1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Rais Magufuli awaomba watanzania kufunga na kuomba

Admin.WagnerD17 Aprili 2020

Rais John Magufuli wa Tanzania amewataka Watanzania kuanzia leo Ijumaa kutenga muda wa siku tatu hadi Jumapili kufanya maombi maamulu kwa ajili ya kudhibiti virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3b3oB
Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Picha: DW/E. Boniphace

Hii ni mara ya kwanza tangu janga hilo kupiga hodi katika nchi za Afrika kwa kiongozi wa nchi kutaka wananchi wake kutenga muda wa siku hizo kwa ajili ya kufanya maombi dhidi ya Corona. 

Rais Magufuli katika ujumbe aliotuma kwa njia ya akaunti yake ya Twiter amesema Watanzania watenga muda wa siku tatu kwa ajili ya dua na sala zao kwa Mwenyezi Mungu ilia apate kuliepusha taifa na jango hilo la Corona lilipiga hodi kwa mara ya kwanza nchini Machi 16, na hadi sasa watu 94 wamethibitishwa kuambukizwa.

Rais Magufuli mara kwa mara amekuwa akiwataka Watanzania kuendelea kumtegemea Mungu katika janga hili, lakini kauli yake ya kutaka watu watenge muda wa siku tatu kwa ajili ya maombi maalumu ameitoa kwa mara ya kwanza.

Mwishoni mwa wiki wakati akishiriki Ibada ya Ijumaa Kuu, Rais Magufuli alisema maombi yanaweza kulivusha taifa katika janga hili.

Tansania Polizei Verstärkung in Ohio
Jeshi la polisi nchini humo limewachara bakora watu hao na hata baa nyingine zililazika kufungwa.Picha: DW/E.Boniphace

Katika hatua nyingine, jeshi la polisi kwa mara ya kwanza jana usiku limeendesha msako kwenye baa na sehemu za starehe na kuwacharaza bakora wale iliyowakuta wakiburudika katika maeneo hayo.

Baa kadhaa hasa zile maarufu zililazimika kufungwa na haijaeleweka kama zitaendelea kufungwa au la na serikali hadi sasa haijatangaza kama baa zote zinapaswa kufungwa.

Wakati hayo yakiwa hivyo, Waziri wa afya Ummy Mwalimu ametangaza mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kipindi cha siku 20. Mkakati huo umepangwa kufanyika katika jiji la Dar es salaam eneo ambalo limekuwamba zaidi na maambukizi ya virusi vya Corona.

Nalo Kanisa katoliki likienda sambamba na mwito wa serikali wa kupunguza misongamano katika maeneo ya ibada, limetangaza kusitisha mazoezi ya uimbaji wa kwaya na limewataka pia, waendeshaji wa shughuli za ibada kuzingatia umbali wa muumini moja na mwingine.

Mwandishi: George Njogopa