1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Wakaazi Marsabit wakimbia makwao kwa kuhofia maisha

Michael Kwena8 Julai 2021

Zaidi ya familia 450 zimeyakimbia makaazi yao katika eneo la Saku jimboni Marsabit nchini Kenya kutokana na hofu ya mapigano ya kikabila, kufuatia mauaji ya watu watatu waliopigwa risasi na majangili siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/3wDAa
Äthiopien Lebensmittellieferung in Moyale
Picha: DW/M. Kwena

Boma kadhaa katika lokesheni ya jirime katika eneo bunge la saku jimboni Marsabit, zimekimbiwa na wenyeji kufuatia hofu ambayo inaendelea kushudiwa kutokana na uhasama wa kikabila.

Uhasama huo umeripotiwa kuzidishwa na kisa cha mauaji ya siku ya jumatatu ambapo watu watatu akiwemo mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa walipigwa risasi na kuawawa na watu wasiojulikana.

Naibu chifu wa jirime Adan Waqo ameeleza kwamba,huenda idadi yafamilia zilizoyakimbia makaazi yao  kutokana na hali hiyo ikawa ya juu Zaidi kuliko taarifa walizonazo kwa sasa.

Soma pia:Viongozi wa Marsabit walaumiwa kufadhili machafuko 

Idara ya polisi ya Marsabit imewataka wananchi kuwa na subra wakati uchunguzi ukiendelea na kuwarai wenyeji kutohusika kwa kulipiza kisasi.

"Nawasihi wakaaji wa hapa wasijichukulie hatua mikononi mwao.Naomba wasilipize kisasi.Sisi kama idara ya polisi tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba,hawa wahalifu wanakabiliwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Johnstone Wachira, mkuu wa polisi wa Marsabit Kati.

Karte Kenia mit Marsabit
Ramani inyoonesha eneo la Marsabit kaskazini mwa Kenya

Wizara ya usalama yanyooshewa kidole cha lawama

Mwakilishi wa wadi ya Marsabit ya Kati Hassan Jarso kwa upande wake, ameitaka wizara ya usalama wa ndani kuwajibika ili kupata suluhisho katika vita vya kikabila kama sehemu zingine za taifa. ‘'Kama walifanikiwa kumaliza vita vya Kapedo na mlima elgon, mbona hivi vita vidogo vya Marsabit inawashinda?''

Gavana wa hapa Muhamud Ali ameelezea kusikitishwa na  mauaji hayo ambayo yamekuwa yakiendelea kuripotiwa katika jimbo hilo, na kubainisha kuwa serikali ya kaunti imetumia fedha nyingi katika juhudi za  la kutafuta maelewano baina ya jamii hasimu.

Soma pia: Mapigano ya kikabila yauwa zaidi ya 300 Kenya 2015

"Tumetumia fedha nyingi kama serikali ya jimbo  kando na fedha za wahisani kama vile UNDP,umoja wa ulaya katika muda wa miaka minne sasa. Washirika wetu wamechoka ni kwa nini licha ya haya yote,bado hutujakaribia kupata suluhu kwenye masuala ya kiusalama,” amesema gavana Ali.

Idara ya polisi imewataka wanachi kutoa taarifa kuhusu  wahalifu huku ikiahidi kuwapa ulinzi watakaotoa ripoti hizo. Katika kipindi cha miezi miwili sasa, zaidi ya watu kumi na tano wameuawa akiwemo afisa wa polisi aliyepigwa risasi mapema mwezi Julai eneo la Jaldesa.