1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wazidi kupinga vizuizi vya COVID-19

28 Desemba 2021

Maandamano yamezidi kushuhudiwa katika miji mbalimbali nchini Ujerumani wakipinga vizuizi vipya vya COVID-19 wakati taifa hilo na ulimwengu wakielekea kwenye maadhimisho ya mwaka mpya.

https://p.dw.com/p/44txR
Deutschland Dresden | Coronavirus | Protest gegen Maßnahmen
Picha: Matthias Rietschel/REUTERS

Mataifa mbalimbali yanaendelea kuchukua hatua za kudhibiti kusambaa zaidi kwa maambukizi ingawa hata hivyo katika baadhi ya maeneo hatua hizo zimeendelea kukabiliwa na ukosoaji. Nchini Ujerumani, sasa kunashuhudiwa maandamano ya kila uchwao ya kupinga vizuizi vinavyotangazwa na serikali. 

Nchini Ujerumani, maelfu ya wakazi hapo jana waliandamana katika maeneo mbalimbali kupinga vizuizi vipya vya corona ambavyo ni pamoja na kupunguza idadi ya watu kukusanyika. Mapema mwezi huu, bunge la Ujerumani pia liliidhinisha watumishi wa afya kupata chanjo kwa lazima. Jeshi la polisi limesema watu 15,000 waliandamana katika jimbo la Mecklenburg-Vorpommern na waandamanaji 9,000 katika jimbo la Brandenburg. Katika mji wa Halle, mashariki mwa jimbo la Saxony-Anhalt, takriban watu 1,500 waliandamana na polisi walilazimika kuwatawanya waandamanaji katika miji maarufu ya Dresden na Leipzig.

Soma Zaidi: Ufaransa: Kwa mara ya kwanza zaidi ya watu 100,000 wauguwa COVID-19 

Kumeshuhudiwa maandamano ya kila mara katika wiki za karibuni ya kupinga vizuizi hivyo kote nchini Ujerumani, ambayo mara nyingi hugubikwa na ghasia na waandamanaji kukamatwa huku polisi wakijeruhiwa. Ujerumani hivi sasa inapambana na wimbi la tano la maambukizi ya corona yanayochochewa zaidi na kirusi cha omicron ambacho kimegunduliwa katika majimbo yote 16 ya shirikisho.

InfoMigrants | Deutschland | Flüchtlinge aus Kamerun
Mahakama hiyo ya kikatiba ya Ujerumani inalitaka bunge kuwa na kanuni za kuwalinda watu wenye ulemavu wakati wa janga la coronaPicha: InfoMigrants/Majda Bouazza

Aidha, mahakama ya katiba nchini humo hii leo imelitaka bunge la Ujerumani kuchukua hatua za haraka za kuwalinda watu wenye ulemavu kufuatia madai kwamba janga hilo linaweza kuwanyima haki ya huduma za tiba. Mahakama hiyo imesema leo kwamba bunge lina wajibu wa kuchukua hatua kutokana na hofu ya maisha yao. Hadi sasa bunge lilikuwa halijachukua hatua yoyote ya msingi na mahakama hiyo sasa inalitaka kufanya maamuzi yatakayokuwa na mafungamano ya kisheria na hasa katika kipindi hiki cha janga.

Watu tisa wenye ulemavu na maradhi yanayowaweka kwenye kundi la watu walio hatarini kuathirika kirahisi na COVID-19 waliwasilisha madai ya kikatiba kutokana na hofu ya kutengwa na madaktari iwapo hakutakuwa na sheria sahihi.

Nchini Uingereza, waziri wa afya Sajid Javid amesema bado kuna kiza kinene kinachozunguka ukweli kuhusu kirusi cha corona cha omicron na kukiri kwamba kinasambaa kwa haraka mno hali inayotishia sekta ya afya nchini humo.

"Bado kuna sintofahamu kubwa kuhusu kirusi hiki, kinakua kwa kasi. Tunahisi labda asilimia 90 ya visa hivi kote Uingereza ni vya omicron. Inakuonyesha jinsi kinavyoenea haraka. Tumesikia hivi karibuni kwamba dalili zake ni za kawaida. Lakini hiyo pekee si habari njema inayojitosheleza. Sote tunapaswa kuwa waangalifu kabisa. Hatudhani kama kuna haja ya hatua zaidi hadi mwaka mpya lakini bila shaka tutakuwa tukitathmini." alisema Javid.

Soma Zaidi:Mechi zaidi zafutwa Premier League ya England

USA | New Orleans CDC genehmigt Pfizer-Impfstoff für Jugendliche
CDC nchini Marekani imepunguza muda wa kukaa karantini kwa baadhi ya makundi nchini humoPicha: Kathleen Flynn/REUTERS

Nchini Marekani, mamlaka zimetangaza jana kupunguza muda wa kukaa karantini kwawatu wasioonyesha dalili za maambukizi kutoka siku 10 hadi 5. Kituo cha kupambana na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza CDC kimesema kwa kuzingatia ushahidi wa awali, wale walioambukizwa virusi vya corona walikuwa na uwezo mkubwa wa kuambukiza wengine katika siku mbili kabla na siku tatu baada ya kuanza kuonyesha dalili.

CDC pia imerekebisha kipindi cha karantini kilichopendekezwa kwa watu waliokaribiana na walioambukizwa COVID-19 na ambao hawajachanjwa au ambao wanatakiwa kupatiwa chanjo ya nyongeza lakini bado hawajapata chanjo hiyo. Watu hao sasa watatakiwa kukaa karantini kwa siku tano na kuvaa barakoa wakati wote katika siku tano za baada ya karantini

Barani Asia, kumeshuhudiwa ongezeko la maambukizi nchini China na hasa katika mji wa Xian. Mji huo sasa umefungwa. China imeripoti visa vipya 162, wakati Hong Kong ikisitisha safari za ndege za shirika la Korea Air kwa wiki mbili baada ya abiria wa ndege hiyo kutoka Korea Kusini kukutwa na maambukizi wiki iliyopita.

Mashirika: DW/DPAE