1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 2 wauwawa kwenye mapambano Ukraine

Josephat Charo
23 Juni 2023

Ukraine imeyatungua makombora 13 yaliyovurumishwa na Urusi usiku wa kuamkia leo (23.06.2023) yakilenga uwanja wa ndege magharibi ya nchi. Ukraine pia imefanikiwa kuzuia uvamizi wa Urusi kuelekea Kupiansk na Lyman.

https://p.dw.com/p/4Syo3
Kämpfe und Zerstörung in Bachmut, Ukraine
Picha: LIBKOS /AP/picture alliance

Jeshi la anga la Ukraine limethibitisha kuyatungua makombora 13 ya Urusi yaliyokuwa yameelekezwa kupiga uwanja wa ndege katika eneo la Khmelnytskyi. Urusi ilianzisha wimbi la mashambulizi ya mfululizo kutumia makombora na droni za kufanyia mashambulizi wakati wa msimu wa baridi, hatua iliyoilazimu serikali ya mjini Kyiv kuomba msaada kwa washirika wake nchi za Magahribi ziimarishe mfumo wake wa ulinzi wa anga dhidi ya makombora.

Mashambulizi ya Urusi yamefanywa mida ya saa sita usiku kutokea bahari ya Caspian. Meya wa eneo la Khmelnytskyi, Oleksandr Symchyshyn ameripoti milipuko katika mji huo uliokuwa na idadi ya wakazi kiasi 275,000 kabla vita kuzuka na kupongeza uimara wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine. Ukraine pia imesema imetungua droni moja ya Urusi usiku wa kuamkia leo iliyokuwa ikikusanya taarifa.

Soma zaidi: Shambulizi la Ukraine laharibu daraja la Crimea: Urusi

Watu wapatao wawili wameuliwa katika shambulizi la Urusi katika mji wa Kherson kusini mwa Ukraine. Gavana wa eneo hilo Oleksandr Prokudin amesema katika taarifa ya awali aliyoituma kwenye mtandao wa Telegram kwamba kampuni ya usafiri imelengwa katika shambulizi hilo, ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 55 ameuwawa papo hapo na watu wengine watano wamepelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa. Baadaye gavana huyo ameripoti mwanamume mwingine wa umri wa miaka 43 amekufa hospitalini kutokana na majeraha.

Ukraine Krieg | Videoansprache des Präsidenten Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Presidential Office of Ukraine

Mashambulizi ya Urusi yazimwa

Wakati haya yakiarifiwa vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kuzuia uvamizi wa Urusi katika miji miwili ya Kupiansk na Lyman mashariki mwa nchi na sasa wanasonga mbele upande wa kusini. Naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar ameiambia televisheni ya Ukraine kwamba wamekuwa na mapambano makali upande wa miji ya Kupiansk na Lyman. Waziri Maliar aidha amesema Urusi inapania kuyadhibiti maeneo yote ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine. Ameongeza kuwa operesheni ya kijeshi ya Ukraine kusini mwa nchi inaendelea vizuri kama ilivyopangwa na vikosi vyake vinasonga mbele, ingawa maeneo kulikotegwa mabomu ya ardhini yanakwamisha kasi yao.

Soma zaidi: Zelensky asema operesheni ya kujibu mapigo inajikokota

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameituhumu tena Urusi kwa kupanga shambulizi la kigaidi katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya kusini mwa nchi. Akizungumza jana Alhamisi katika video iliyosambazwa kwenye mitando ya kijamii, Zelensky amesema amepokea taarifa kutoka kwa idara ya ujasusi ya Ukraine, SBU. Kinu hicho cha nyuklia kilidhibitiwa na Urusi baada ya uvamizi wake miezi 16 iliyopita. Mapigano yanahofiwa kutokea katika maeneo yanayopakana na kinu hicho kama sehemu ya operesheni maalumu ya Ukraine dhidi ya vikosi vya Urusi iliyoanza mwanzoni ma mwezi huu wa Juni.

(afp/reuters)