1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya Covid yapindukia laki 2 kwa siku Ujerumani

28 Januari 2022

Janga la virusi vya corona bado linautikisa ulimwengu huku Ujerumani ikisajili zaidi ya maambukizi laki mbili kwa siku kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga hilo.

https://p.dw.com/p/46DUm
Deutschland Essen Krankenschwester Intensivstation
Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Maambukizi nchini Ujerumani yanazidi kuongezeka baada ya Taasisi inayohusika na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch kuripoti kwamba watu 203, 136 waliambukizwa virusi hivyo nchini Ujerumani katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita. Idadi hiyo imezidi kwa 69,600 ya visa vilivyorikodiwa siku ya Alhamis wiki iliyopita.Idadi hiyo kubwa ya maambukizi imesababisha upungufu wa wafanyakazi katika baadhi ya makampuni nchini Ujerumani ikiwemo kampuni ya Lufthansa.

Huko England nako, nchi hiyo inarudi katika mpango wake wa kwanza uitwao mpango A ambapo kila mmoja anashauriwa kujifunza jinsi ya kuishi na ugonjwa wa Covid ambao huenda usiweze kuangamizwa.

Wasiochanjwa wajilipie wenyewe gharama za hospitali

Sehemu kubwa ya vikwazo vilivyokuwa vimewekwa nchini humo sasa vimeondolewa kuanzia Alhamis na serikali ya England inasema chanjo za tatu za nyongeza, vidonge vya kukabiliana na virusi hivyo na kirusi kipya cha Omicron kutosababisha homa kali, ni mambo ambayo yataipelekea serikali kuweza kukabiliana na mripuko wowote utakaotokea. Shirika la Afya la Uingereza UKHSA linasema chanjo ya tatu inasaidia kwa asilimia 95 kuzuia vifo kutokea kwa watu walio na umri wa miaka 50 au zaidi.

Großbritannien | Coronavirus London Werbeplakat Covid-19 Booster Impfung
Bango la kuhimiza chanjo ya ziada mjini LondonPicha: Justin Ng/Avalon/Photoshot/picture alliance

Nchini Ufaransa, mkuu wa mifumo ya hospitali nchini humo amezua mjadala mkali nchini humo baada ya kusema watu ambao wameamua kutochomwa chanjo ya Covid-19 hawastahili wanastahili kujisimamia wenyewe matibabu ya ugonjwa huo badala ya kulipiwa na bima ya afya.

Chini ya mfumo wa afya kwa wote nchini Ufaransa, wagonjwa wote wa Covid-19 ambao wanaishia katika vyumba vya wagonjwa mahututi, wanalipwa malipo yote na bima ya afya. Malipo hayo ni kama yuro 3000 kwa siku na kwa kawaida mgonjwa huwa katika chumba hicho kwa wiki moja hadi siku kumi.

Haya yanafanyika wakati ambapo shirika la kudhibiti madawa la Ulaya limetoa idhini ya kutumika kwa vidonge vya kukabiliana na virusi vya corona vilivyotengenezwa na kampuni ya Pfizer kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa ambao ni wazee na walio katika hatari ya kupata homa kali wanapopata ugonjwa wa Covid-19.

Wasafiri kuketi karantini kwa siku 21 

Kwa upande wake Umoja wa Falme za Kiarabu umewasilisha chanjo milioni moja katika Ukanda wa Gaza. Chanjo hizo zimewasili kupitia mpaka wa Rafah kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la kitaifa la WAM. Chanjo hizo za Sputnik ndio msaada mkubwa kuwasilishwa Gaza kutoka Falme za Kiarabu tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona.

Huko Hong Kong nako sera ya kisiwa hicho chenye utawala wa ndani ya kuhakikisha kwamba wameuangamiza ugonjwa wa Covid, inashutumiwa mno na wataalam. Sera hiyo inawataka wasafiri wote wanaoingia nchini humo kuketi karantini kwa siku 21 na kuwasilisha vipimo vya PCR kwa taasisi za serikali kuhakikisha kwamba hawajaambukizwa virusi vya corona.

Hongkong | Regal Airport Hotel nach neuer Coronavirus Variante
Wasafiri Hong Kong wanastahili kukaa karantini kwa siku 21Picha: Peter Parks/AFP/Getty Images

Jambo hilo limesababisha hoteli na vituo vya karantini vya serikali kufurika watu na biashara nyingi kufungwa. Raia katika kisiwa hicho wanasema sheria za kukabiliana na maradhi hayo zinazidi kuwa kali kuliko zile zilizowekwa mara ya kwanza mwaka 2020 virusi hivyo vilipogundulika.

Vyanzo/Reuters/APE