1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUfaransa

Macron: Vikosi vya ziada vitasambazwa kudhibiti maandamano

30 Juni 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema vikosi vya ziada vya usalama vitasambazwa kote nchini humo ili kudhibiti maandamano ya vurugu kufuatia siku tatu mfululizo za ghasia.

https://p.dw.com/p/4THcR
Frankreich | Internationaler Gipfel für einen neuen globalen Finanzpakt in Paris
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa imesema kwamba imetiwa wasiwasi na mauaji ya kijana huyo ambayo yamefufua upya malalamiko ya muda mrefu kuhusu tabia ya polisi wa Ufaransa kulenga watu weusi na waarabu pamoja na jamii zinazoishi katika vitongoji vya watu wenye kipato cha chini. 

Akihutubia mkutano wa timu maalum ya mawaziri wenye kushughulikia migogoro, Rais Macron ameongeza kuwa "mbinu za ziada” zitatumika na wizara ya mambo ya ndani kukabiliana na ghasia hizo na kulaani kile alichokiita "watu kutumia mauaji ya kijana kufanya vurugu zisizokubalika.”

Soma pia: Watu 667 wakamatwa kote Ufaransa kufuatia ghasia za umma

Macron ametoa mwito kwa wazazi kuwazuia vijana wao kutotoka nje ili kutuliza ghasia zinazoenea kwa kasi nchini humo, na kuongeza kuwa mitandao ya kijamii inaongeza petroli kwenye moto.

Mitandao ya kijamii inaelezewa kuchochea ghasia

Frankreich, Nanterre I Unruhen nach Polizeigewalt
Maandamano ya vurugu yametokea katika kitongoji cha Nanterre, nje kidogo ya mji wa Paris.Picha: Aurelien Morissard/Xinhua/IMAGO

Baada ya mkutano wa pili na mawaziri, kiongozi huyo ameeleza kuwa mitandao ya kijamii imechukua jukumu kubwa la kuenea kwa ghasia.

Ameitaka mitandao kama vile Snapchat na Tiktok kuondoa maudhui yanayochochea vurugu na kuongeza kwamba aghalabu ghasia zinapangwa mitandaoni.

"Asante sana. Baada ya mkutano huu wa dharura, kwanza ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa maafisa wetu wa polisi, askari wa zima moto, wakuu wa mikoa na wahudumu wote wa serikali ambao wamefanya kazi ya ziada kujaribu kuzuia ghasia katika kipindi cha siku chache zilizopita."

Awali, Waziri Mkuu Elisabeth Borne alisema kuwa serikali inatafakari kuchukua "hatua zozote” ili kurejesha utulivu ikiwa ni pamoja na kutangaza hali ya hatari.

Soma pia: Vurugu zaendelea Ufaransa kulaani kifo cha kijana Nahel

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama serikali ina uwezekano wa kutangaza hali ya hatari kama ambavyo baadhi ya vyama vya upinzani vya mrengo wa kulia vinavyoshinikiza, Borne amejibu kuwa, hawezi kusema lolote kwa sasa ila wanaangalia njia zote lakini kipaumbele ni kurejesha hali ya utulivu kote nchini humo.

"Kwa kweli, hawa ni watu makatili sana, wengine ni vijana wadogo ambao wanashambulia vituo vyetu vya polisi, ukumbi wa mikutano, miundombinu ya umma na ningependa kusisitiza kwamba watu hawa ni wazi hawawakilishi wenyeji ambao nao wameshtushwa kama tulivyo sisi. Hata viongozi waliochaguliwa pia wanashambuliwa na watu hawa wakorofi."

Waziri Mkuu huyo, aliyekuwa amefanya ziara katika kituo cha polisi kilichoko Evry-Courcouronnes kusini mwa mji mkuu Paris, anahudhuria mkutano wa dharura unaoongozwa na Rais Emmanuel Macron.

Majengo ya umma yameharibiwa katika maandamano ya vurugu

Kutangazwa kwa hali ya hatari kutaipa serikali mamlaka zaidi kama vile kuweka sheria ya watu kutotoka nje usiku, kupiga marufuku maandamano na pia kuwapa polisi uhuru wa kuwazuia washukiwa wanaozua rabsha na kupekua majumba yanayoshukiwa kuwapa hifadhi wahuni.

Msimamo huo mgumu unatokea baada ya vyanzo vya polisi kuripoti visa vya uporaji wa mali, ikiwemo kwenye maduka ya kampuni ya Nike na Zara mjini Paris.

Frankreich,  Roubaix I Unruhen nach Polizeigewalt
Jengo la kampuni ya Tessi group ni moja kati ya majengo na miundombinu iliyoharibiwa katika maandamano ya vurugu.Picha: Pascal Rossignol/REUTERS

Majengo ya umma kote nchini humo hayakusazwa katika maandamano hayo ya vurugu, pamoja na kushambuliwa kwa vituo vya polisi na shule. Mamlaka imesema kuwa magari yapatayo 2,000 yameteketezwa moto tangu ghasia hizo zilipozuka.

Polisi ya Ufaransa imewakamata watu 875 wakati wa ghasia za usiku kucha, karibu nusu ya idadi hiyo wakikamatwa mji mkuu wa Paris.

Jumla ya majengo 492 yameharibiwa, na matukio 3,880 ya moto kuripotiwa, kulingana na takwimu zilizotolewa na Rais Emmanuel Macron mwanzoni mwa mkutano wa dharura uliotishwa hii leo.

Ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa imesema kwamba imetiwa wasiwasi na mauaji ya kijana huyo.

Soma pia:Serikali ya Ufaransa yakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani nayo 

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai kuwepo kwa ubaguzi wa kimfumo ndani ya taasisi za serikali, madai ambayo Macron ameyakanusha. Mnamo mwaka 2020, serikali yake iliahidi kuchukua msimamo wa ‘kutovumilia kabisa' ubaguzi katika vyombo vya sheria ikiwemo jeshi la polisi.

Msemaji wa Ofisi ya haki za Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani amesema Ufaransa inaweza kutumia tukio la mauaji ya Nahel M kama fursa ya kushughulikia kwa kina suala la ubaguzi wa rangi katika utekelezaji wa sheria.

Vyanzo: ap/afp/dpa/reuters