1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu asema Magufuli amehamishiwa India akiugua Covid-19

11 Machi 2021

Kiongozi mkuu wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, amesema Alhamisi kuwa rais John Magufuli, ambaye hajaonekana hadharani kwa karibu wiki mbili, yuko India akitibiwa virusi vya corona na kwamba yuko katika hali mbaya.

https://p.dw.com/p/3qV0I
Bildkombo Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli und Tundu Lissu

Tundu Lissu, ambaye alishindwa na Magufuli kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana, ametaja duru za kiafya na usalama kama vyanzo vya taarifa kwamba rais Magufuli amehamishwa kutoka hospitali nchini Kenya na kupelekwa India akiwa hali mahututi - lakini hakutoa ushahidi.

Wasemaji wa serikali ya Tanzania wamesalia kimya wakati uvumi ukienea kuhusu uwepo wa rais Magufuli mwenye umri wa miaka 61 pamoja na hali yake ya kiafya. Wawakilishi wa serikali za Kenya na India waliotafutwa na shirika la habari la Reuters hawakutoa taarifa pia.

Akiwa madarakani tangu 2015 na kupewa jina la utani la "Bulldozer," Magufuli alionekana kwa mara ya mwisho Februari 27 akiwa mwenye afya njema wakati wa hafla katika ikulu ya rais mjini Dar es Salaam.

Lissu aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Magufuli alipelekwa kwenye hospitali ya nchini Kenya mwanzoni mwa wiki hii na kisha mahala pasipojulikana nchini India. "Amezimia tangu jana asubuhi," aliiambia Reuters bila kutoa ufafanuzi.

Tansania Wahlen Präsident John Pombe Magufuli
Magufuli akisalimiana na makamu wake Samia Hassan Suluhu.Picha: Tanzania State House Press/REUTERS

Gazeti la Nation la nchini Kenya lilinukuu duru zisizotambulishwa za kisiasa na kidiplomasia siku ya Jumatano zikisema kwamba kiongozi wa Kiafrica, ambaye halikumtaja, alikuwa akitibiwa Covid-19 na akipumua kwa msaada wa mashine katika hospitali ya Nairobi.

Wawakilishi wa hospitali waliiambia Reuters hawakuwa na taarifa za kutoa. Mkurugenzi wa mawasiliano wa rais Magufuli Gerson Msigwa na msemaji wa serikali Hassan Abbas hawajajibu ujumbe wa Reuters kuzungumzia suala hilo. Wizara ya mambo ya nje ya India na ubalozi wake mjini Nairobi pia haukuwa na la kusema.

Ukanushaji wa Covid watatukatatuka

Magufuli amepuuza kitisho cha Covid-19, akisema Mungu na tiba za nyumbani kama vile kujifukiza vingewalinda Watanzania. Alivikejeli vipimo vya virusi vya corona, kukosoa chanjo akiitaja kuwa sehemu ya njama ya mataifa ya magharibi kuchukuwa utajiri wa Afrika, na alipinga uvaaji wa barakoa na watu kutotangamana kwa ukaribu.

Maoni ya Watanzania juu ya Covid 19 na chanjo yake

"Ukanushaji wake wa Covid-19 umetatukatatuka, kukumbatia kwake sala tu na kupuuza sayansi kumemgeukia," alisema Lissu katika ujumbe wa Twitter mapema Alhamisi.

Soma pia: Corona: Rais Magufuli awaomba watanzania kufunga na kuomba

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, makamu wa rais Samia Suluhu Hassan atachukua hatamu za uongozi kwa kipindi kilichosalia kwenye muhula wa miaka mitano ikiwa rais hawezi kutekeleza majukumu yake.

Tanzania iliacha kutoa takwimu kuhusu virusi vya corona Mei mwaka jana, wakati iliposema kwamba ilikuwa na visa 509 na vifo 21, kwa mujibu wa data zilizopo kwenye shirika la afya duniani WHO.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika Matshidiso Moeti aliuambia mkutano wa waandishi habari siku ya Alhamisi kwamba hana taarifa za moja kwa moja kuhusu afya ya rais Magufuli na kwamba haitakuwa busara kuvumisha. Amebainisha kwamba Tanzania sasa imetambua hatari ya Covid-19 kufuatia vifo vya maafisa wawili wa juu serikalini, na kusema data zaidi kutoka nchini humo zinakaribishwa.

"Vyovyote ilivyo kuhusu rais Magufuli, tunaweza tu kumtakia vema iwapo taarifa hizi zina ukweli, na tunakariri utayarifu wetu kuisadia serikali na watu wa Tanzania," alisema.

Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Rais Maguli akila kiapo kuongoza muhula wa pili baada ya kuchaguliwa tena Oktoba 2020, ambapo alimshinda mgombea wa Chama cha Democrasia na Maendeleo CHADEMA, Tundu Lissu. Lissu anadai Magufuli ni mgonjwa mahututi.Picha: Tanzania Presidential Press Service

Magufuli, profesa wa zamani wa kemia kutoka kijiji cha Chato kaskazini-magharibi mwa Tanzania, alipanda haraka ngazi ya kisiasa baada ya kushinda kiti cha ubunge mwaka 1995. Magufuli aliechaguliwa rais mwaka 2015, amekabiliwa na tuhuma kutoka mataifa ya magharibi na vyama vya upinzani kwa kukandamiza demokrasia, madai ambayo anayakanusha.

Picha za televisheni zilimuonyesha Magufuli Januari 8 akimshukuru mwanadiplomasia wa juu wa China Wang Yi kwa kuja bila barakoa kukutana naye wakati wa ziara yake barani Afrika. Magufuli alisema hilo lilionyesha kwamba waziri huyo alikuwa akifahamu kuwa Tanzania haina Covid-19 na aliendelea kupeana naye mkono mbele ya kamera wakati wawili hao wakitabasamu. Maafisa wengine wa China waliokuwepo walivaa barakoa.

Chanzo: Reuters