1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaikamata ndege ya rais wa Venezuela Nicolas Maduro

Josephat Charo
3 Septemba 2024

Marekani imeikamata ndege ya rais wa Venezuela Nicolas Maduro ikisema ndege hiyo ilinunuliwa kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/4kCYf
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Fausto Torrealba/REUTERS

Marekani imeikamata ndege ya rais wa Venezuele Nicolas Maduro katika Jamhuri ya Dominican na kuirejsha katika jimbo la kusini la Florida. Maduro ameikosoa hatua hiyo akiita kuwa ni uharamia lakini Marekani imesema ilihitajika kutokana na kukiukwa kwa vikwazo.

Maafisa wa Marekani wameichukua ndege hiyo chapa Dassault Falcon 900EX, ndege ya kibinafasi iliyokuwa ikitumiwa na Maduro na wanachama wa serikali yake, huku wizara ya sheria ya Marekani ikisema ndege hiyo ilinunuliwa kinyume cha sheria.

Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland amesema katika taarifa kwamba wizara ya sheria ya Marekani imeikamata ndege hiyo wanaoituhumu kwa kununuliwa kwa njia isiyo halali kwa dola milioni 13 kupitia kampuni ya nje ya Venezuela na kutolewa nje ya Marekani kimagendo kwa ajili ya matumizi ya rais Maduro na washirika wake.

Wizara ya mambo ya nje ya Venezuela imetoa taarifa kulaani hatua hiyo ya Marekani kuikamata ndege hiyo.

Wavuti unaofuatilia safari za ndege Flightradar24 unaonesha ndege hiyo ilisafiri kutokea Santo Domingo had Fort Lauderdale jana Jumatatu asubuhi. Jamhuri ya Dominican imesema haikushiriki katika uchunguzi wa Marekani kuhusiana na ndege hiyo.