1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masaibu ya watoto nchini Iraq

Mwakideu, Alex10 Machi 2008

Uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq umewaathiri zaidi watoto kuliko wananchi wengine wote

https://p.dw.com/p/DLvM
Mtoto mwenye miaka minne alia machozi kwasababu wenzio wanamtishia kwa bastola za uongo.Picha: AP

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba nusu milioni ya watoto nchini humo wamefariki katika kipindi cha zaidi ya miaka 12 iliyoshuhudia Iraq ikiwekewa vikwazo vya kiuchumi na pia jeshi la Marekani likiingia vitani nchini humo mnamo machi 2003. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba sababu kuu iliyosababisha vifo vya watoto nchini humo ni utapia mlo na magonjwa.


Kulingana na ripoti iliyowekwa wazi na shirika la Oxfarm International julai mwaka jana utapia mlo nchini Iraq umeongezeka kwa asilimia 9.

Utafiti mwengine uliofanywa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Save the Children unaonyesha Iraq ikiendelea kuongoza kwa vifo vya watoto wasiozidi miaka tano. Hali hiyo imeongezeka kwa asilimia 150 tangu wakati wa vita vya Ghuba vya kwanza. Utafiti huo unaendelea kusema mmoja kati ya watoto wanane hufariki kabla ya kutimiza miaka tano. Watoto 122, 000 walifariki mwaka wa 2005 pekee. Iraq ina idadi ya watu milioni 25.


Matokeo ya uchunguzi uliofanywa na watafiti kutoka kitengo cha hazina ya watoto katika Umoja wa Mataifa mwezi huu yanaonyesha kwamba watoto milioni 2 wanakosa lishe bora. Kwa upande mwengine shirika la chakula ulimwenguni liliripoti katika uchunguzi wake mwaka wa 2006 kwamba watoto nchini Iraq wanakabiliwa na tisho la kuachishwa shule, kukosa sindano za kinga dhidi ya magonjwa pamoja na kukumbwa na magonjwa yanayosababisha kuendesha.

Mmoja kati ya watoto walioathirika nchini Iraq ni Firas Muhsin anaeishi na mamake katika jijii kuu la mkoa wa Diyala linaloitwa Baquba ambalo liko kilomita 40 kaskazini magharibi mwa Baghdad.


Babake Firas aliuwawa na wanamgambo kwa kupigwa risasi alipokuwa dukani mwake.


Firas huenda katika shule iliyoko karibu na nyumbani mwao na yeye hukaa huko kwa saa nne huku mamake akimtazama kila wakati.

Mototo huyo huruhusiwa kuenda mita kumi tuu mbali na nyumbani mwao kwasababu mamake ana wasi wasi kwamba huenda akatekwa nyara kwani utekaji nyara wa watoto umeongezeka sana nchini Iraq. Inaaminika kwamba wanaotekwa nyara huuzwa kama wafanyikazi na wengine utumiwa kwa ngono.


Hata hivyo maafisa wa serikali na wafanyikazi wa misaada wameanza kulitilia maanani jambo hili.


Kiongozi wa shirika la Iraq Family Association lililozinduliwa mwaka wa 2004 kwa minajili ya kusajili visa vya kupotea na kutekwa nyara kwa raia wa Iraq, alinukuliwa na wanahabari akisema takriban watoto wawili huuzwa na wazazi wao kila wiki na isitoshe jumla ya watoto wengine wanne hupotea kila wiki.


Khalid amesema kumekuwa na ongezeko la asilimia 20 ya watoto wanaopotea katika kipindi cha mwaka mmoja.


Hiyo huenda ikawa sababu ambayo imempelekea Firas mwenye miaka saba kukaa nje ya mlango wao siku kucha akiangalia wapita njia kwani hapo ndio mahali pa pekee anapoweza kukaa kabla ya kuitwa ndani na mamake mwendo wa jioni ili afanye kazi za shule na baadaye atizame vipindi vya watoto kwa runinga iwapo kikaangavuke chao kitakuwa na nguvu za umeme.


Watoto wengi walioko na umri sawa na Firas hawaendi shuleni kabisa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba asilimia 17 ya watoto nchini Iraq wametolewa rasmi katika shule za msingi na wengine 220,000 wanakosa shule kwasababu familia zao zimeachwa bila makao. Hiyo inafikisha idadi ya watoto wanaokosa masomo ya shule ya msingi kufikia 760,000 kulingana na takwimu za mwaka wa 2006.


Idadi hii haijumlishi mamia na maelfu ya watoto ambao familia zimetotokea nchi zingine na kuwalazimisha wakose. Takwimu za shirika la wakimbizi la UNHCR zinaonyesha kwamba takriban wairaqi milioni 2.25 wametoroka nchini mwao.


Firas amekosa mahitaji yote ya kimsingi yanayomfaa kila mtoto kwani hana mahali pa kucheza, wala watoto wa kucheza naye na hata mtu yeyote wa kumuangalia kama mfano bora katika jamii.


Kulingana na hazina ya watoto ya Umoja wa Mataifa asilimia 40 pekee ya watoto nchini Iraqi ndio wanaoweza kupata maji safi na salama ya kunywa na takriban watoto 75,000 wanaishi katika makaazi ya mda.