1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Kim atarajiwa kukutana na Putin nchini Urusi

5 Septemba 2023

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anapanga kuelekea Urusi mwezi huu kukutana na Rais Vladimir Putin ili kujadili uwezekano wa kupeana silaha. Hayo ni kulingana na jarida la Marekani la New York Times.

https://p.dw.com/p/4Vy8W
Russland Nordkorea Gipfel in Wladiwostok | Kim Jong Un und Putin
Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Likinukuu vyanzo kutoka Marekani na washirika wake, gazeti hilo limeripoti jana Jumatatu kuwa katika safari hiyo adimu nje ya nchi, Kim anatarajiwa kusafiri kutoka Pyongyang kwa kutumia treni ya kivita hadi huko Vladivostok, kwenye Pwani ya Pasifiki ya Urusi, ambapo atakutana na Putin.

Msemaji wa baraza la usalama wa kitaifa wa Marekani John Kirby alisema Agosti 30 kwamba Marekani ilikuwa na wasiwasi kuhusu hatua chanya iliyofikiwa katika mazungumzo ya kupeana silaha kati ya nchi hizo mbili, na ziara hiyo inayotarajiwa ya Kim itajiri baada ya Urusi kubaini kuwa inalenga kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Korea Kaskazini.

Nordkorea Training Abschuss von Raketen
Jaribio la makombora la Korea Kaskazini lililofanywa tarehe 10.03.2023Picha: KCNA via Reuters

Huko Vladivostok, mji wa bandari usio mbali na Korea Kaskazini, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili kuhusu hatua ya Kim kutuma silaha kwa Urusi ikiwa ni pamoja na makombora ya kisasa huku Moscow ikiipatia Pyogyang ujuzi wa teknolojia  ya satelaiti na nyambizi zinazotumia nguvu za nyuklia.

Hata hivyo siku ya Jumanne, Ikulu ya Kremlin imekataa kuelezea chochote kuhusu ziara hiyo inayotarajiwa ya Kim kama ilivyoripotiwa na Jarida hilo la New York Times.

Soma pia: Marekani yasema Kim atarajia kukutana na Putin

Baba wa Kim, hayati Kim Jong Il ambaye aliepuka kusafiri kwa ndege na kutumia mara kadhaa treni ya kivita yenye uwezo wa kuzuia mashambulizi, aliitembelea Urusi mnamo mwaka 2011, miezi michache kabla ya kifo chake.

Urusi kuimarisha uhusiano wake na Korea Kaskazini

Russland Nordkorea Gipfel in Wladiwostok | Kim Jong Un und Putin
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (kushoto) akiwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin walipokutana Aprili 25,2019 huko Wladiwostok.Picha: Kremlin Pool/Russian Look/picture alliance

Shirika la habari la Interfax limemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu ambaye alifanya ziara nchini Korea Kaskazini mwezi Julai, akisema hapo jana kuwa hakuna anayechagua majirani zake na kwamba ni bora kuishi na majirani zako kwa amani na maelewano.

Wiki iliyopita, Ikulu ya Kremlin iliweka bayana kuwa inakusudia kuimarisha kile ilichokiita "mahusiano yenye heshima" na Korea Kaskazini ambayo ni moja wa washirika wake wa enzi za vita baridi na moja ya nchi zinazounga mkono uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Soma pia: Marekani yaionya Korea Kaskazini dhidi ya kuiuzia silaha Urusi

Mara kadhaa Korea Kaskazini imekuwa ikikanusha kuwa na mpango wa kubadilishana silaha na Urusi. Lakini hivi majuzi Marekani iliyawekea vikwazo mashirika matatu yanayoshutumiwa kuhusishwa na mikataba ya silaha kati ya Korea Kaskazini na Urusi.

Pyongyang imefanya majaribio sita ya nyuklia tangu mwaka 2006 na imekuwa ikifanya majaribio ya makombora mbalimbali katika miaka ya hivi karibuni lakini imekuwa ni nadra kufanya luteka ya kijeshi na majirani zake.

Kwa upande mwingine, Marekani na mshirika wake, Korea Kusini wamekuwa mara kadhaa wakifanya mazoezi ya kijeshi ambayo Korea Kaskazini inashutumu kuwa tishio na maandalizi ya vita dhidi yake.