1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MADRID.Safari ya kurejeshwa nyumbani wahamiaji yasimaishwa

14 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDCM

Senegal imesimamisha zoezi la kuwarudisha nyumbani wahamiaji kadhaa muda mfupi tu kabla ya ndege mbili zilizowabeba kuondoka kutoka visiwa vya Canary nchini Uhispania.

Ndege hizo zilitarajiwa kuondoka leo asubuhi kutoka Fuerteventura Uhispania kuelekea Dakar nchini Senegal.

Sababu ya kusimamisha safari hiyo Senegal imeeleza kuwa ni matatizo ya kiufundi huku Uhispania ikieleza kuwa ni kuchelewa kwa kawaida tu.

Senegal siku ya jumanne ilikubali kuwa itashirikiana na Uhispania kufanikisha zoezi hilo iwapo tu haki za kibinadamu za wahamiaji wanaokabiliwa na hatua ya kurudishwa zitazingatiwa.

Mwaka huu takriban wahamiaji alfu 24 waliwasili katika visiwa vya Canary wakitumia mitumbwi.

Mamia ya wahamiaji wamefariki katika safari za aina hiyo zenye hatari kubwa kutoka Afrika ya magharibi.

Jitihada zao za kutafuta maisha bora na kuukimbia umasikini zimezusha mjadala katika nchi za Uhispania na Senegal huku umoja wa nchi za ulaya ukitolewa mwito wa kusaidia.