1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haniyeh awasili Misri kuzungumzia usitishaji mapigano Gaza

20 Desemba 2023

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh, amewasili mjini Cairo kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza baada ya Israel kusema iko tayari kwa awamu nyingine ya kusimamisha vita.

https://p.dw.com/p/4aP1q
Ismail Haniyeh mjini Doha / Kiongozi wa Hamas
Kiongozi wa Hamas Ismail HaniyehPicha: Hamas Chief Office/ZUMA Pree Wire/picture alliance

Taarifa ya safari ya kiongozi huyo imetolewa na kundi la Hamas ambalo limesema akiwa nchini Misri, Haniyeh atafanya mazungumzo na mkuu wa ujasusi wa taifa hilo na viongozi wengine kuhusu usitishaji mapigano huko Gaza na kuachiwa wafungwa zaidi wa Kipalestina.

Miito ya kimataifa inaongezeka kutaka yapatikane makubaliano mapya ya kusitisha vita yatakayosaidia kuingizwa msaada ziada wa kiutu kwenye Ukanda wa Gaza na mabadilishano ya wafungwa pamoja na mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Soma pia: Hamas: Hatutoshiriki upatanishi hadi hujuma zisitishwe Gaza

Nchini Israel, viongozi wa taifa hilo wameashiria kuwa tayari kusitisha hujuma dhidi ya Ukanda wa Gaza katika wakati wanaandamwa na shinikizo la umma unaotaka zitafutwe njia za kuachiwa huru kwa mateka wa nchi hiyo.