1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky asema operesheni ya ´kujibu mapigo´ inajikokota

22 Juni 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema operesheni ya jeshi la nchi yake ya kujaribu kuyakomboa maeneo yaliyokamatwa na Urusi inakwenda mwendo wa polepole kuliko ilivyotarajiwa.

https://p.dw.com/p/4SucQ
Ukraine-Krieg - Bachmut
Mapambano nchini Ukraine Picha: Iryna Rybakova/AP/dpa/picture alliance

Matamshi hayo ameyatoa wakati viongozi wa mataifa ya magharibi wanaoshiriki mkutano wa kusaidia kuijenga upya Ukraine wameapa kuwa Urusi italipa kwa kitendo chake cha kuivamia nchi hiyo. 

Rais Zelensky amekaririwa na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, akisema jeshi la nchi yake linapiga hatua za mwendo wa kobe katika operesheni kabambe iliyotangazwa wiki chache zilizopita za kuyarejesha chini ya himaya ya Ukraine maeneo yote yaliyokamtwa na Urusi.

Amesema kasi ya kusonga mbele vikosi vyake kwenye uwanja wa vita ni ndogo "kuliko ambavyo wengi wangetamani". Amesisitiza lakini licha ya ukweli huo serikali mjini Kyiv haitokubali shinikizo la kuongeza kasi.

Amewatahadharisha wale wanaodhani mapambano yanayoendelea kuwa ni sawa na filamu ya kubuni wanafanya makosa na ametaka watambue kilicho rehani ni maisha ya watu walio kwenye uwanja wa mapambano.

Licha ya changamoto mafanikio madogo yanapatikana 

Ukraine Donetsk
Wanajeshi wa Ukraine wakijifunza mbinu za vita huko Donetsk Picha: Wojciech Grzedzinski/AA/picture alliance

Pamoja na hali ya mapambano ya kujikokota Zelensky amesema lakini bado vikosi vya Ukraine vimepata mafanikio fulani huko upande wa kaskazini mashariki na kusini ambako inaarifiwa jeshi la Urusi limezidisha hujuma zake.

"Kwenye uwanja wa vita mapambano ni makali. Huko kusini tunamuangamiza kabisa adui. Katika mkoa wa Donetsk , tunamwangamiza adui. Na hata upande wa Kupiansk, chochote ambacho magaidi wa Urusi wanapanga, bado tutafanikiwa kumwangamiza adui" amesema rais Zelensky.

Tangu kuanza kwa operesheni hiyo ya kujibu mapigo  Ukraine imedai kuwa imekomboa vijiji vinane ikiwa ni mafanikio yake ya kwanza ya kujivunia ndani ya  kipindi cha miezi saba iliyopita.

Mataifa ya magharibi yalisubiri kwa shauku kuanza kwa operesheni hiyo na mengi yameelezea matumaini kuwa itapata mafanikio.

Hata hivyo Urusi kwa upande wake imemkejeli rais Zelensky. Hasimu wake mkuu, rais Vladimir Putin amekaririwa akisema serikali mjini Kyiv ilifahamu tangu mwanzo kuwa haina nafasi ya kupata mafanikio ya maana kwenye operesheni yake.

Mataifa ya magharibi yasema Moscow italipa gharama za kuijenga upya Ukraine

Mkutano wa kuijenga upya Ukraine ukiendelea mjini London
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akimkaribisha rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine kuhutubia mkutano wa kuchangisha fedha za kuijenga upya Ukraine unaofanyika mjini London.Picha: Henry Nicholls/dpa/picture alliance

Maneno hayo ya Putin hayajawazuia washirika wa Ukraine kutoa  hadhari kwa serikali mjini Moscow kwamba italipa kwa uvamizi wake nchini Ukraine.

Matamshi hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa nchi za magharibi walioko mjini London kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa kuchangisha fedha na kupigia upatu uwekezaji ili kusaidia kuijenga upya Ukraine.

Miongoni mwao ni Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken ambao walikula yamini hapo jana kwamba watahakikisha Urusi inalipa sehemu ya gharama za kuijenga tena Ukraine.

Kwa mfano waziri mkuu Sunak ameahidi kuendelea kushinikiza vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Moscow na fedha zitakazopatikana kupitia mali zinazokamatwa zitatumika kufidia gharama za kusaidia Ukraine kusimama tena.

Mkutano wa mjini London unaofikia kilele hii leo, umeshuhudia Ukraine ikipokea hadi ya michango ya mabilioni ya dola kutoka kwa washirika wake tangu Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani n mwenyeji Uingereza.