1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marsabit yaelezea wasiwasi kwa operesheni ya serikali Kenya

15 Februari 2023

Serikali ya jimbo la Marsabit, kenya imekerwa na hatua ya wizara ya usalama kutoiorodhesha miongoni mwa majimbo ambayo operesheni ya kukabiliana na majangili na wezi wa mifugo inaendeshwa katika eneo la bonde la ufa

https://p.dw.com/p/4NV3v
Kenia Vor den Wahlen 2022
Picha: Michael Kwena/DW

Siku mbili tu baada ya rais William Ruto kutangaza operesheni ya kijeshi katika eneo la bonde la ufa katika juhudi za kukusanya silaha haramu na kupambana na wezi wa mifugo katika eneo hilo,serikali ya kaunti ya Marsabit imeezelea masikitiko yake baada ya kuachwa nje ya orodha ya majimbo ambayo operesheni ya kijeshi inaendeshwa.

Kwa mujibu wa naibu gavana wa Marsabit Solomon Riwe,jimbo la Marsabit linalokaliwa na jamii za wafugaji kadhalika limekuwa likishambuliwa na majangili waliojihami kwa bunduki na kwamba jimbo hili lilipaswa kuangaziwa kwenye operesheni iliyotangawa na rais ili amani na usalama wa kudumu upatikane.

Kenya: Wakaazi Marsabit wakimbia makwao kwa kuhofia maisha

Akizungumza muda mfupi baada ya kutoa maoni yake kwenye jopo linaloangazia mageuzi kwenye idara ya polisi nchini,Riwe amedai kuwa operesheni hiyo kutoendeshwa Marsabit ni hatari kwa Maisha ya wakaazi wanaopakana na kaunti jirani ya Samburu kunakoendeshwa operesheni hiyo.

Wakaazi wanahofu huenda majangili wakakimbilia Marsabit

Karte - Kenia mit Counties - DE
Ramani inayoonesha ilipo eneo la Marsabit

Baadhi ya wakaazi pia wanahofia kuwa,huenda majangili kutoka kaunti jirani kunakoendeshwa operesheni hiyo wakavuka na kuingia Marsabit hali inayoweza kuhatarisha Maisha ya raia.

Hata hivyo,kaimu kamishna wa Marsabit David Saruni ameshikilia kuwa,wizara ya usalama imeweka mikakati ya kukabiliana na majangili hao endapo watajaribu kuvuka na kuingia Marsabit wakikwepa mkono wa sheria.

Marsabit yasitisha uhasama

Siku ya jumatatu,rais William Ruto alitangaza  operesheni hiyo katika maeneo yaliyoripoti mashambulizi ya majangili wa mifugo japo alitoa muda wa siku tatu kwa raia kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria kabla ya operesheni hiyo kuanza rasmi.

Majimbo yaliyoorodheshwa kwenye operesheni hiyo ni Elgeyo Marakwet,Turkana,Pokot magharibi,Baringo,Laikipia na kaunti Jirani ya Samburu.

Michael Kwena DW Marsabit