, watu waliofika nyumbani kwangu wakiamini kuwa eneo la kati la Gaza lilikuwa salama. Sasa tunatafuta mahali pa kufika,” alisema Odeh, mkazi wa kambi za wakimbizi.

Jeshi la Israel limesema linapitia ripoti ya tukio la Maghazi na limeahidi kupunguza madhara kwa raia. Hamas inakanusha madai ya Israel kwamba inaendesha shughuli zake katika maeneo yenye watu wengi au inatumia raia kama ngao za binadamu.

Soma pia: Vita vya Gaza na Ukraine vyatia kiwingu sikukuu ya Krismasi

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilichapisha picha za wakaazi waliojeruhiwa wakisafirishwa hadi hospitalini, na kusema ndege za kivita za Israel zilikuwa zikishambulia kwa mabomu barabara kuu, na kuzuia njia za magari ya kusafirisha wagonjwa na magari ya dharura.

Katika hotuba yake ya Siku ya Krismasi "Urbi et Orbi" (kwa mji na ulimwengu), Francis pia alitaja shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israeli na wanamgambo wa Hamas kuwa "chukizo" na akaomba tena kuachiliwa kwa karibu mateka 100 ambao bado wanashikiliwa Gaza.

Makasisi walifuta sherehe huko Bethlehem, mji wa Kipalestina unaoakaliwa kimabavu na Israel katika Ukingo wa Magharibi, ambapo mafundosho ya Kikristo yanasema Yesu alizaliwa katika zizi miaka 2,000 iliyopita.

Ukanda wa Gaza | Kanisa Katoliki la Gaza.
Wakristo katika Ukanda wa Gaza hawakusherehekea Kriskam mwaka huu kutoka na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas.Picha: Ahmad Hasaballah/IMAGESLIVE via ZUMA Press/picture alliance

Wakristo wa Palestina walifanya mkesha wa mishumaa wa Krismasi mjini Bethlehem kwa nyimbo na sala za amani kwa ajili Gaza, badala ya sherehe za kawaida.

Hakukuwa na mti mkubwa, kitovu cha kawaida cha maadhimisho ya Krismasi ya Bethlehemu. Sanamu za Kuzaliwa kwa Yesu katika makanisa ziliwekwa katikati ya vifusi na waya zenye miinuko kama ishara ya mshikamano na watu wa Gaza.

Mazingira ya maafa

Hamas na kundi dogo mshirika la wanamgambo wa Islamic Jihad, wote walioapa kuiangamiza Israel, wanaaminika kuwashikilia mateka zaidi ya 100 kutoka kati ya 240 waliowakamata wakati wa shambulio la Oktoba 7 katika miji ya Israel, walipoua watu 1,200.

Tangu wakati huo, Israel imeuzingira Ukanda mwembamba wa Gaza na kuharibu sehemu yake kubwa, huku zaidi ya watu 20,400 wakithibitishwa kuuawa, kulingana na mamlaka za ukanda huo unaoongozwa na Hamas, na maelfu ya wengine wanaaminika kuuawa chini ya vifusi.

Soma pia: Guterres atoa heshima zake kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliouawa Gaza

Idadi kubwa ya watu milioni 2.3 wa Gaza wamefurushwa kutoka makwao, na Umoja wa Mataifa unasema hali ni mbaya.

Tangu kuvunjika kwa mapatano ya wiki moja mwanzoni mwa mwezi, mapigano yamezidi kupamba moto, huku vita vikienea kutoka kaskazini hadi urefu kamili wa ukanda huo wenye watu wengi.

Jeshi la Israel lilisema Jumatatu kuwa wanajeshi wake wawili walifariki katika siku iliyopita, na kufikisha idadi ya waliouawa kuwa 158 tangu operesheni za ardhini zilipoanza Oktoba 20.

Siku moja kabla Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikiri "gharama kubwa"  ya vita hivyo lakini akasema "hakuna chaguo" ila kuendelea kupigana ndani zaidi ya Gaza hadi "ushindi kamili" dhidi ya Hamas upatikane.

Hamas yadai kuisababishia hasara kubwa Israel

Mkuu wa kundi la Hamas katika Ukanda Gaza, Yehya al-Sinwar, anasema wapiganaji wake wamesababisha hasara kubwa ya maisha na vifaa kwa wanajeshi wa Israel katika mzozo huo.

Katika barua kwa mwenyekiti wa kamati ya siasa ya chama cha Hamas, Ismail Haniya, na wajumbe wengine wa kamati hiyo, al-Sinwar alizungumzia vita vikali, vya kikatili na visivyo na kifani dhidi ya vikosi vya Israel vinavyopiganwa na brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la vuguvugu hilo.

Soma pia:Vikosi vya Israel vyaelekeza mashambulizi katikati mwa Gaza 

Alidai kuwa, Vikosi vya Qassam viliwashambulia wanajeshi wasiopungua 5,000 wa Israel na kuua theluthi moja, kujeruhi vibaya theluthi nyingine na kulemaza kabisa theluthi nyingine.

Takwimu hizi zinakinzana na takwimu za jeshi la Israel, zinazoonysha zaidi ya wanajeshi 150 wa Israel wameuawa katika Ukanda wa Gaza katika mzozo wa sasa.

Makubaliano ya kusitisha vita Israel-Hamas kurefushwa?

Al-Sinwar pia aliandika kwamba magari 750 ya kijeshi ya Israeli yalikuwa yameharibiwa kabisa au kwa sehemu. Jeshi la Israel halitoi taarifa zozote kuhusu hili. Mkuu huyo wa Hamas Gaza alihitimisha kuwa vikosi vya Qassam vilikuwa "vimewapiga vibaya" wanajeshi wa Israel na kwamba vilikuwa njiani kuwaangamiza kabisaa.

Tawi hilo la kijeshi la Hamas halitokubali masharti ya Israeli ya kukomesha uhasama wa kivita, aliongeza. Marekani, Israel, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa yanairodhodhesha Hamas kama kundi la kigaidi.

Chanzo: dpa, afpe, ape